Dar es Salaam. Mkuu wa Kitengo cha Usalama wa Chadema,Wilfred Lwakatare jana alikamatwa, akahojiwa na kupekuliwa na polisi kwa tuhuma za uchochezi wa uvunjifu wa amani.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso aliliambia Mwananchi jana kuwa Lwakatare alikamatwa kutokana na taarifa zilizopatikana kutoka katika video kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwahamasisha watu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani au uhalifu. Alipoulizwa mahali na lini alikamatwa Lwakatare, Senso alisema hilo halijalishi, lakini jambo la msingi ni kwamba wako naye kwa ajili ya uchunguzi na hakutaka kuweka bayana ni lini wangemwachia.
Siku nzima ya jana mitandao ilikuwa imetawaliwa na habari ya picha ya video ikimwonyesha Lwakatare akidaiwa kupanga mikakati ya kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky. Lwakatare alionekana akitoa maelekezo kwa watu, ambao sura zao hazikuonekana, akiwataka kufuatilia nyendo za Msacky.
Alionyeshwa akiwataka watu hao kumkamata bila ya kumdhuru Msacky, lakini wamtupe mbali kama njia ya kumnyamazisha. Alikuwa anamtuhumu Msacky kama alikuwa anashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ili kukihujumu chama chao.
“Inabidi mfahamu nyendo za mtu huyu, kama anapenda vitu kama kutembea usiku au kinywaji anachokunywa,” alinukuliwa kwenye mtandao huo.
Pia anaonekana kwenye video hiyo akitoa mbinu mbalimbali za namna ya kufanya utekaji nyara.
Wakili wa Lwakatare alonga
Wakati akihojiwa na kupekuliwa, Lwakatare aliongozana na wakili wa kujitegemea, Nyaronyo Kicheere, ambaye alilieleza Mwananchi kuwa mteja wake alichukuliwa kutoka ofisini kwake kwenye Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kicheere alidai kuwa hakuwa na uhakika kuwa Lwakatare alikamatwa muda gani ofisini kwake kwani yeye aliitwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi saa 9.00 alasiri.Mwananchi, hata hivyo, lina taarifa kuwa Lwakatare alikamatwa na askari wanne saa 7.00 mchana na kupelekwa Makao Makuu ya Polisi.
Lwakatare, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini kupitia CUF na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alipokamatwa alifuatana na maofisa kadhaa wa Chadema akiwamo Ofisa wa Ulinzi wa chama hicho, Hemed Sabula na Ofisa wa Mawasiliano aliyejulikana kwa jina moja tu la Karungebe.
Alichukuliwa ndani ya gari aina ya Land Cruiser na kupelekwa moja kwa moja Makao Makuu ya Jeshi la Polisi katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Mahojiano
Kicheere alisema Lwakatare alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi ingawa alidai polisi hawakubainisha ni uchochezi upi.
Mahojiano hayo kwa Lwakatare yaliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Obadia Jonas.
“Lwakatare alihojiwa kuanzia saa 9.00 alasiri hadi 9.55 jioni na tuhuma zilizomkabili ni uchochezi. Ila askari hawakuniambia ni uchochezi upi,” alieleza Kicheere. Alisema kuwa baada ya mahojiano yale waliamriwa kwenda nyumbani kwa Lwakatare kwa ajili ya upekuzi.
Upekuzi
Lwakatare, ambaye anaishi eneo la Kimara King’ong’o jijini Dar es Salaam, alisindikizwa na askari saba walioongozwa na ACP Jonas. Katika msafara huo wa kwenda kupekua nyumbani kwake, maofisa wa Chadema walizuiwa kuongozana naye, isipokuwa mwanasheria wake, Kicheere, ndiye aliruhusiwa kuongozana naye.
“Tunavyoongea na wewe hivi sasa ni kwamba upekuzi unaendelea katika vyumba vya nyumba . Kwa sasa tuko ndani ya chumba chake cha kulala,” alieleza Kicheere.
Kicheere alisema upekuzi huo ulianza saa 10.30 jioni na ulilenga katika kutafuta nyaraka ambazo zingeweza kutumika kama ushahidi wa tuhuma hizo. Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa upekuzi kilichokuwa kinatakiwa kufuata ni kuandikisha maelezo katika Kituo cha Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
“Hawa jamaa wanaendelea na upekuzi na hawajapata kitu chochote muda huu tunavyoongea na wewe. Ila tukimaliza tutarudi Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuandikisha maelezo,” aliongeza Kicheere.
Dk Slaa anena
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema polisi walifika katika ofisi za chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam na kuomba kuzungumza na Lwakatare.
chanzo gazeti la mwananchi
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa