TAHADHARI YA UGONJWA WA NIMONIA INAYOTOKANA NA CORONA VIRUS
Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, imepokea taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo
tarehe 22 Mei 2013, kuhusu kuwepo kwa ugonjwa wa Nimonia unaosababishwa
na kirusi cha “Novel Coronavirus”.Taarifa hiyo inaeleza kuwa,tangu
ugonjwa huo utokee mwishoni wa mwaka 2012 hadi tarehe 23 Mei 2013 idadi
ya wagonjwa wapatao 44 na vifo 22 viliripotiwa
Shirika la Afya
Duniani limethibitisha ugonjwa huu kuwepo katika nchi za Mashariki ya
Kati yaani Jordan, Qatar, Saudi Arabi na Falme za Kiarabu (UAE). Katika
bara la Ulaya, ugonjwa huu umethibitishwa kutokea nchi za Ujerumani,
Ufaransa, na Uingereza. Katika bara la Afrika, ugonjwa huu umetokea
Tunisia.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa tahadhari
ya Ugonjwa huu kwa wananchi wote, katika mikoa yote ya Tanzania na hasa
wale wanaosafiri kuelekea maeneo tajwa yenye uthibitisho wa ugonjwa huu.
Ugonjwa
huu unaenezwa na kirusi kiitwacho “novel coronavirus (nCoV).”. Dalili
kuu za ugonjwa huu ni kushindwa kupumua kwa ghafla, homa kali, kukohoa,
na kubanwa na mbavu na hatimaye kupata Nimonia. Dalili nyingine ambazo
zinaweza kutokea ni pamoja na kupata maumivu makali ya tumbo pamoja na
kuharisha.Vile vile ugonjwa huu unaweza kupelekea figo kushindwa kufanya
kazi na hata kusababisha kifo. Kipindi cha kuonekana kwa dalili za
ugonjwa huu
ni kati ya siku 2 hadi 10 baada ya kupata maambukizi. Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo.
Ugonjwa
huu unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Njia
za maambukizo bado hazijajulikana ingawa uwezekano mkubwa wa maambukizo
ni kwa kwa njia ya hewa (kukohoa/kupiga chafya) au kwa kugusa
majimaji/makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa
huo.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imechukua hatua zifuatazo katika kukabiliana na tishio la ugonjwa huu:
Kutoa
taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa Waganga Wakuu wote wa
Mikoa na Wilaya kwa Tanzania bara. Aidha, taarifa hii pia imejumuisha
namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa (Ainisho la Ugonjwa), “Fact sheet”
ya ugonjwa, Mwongozo kwa watumishi wa afya wa namna ya kuchukua sampuli
ikiwa ni pamoja na vipeperushi vinavyoelezea jinsi ya kujikinga na
maambukizi ya ugonjwa huu.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huu
kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya
mipakani. Aidha watalaamu hawa pia wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu
dalili za ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga na maambukizi ili endapo
ugonjwa huo utatokea uweze kutolewa taarifa mapema.
Wizara
inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili kwa
wasafiri watakaokwenda au kurudi katika maeneo tajwa yaliyothibitishwa
kuwa na ugonjwa huu. Vipeperushi vya ugonjwa huu vimetumwa katika maeneo
ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na
dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua
stahili ziweze kuchukuliwa.
Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na
mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya
ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana
Kupeleka vifaa kinga kwa ajili ya watumishi wa afya
Wananchi
wanashauriwa kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyeripotiwa nchini. Wizara inapenda kutoa tahadhari kwa wananchi juu
ya umuhimu wa KUNAWA MIKONO VIZURI KWA SABUNI NA MAJI MARA KWA
MARA na pia KUZUIA MDOMO NA PUA KWA KITAMBAA AU KARATASI LAINI WAKATI WA
KUKOHOA AU KUPIGA CHAFYA.
Pia wananchi wanashauriwa kutoa
taarifa kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu mara
watakapoona mgonjwa yeyote atakayehisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na;
Nsachris Mwamwaja
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
30/05/2013
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa