Translate in your language

Friday, October 19, 2012

VURUGU ZA DAR ES SALAAM



HALI ya jiji la Dar es Salaam  imeweza kuwa tete kwa muda wa masaa kadhaa kufuatia baadhi ya wanaodaiwa kuwa waumini wa taasisi za dini za kiislamu kushinikiza kuandamana kwenda Ikulu kudai haki mbalimbali hapa nchini ikiwemo kushinikiza kuachiwa huru Shehe Ponda wa taasisi hizo.
Hali tete hiyo ilianza majira ya mchana mara baada ya ibada ya waumini hao wakitoka msikitini na ndipo vurugu ilipoanza hasa katika msikiti wa Mtoro uliopo Kariakoo.
Hata hivyo awali, waumini wao kwa wao  walitofautiana na muda mfupi Polisi ilipofika hali  ilikuwa tete na kuwa uwanja wa mapambano baada ya kundi la watu linalosadikiwa kuwa ni la Kiislamu kusababisha vurugu baina yao na askari polisi katika eneo la Kariakoo.
**
Vurugu hizo zimekuja kufuatia kundi hilo la waislamu lilipokuwa likikaidi agizo la polisi la kutojihusisha na maandamano, yaliyoanzia katika Msikiti wa Mtoro kutaka kuelekea Ikulu, ndipo ilipoanza tafrani hiyo, ambapo vikosi vya polisi wa kutuliza ghasia (FFU)waliwatawanya kwa maji ya kuwasha sambamba na mabomu ya machozi.
Tanzania Daima ilishuhudia tukio hilo ambalo lilizua tafrani kubwa iliyopelekea wasiwasi mkubwa kwa wananchi hususani wafanyabiashara wa eneo hilo, ambao walilazimika kusitisha shughuli zao kuhofia usalama wao.
Aidha,baada ya askari polisi kuonekana kuzidiwa nguvu na waandamaji hao, kutokana kurushiwa mawe, ndipo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lililokuwa na magari yapatayo 10 yaliyojaa askari wakiwa na silaha kuingilia kati ili kunusuru hali hiyo.
Kwa upande wa waandamaji hao walisikika wakisema kuwa,lengo lao ni kufikisha malalamiko yao kwa Rais Jakaya Kikwete,ili yatafutiwe ufumbuzi wa haraka.
"Hapatakuwa na amani, labda tuonane na Mkuu wa nchi, polisi wakifanikiwa kutuzuia leo lazima ijumaa ijayo Oktoba 26 tuandamane kama dhamira yetu tulivyokusudia" alisema Juma Othuman.
Wafanyabiashara wanazungumziaje
Wakati vurugu hizo zikiendelea, liliibuka kundi la wafanyabiashara katika eneo hilo likilaani kitendo hicho kinachofanywa na kundi la waislamu kuwa ni cha kikatili kwa sababu, mbali na kuondoa amani ya nchi lakini kinapandikiza chuki baina ya wakristo na waislamu.
"Tunaelezwa kuwa Tanzania ni nchi ya amani, hakuna amani nakataa kwa haya tunayoyaona na kuyashuhudia amani imetoweka, mimi dada unavyoniona ni muislamu halisi lakini nina wasiwasi na hali ya nchi inavyoelekea" alisema Fadhili Mohameid.



No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)