Translate in your language
Sunday, August 26, 2012
ZOEZI LA SENSA KUANZA LEO
SENSA ya Watu na Makazi inaanza leo kote nchini na itadumu kwa siku saba, katika mpango unaotarajiwa kutoa takwimu za idadi ya watu na makazi utakaoisaidia Serikali kupanga uwiano wa kimaendeleo kulingana na maeneo nchini.
Sensa hiyo inafanyika huku Jeshi la Polisi likitoa onyo kali dhidi ya watu wachache waliojitokeza waziwazi kupinga mkakati huo kufanyika kwa ufanisi.
Hata hivyo, hadi jana jioni taarifa zilizopatikana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, zinaonyesha hali kuwa shwari huku maofisa watakaosimamia mpango huo wakiwa kwenye harakati za mwisho za kuanza kazi hiyo.
Hata hivyo, Ofisa wa Uhamasishaji Sensa Taifa, Said Ameir aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa mpango wa sensa ulianza jana usiku jijini Dar es Salaam kwa kuchukua takwimu za watu kwenye maeneo wanayokaa watu wasio na makazi maalumu.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni Uwanja wa Ndege, vituo vya mabasi na treni.
Alisema kuwa jana walikamilisha mkakati wa kugawa vifaa maeneo mengi nchini licha ya kuwepo matatizo ya hapa na pale kutokana na mawasiliano mabaya ya barabara.
Hata hivyo, Ameir alisema kuwa ingawa matangazo yanaonyesha sensa kufanyika kwa siku saba, lakini wameazimia kumaliza kazi hiyo ndani ya siku tatu au nne.
Kuhusu kuwapo baadhi ya watu na vikundi vinavyopinga sensa, Ofisa wa Uhamasishaji huyo alisema kuwa habari hizo wanazo lakini akasema watu hao ni wachache.
Hata hivyo, alisema kuwa ofisi yake itaendelea kuhamasisha ili watu wote washiriki sensa na kwamba anaamini watafanya hivyo.
"Ingawa wanasema ni Waislamu wote hawatashiriki, lakini hiyo siyo kweli, ni wachache. Mimi ni Mwislamu na nahamasisha watu wakiwamo Waislamu wenzangu washiriki sensa," alisema Ameir.
Wakati hayo yakiendelea, viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi, jana waliendelea kuhimiza watu kujiandaa kuhesabiwa kwa kuhakikisha wanajibu maswali yote ya makarani wa sensa kwa ufasaha.
Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jana iliendelea kuwahimiza Wazanzibari kushiriki sensa kufuatia baadhi ya watu kutishia kususia zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika leo nchi nzima.
Baadhi ya wananchi wamesema kuwa watashirikiana na SMZ kuhakikisha sensa hiyo inafanikiwa, licha ya watu wengine kuanza kutoa vitisho kwa watakaoshiriki.
Songea
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkirikiti jana alikionya kikundi cha watu waliopanga kupita misikitini kuzuia watu wasihesabiwe akieleza kuwa watachukuliwa hatua kali.
Alisema kuwa ametoa kauli hiyo kutokana na taarifa za kuwapo kwa kikundi cha watu hao akiwataka wananchi wasikubali kuwasikiliza kwani nao watachukuliwa hatua za kisheria.
Arusha
Maofisa wa Serikali jana walifanikisha mpango wa kuipatia kitoweo cha pundamilia 12 Jamii ya Wahadzabe walio katika Pori la Eyasi wilayani Karatu ili wajitokeze kuandikishwa katika la sensa.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana, Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha, Margreth Martin alisema tayari vifaa vyote vimesambazwa maeneo husika kufanikisha zoezi hilo.
Alisema ofisi yake imetoa Sh5 milioni, ili kuwezesha uwindaji wa Pundamilia hao 12 na watasambazwa katika vituo 12 vya Wahadzabe.
Kigoma
Mkakati wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika leo huenda ukaingia dosari kutokana na makarani wa Sensa katika baadhi ya vituo kukataa kula kiapo mbele ya hakimu.
Wakizungumza kutoka katika Kituo cha Nguruka kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma baadhi ya makarani walisema kuwa wamekataa kula kiapo mbele ya hakimu kwa vile bado hawajalipwa sehemu ya posho zao za semina waliyofanya.
Serengeti
Baadhi ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji wameapa kutokuwapa ushirikiano makarani wa sensa ikiwa hawatalipwa posho kwa madai kuwa wawatumie madiwani waliopata semina na posho.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara umebaini kuwapo kwa mgomo huo, huku baadhi ya maeneo wenyeviti wakidai hawako tayari kuongozana na makarani wa sensa kwa sababu hawajawahi kupewa semina wala kulipwa kwa kazi hiyo.
Mratibu wa Sensa Wilaya ya Serengeti, Martine Mlelema alikiri kuwapo tatizo hilo lakini akasema tayari wamelipatia ufumbuzi na watatoa ushirikano.
Moshi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amewataka wakazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, kushiriki sensa ili kufanikisha Serikali kupanga mikakati ya kimaendeleo yao.
Gama aliyasema hayo usiku wa kuamkia jana katika tamasha la burudani la Fiesta linalofanyika kila mwaka, ambapo aliwataka wananchi wake kujiandaa vizuri pamoja na kuwapa ushirikiano mawakala wa Sensa ya Watu na Makazi.
Mtwara
Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi wa Mkoa wa Mtwara, Simon Semindu alisema kuwa mipango ya uendeshaji sensa mkoani humo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 95.
“Fedha zote tumetuma kwa kila wilaya," alisema mratibu huyo.
Tabora
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tabora, Hussein Bashe alisema mgomo wa baadhi ya Waislamu kutaka kugomea zoezi la sensa ni matokeo ya viongozi wa chama chake kuanza kuusemea na kuutumia udini.
Akizungumza na viongozi wa kata na matawi katika Kata za Wela, Miguha na Mbogwe, Bashe alisema kwamba kuibuka kwa mgomo wenye sura ya udini katika zoezi hilo kunaanza kudhihirisha kuibuka kwa udini nchini na kuonya kuwa jambo hilo ni hatari likiachwa kuendelea.
“Niwaombe ndugu zangu Waislamu, hii sensa haihesabu kutafuta Imamu au Sheikh, haitafuti Imamu, ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Tujitokeze kushiriki sensa kwani wanaotushawishi kuigomea hawa ni wadini na wanapandikiza mbegu mbaya ya udini tuwakatae,” alisisitiza Bashe.
Tanga
Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alisema anaamini zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litafanyika kwa ufanisi kwa kuwa maandalizi yamekamilika katika wilaya zote.
"Ninaamini zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mkoa wote wa Tanga litafanyika kwa ufanisi kwa kuwa tayari maandalizi yameshakamilika," alisema Gallawa.
Habari hii imeandikwa na Peter Saramba na Mussa Juma - Arusha, Anthony Kayanda - Kigoma, Herieth Makwetta - Moshi,
Burhani Yakub- Tanga. Frederick Katulanda - Mwanza, Anthony Mayunga - Serengeti, Abdallah Bakari - Mtwara, Joyce Joliga - Songea Salma Said na Talib Ussi - Zanzibar.
kwa msaada wa gazeti la mwananchi
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa