Nini tafsiri ya ushindi mdogo wa uchaguzi wa rais kwa Kenya na changamoto za aina gani zinamkabili rais mpya anaetuhumiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa vita
Mbinu za Uhuru Kenyatta zimeleta tija. Mtoto huyo wa baba wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta, alishirikiana katika uchaguzi huu na hasimu yake mkubwa, William Ruto. Kiroja cha matokeo ya uchaguzi huo ni kwamba wanasiasa wote hao wawili wanatuhumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Wanatuhumiwa kuwachochea wafuasi wao wafanye fujo baada ya uchaguzi wa mwaka 2007,ambapo zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha yao na malaki kuyapa kisogo maskani yao.
Kawaida Wakenya huwapigia kura watu wanaotokana na makabila yao. Na safari hii wamefanya hivyo hivyo. Mipango ya vyama iliwekwa nyuma. Wakenya wengi wanafaidika kutokana na ile hali kwamba watawala hadi wakati huu wakiwatanguliza mbele watu wa makabila yao na kuwapatia nyadhifa muhimu za kiuchumi na kisiasa. Kenyatta ni kiongozi wa kisiasa wa watu wa kabila la kikuyu-kabila kubwa kabisa nchini humo. Makamo wake katika kuania wadhifa wa rais William Ruto ni wa kabila la Kalenjin-kabila la nne kwa ukubwa nchini Kenya. Katika muungano wa Jubilee,"Uhuruto"-kama wanasiasa hao wawili wanavyoitwa nchini Kenya,walishirikiana kuwazinduwa wafuasi wao. Kwa namna hiyo walitaka kumzuwia mgombea wapili mkuu wa kiti cha urais, Raila Odinga ambae ni wa kabila la Luo asishinde.
Hii ilikuwa mara ya tatu kwa Raila Odinga kugombea kiti cha urais.Kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa mwaka 2007,na safari hii pia anahisi kumefanyika udanganyifu - anataka kwenda mahakamani ili kubisha uhalali wa matokeo ya uchaguzi. La muhimu kwa sasa ni kwa mahakama ya katika kushughulikia dhana za udanganyifu na kuhakikisha kila upande unayatambua matokeo ya uchaguzi.Utulivu na Umoja wa taifa hilo la mchanganyiko wa makabila tofauti ndio kipa umbele uli amani ipate kuimarishwa nchini humo.
Kauli mbiu isalie kuwa Harambee
Kenyatta ni rais wa nne na kijana zaidi wa Kenya.Sio peke yao wakenya wanamkodolea macho,bali ulimwengu mzima unachunguza,nini kitatokea. Kenyatta anabidi adhihirishe kwamba yeye si rais wa watu wa kabila lake tu,bali rais wa wakenya wote. Anabidi autunze ushirikiano wake pamoja na William Ruto,na kuendeleza mageuzi - kama ilivyotajwa katika katiba. Muhimu zaidi ni kuvifanyia mageuzi vikosi vya polisi vinavyotuhumiwa kuhusika na visa vibaya kabisa vinavyokiuka haki za binaadam na ambavyo hadi sasa havikuandamwa kisheria.
Ushindi wa Kenyatta,mwenye umri wa miaka 51,aliyesomea uchumi katika chuo kikuu mashuhuri kabisa cha Amherst nchini Marekani, unaweza kuzusha madhara ya kidiplomasia na kiuchumi kwa nchi hiyo. Mwakilishi wa serikali kuu ya Ujerumani anaeshughulikia masuala ya Afrika, Günter Nooke amesisitiza hadi hukmu itakapotolewa, Kenyatta sawa na wote wengine wanaotuhumiwa na mahakama kuu ya kimataifa,wanasalia hawana hatia. Kesi yao ambayo awali ilikuwa ifanyike mwezi ujao wa April imeakhirishwa, ya Ruto itasikilizwa Mai na ya Kenyatta mwezi wa July. Wakihukumiwa, basi jambo hilo linaweza kuitumbukiza katika hali ya mtafaruku, nchi hiyo inayotegemea sana utalii.
Kenya ni muhimu kwa utulivu wa eneo lote, kutokana na mpaka wake mrefu pamoja na Somalia, inaangaliwa kama ngome ya mapambano dhidi ya wanamgambo wa kiislam wa Al Shabab. Kenya inaweza kujikuta katika hali kama ile ya Sudan. Sudan n nchi pekee ambayo rais wake anasakwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu.
Mbali na kesi dhidi ya Kenyatta na Ruto,suala la dhulma katika kugawanywa ardhi ni tatizo jengine kubwa linalomkabili rais huyo mpya. Katika miezi iliyopita, mapigano yaliripuka na damu kumwagika kwasababu ya ardhi. Ukoo wa Kenyatta unamiliki,mbali na makampuni makubwa makubwa ya kutengeneza maziwa,hoteli za kifahari,vyombo vya habari, benki na ardhi kubwa kupita kiasi.Kenyatta itabidi adhihirishe kwamba yeye ni rais wa wakenya wote. Hofu za watu wa makabila mengine ni kubwa. Kwa wafuasi wake Kenyatta ni shujaa.Kwa wengine yeye ni kitambulisho cha wasomi waliobobea kwa rushwa nchini humo.
Hivi sasa kwa mara nyengine tena kauli mbiu inabidi iwe Harambee - kama ilivyohanikiza miaka 50 iliyopita, nchi hiyo ilipojipatia uhuru.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa