Translate in your language

Thursday, November 1, 2012

Sinodi yawatema vigogo Kanisa la Moravian

BAADA ya kutokea vuta nikuvute kati ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki na uongozi wa juu wa jimbo hilo, hatimaye Mkutano Mkuu wa Sinodi umebariki kuondolewa madarakani viongozi waliosimamishwa akiwemo Mwenyekiti wa jimbo hilo, Mchungaji Clement Fumbo.


Mkutano huo pia umebariki kuondolewa madarakani Mweka Hazina aliyesimamishwa Mchungaji Ambilikila Lwaga na kuagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake kutokana na matumizi mabaya ya fedha za kanisa hilo.


Akizungumza na gazeti hili, mjumbe wa Halmashauri Kuu ambaye alihudhuria mkutano huo (jina tunalo), ambao ulifanyika mjini Morogoro, alithibitisha kutolewa kwa maamuzi hayo mazito na Sinodi ili kulinda taratibu za uendeshaji wa kanisa hilo.


Hatua hiyo imefikiwa baada ya sakata la mgogoro ndani ya kanisa hilo lenye Makao Makuu yake jijini Dar es Salaam, kuzua vuta nikuvute tangu lilipoibuliwa Aprili mwaka huu.


Sakata hilo liliibua sura mpya baada ya baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya kanisa hilo kufichua siri kuwa mgogoro huo ulichangiwa na matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha na upotevu wa mali za kanisa vikiwemo vyerehani 10, jenereta, kamera na  upuzwaaji mkubwa wa vikao vya kanisa.





Vyanzo vya kuaminika vilidai kuwa, vitendo hivyo ambavyo vilikuwa vikikiuka kanuni na taratibu za kanisa hilo, vilikuwa vinafanywa na Mchungaji Fumbo.

Hata hivyo, mara zote Mchungaji Fumbo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari, pamoja na kukiri kuwepo kwa mgogoro huo, alidai wapo watu wachache wenye nia ya kutaka kuliharibu kanisa hilo kwa masilahi yao binafsi.


Taarifa kutoka Morogoro zinadai kuwa, mkutano huo wa Sinodi ulibaini pasipo shaka ukosefu wa maadili na upuuzwaji wa maelekezo ya uendeshaji wa kanisa.


Hali hiyo ilisababisha kupotea au kutumiwa vibaya kwa fedha za kanisa na baadhi ya mali zilizokuwa katika Ushariki wa Ukonga, kupotea hivyo kufikia uamuzi wa kumuondoa madarakani Mchungaji Fumbo na wenzake.


Wakizungumzia ukiukwaji wa kanuni, wajumbe waliohudhuria Sinodi hiyo walisema Mchungaji Fumbo alitiwa kitanzini kwa kukaidi agizo la vikao vyote vya kanisa na Sinodi la kumtaka kumuondoa kwenye nafasi yake Mweka Hazina wa kanisa hilo kutokana na kukosa sifa.


“Sinodi ilishauri basi kama tunataka Mweka Hazina aliyepo aendelee kuwepo, tumpeleke akasome lakini Mchungaji Fumbo aligoma,” kilisema chanzo hicho.


Inaelezwa kuwa, vikao halali pia viliagiza kuajiriwa kwa Mkaguzi wa Ndani, lakini Mchungaji Fumbo alikataa kwa madai yasiyo ya msingi pamoja na kukiuka maazimio halali ya kanisa yaliyofikiwa katika vikao vya juu.


Baadhi ya waumini waliozungumza na gazeti hili baada ya maamuzi hayo walisema hatua hiyo itasaidia kurejesha amani na utulivu ndani ya kanisa hilo katika Jimbo la Misheni Mashariki ambalo lipo mbioni kuwa jimbo kamili baadaye mwaka huu.


toka gazeti la majira 

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)