Translate in your language

Wednesday, April 16, 2014

UMUHIMU WA KUSHIRIKISHA JAMII KATIKA UIMARISHAJI WA AFYA NA USAFI KATIKA MAENEO YAO

UMUHIMU WA KUSHIRIKISHA JAMII KATIKA UIMARISHAJI WA AFYA NA USAFI KATIKA MAENEO YAO
Eneo la mafunzo: Lugono, wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro
Imeandaliwa na Othman R. Masanga kutoka QI presentation kuchimba dawa katika kikao cha tatu cha kuboresha huduma za afya Tanzania, tarehe 27 novemba 2013, Mlimani conf centre

Tatizo la maeneo/vituo yanayotumika na abiria kwa kushuka na kupata mahitaji yao, kwa mfano:- kujisaidia (kuchimba dawa), vyakula na huduma za simu limekuwa tatizo na kukua siku hadi siku.
Tanzania bara ina sehemu/vituo vingi kwa abiria, wafanyakazi na waendesha magari makubwa ya mizigo na mabasi kusimama na kupata mahitaji yao pembezoni mwa barabara kubwa ziendazo mikoani, sehemu zisizo na maeneo, vifaa na faragha kwa ajili ya kujisaidia na kupelekea uchafuzi wa mazingira wa maeneo husika na usambaaji wa magonjwa kwa wasafiri na wenyeji kwa ujumla.
Lugono ni moja ya sehemu inayotumika kwa wasafiri kupata mahitaji yao kama kuchimba dawa na vyakula, ipo umbali wa kilomita 25 toka morogoro mjini na kulingana na taarifa za mkoa wa morogoro mwaka 2010 eneo hilo lilikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, lakini pia eneo limekuwa na hatari kwa wasafiri kugongwa na nyoka kwasababu watu walikuwa wakiingia porini na vichakani kutafuta usiri wakati wakijisaidia.
Kwa kuona tatizo ofisi ya afya mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wadau wengine waliona umuhimu na kufanya yafuatayo:-
*      Kuhamasisha jamii iliyo katika eneo hilo kushiriki katika ujenzi wa vyoo bora vitakavyokuwa na maji, vifaa maalum vya kunawia mikono na usiri
*      Upatikanaji wa vyakula safi na salama kwa wasafiri na wenyeji wa eneo hilo
*      Kuimarisha ujasiriamali kwa vijana na jamii kwa ujumla katika eneo hilo
Njia zilizotumika:-
*      Afisa Afya walitumia shughuli za mpango wa uboreshaji wa huduma za afya na tiba za VVU/UKIMWI kuondoa tatizo la uharibifu wa mazingira eneo la Lugono
*      Afisa Afya kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji walifanya ukaguzi wa kimazingira kujua ukubwa wa tatizo husika

*      Kushirikisha jamii kwa ujumla kugundua na kutambua tatizo husika, kuweka vipaumbele, kuunda mipango kazi na utekelezaji wake
*      Wataalamu wa afya walitoa elimu juu ya usafi wa mazingira, magonjwa ya maambukizi ili kuwajenga kifikra wanajamii juu ya tatizo lililo mbele yao
*      Uhamasishaji wa jamii kushiriki katika mpango wa uboreshaji wa afya na mazingira kwa kutumia viongozi wa kisisasa katika eneo hilo na timu ya afya mkoa

     katika picha hapo juu ni  viongozi katika nyadhifa zao wakiwa katika mikutano ya kuhamasisha jamii kushiriki kwa pamoja kukabiliana na tatizo lililo mbele yao
 


Hali iliyokuwepo kabla ya ukamilishaji wa mpango huo kama inavyoonekana katika picha:-
wanafunzi wakipata mahitaji ya vyakula walipokuwa katika ziara yao kwenda mikumi kuangalia wanyama pori huku kukiwa na lundo la taka karibu na eneo la vyakula 

vyakula vikiandaliwa katika mazingira machafu ambayo ni chanzo cha magonjwa ya matumbo kwa walaji  

waandaaji wa nyama choma wakiwa hawana sare za kazi 
Matokeo baada ya uhamasishaji:
Jamii ilichangia milioni ishirini (TShs 20,000,000/=) kwa kuuza mifugo na mazao kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika eneo hilo.  Vyoo vilijengwa kwa awamu mbili tofauti, choo cha kwanza kikiwa na vyumba 14 vya kujisaidia na baada ya mwaka kilijengwa kingine chenye idadi ya kama hio
) Eneo la nje la jengo la choo bora 
Eneo la ndani la choo cha awamu ya pili kikiendelea na ujenzi 

*      Jamii ilichangia vifaa vya ujenzi vinavyopatikana katika eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa sehemu za kuuzia vyakula, matunda na maji
Matunda yakiwa yamepangwa juu ya vichanja na utunzaji mzuri wa takataka katika ndoo za plastiki 
*      Pia Mkuu wa Wilaya alitoa ahadi ya kuchimba kisima kurahisisha upatikanaji wa maji katika eneo hilo baada ya kuridhika na uwajibikaji wa jamii husika
*      Sehemu 2 za kuchinjia wanyama zikiwa na paa zilijengwa
*      Zaidi ya watu 120 wamejiajiri katika eneo hilo kuanzia mwezi aprili/2013 na Kipato kwa siku kimeongezeka kati ya TShs 20,000-30,000 na kiwango cha chini kikiwa ni TShs 10,000 
Kundi la vijana waliojiajiri wakiwa na sare zilizopendeza na safi 

*      Mbuzi na kondoo wamefikia 25-30, ambao huchinjwa kila siku ikilinganishwa na kondoo na mbuzi 10 tu kabla ya mradi huo
*      Kwa sasa nyama hukaguliwa kabla ya kuliwa na Mganga wa mifugo ili kulinda afya za walaji kutokana na magonjwa ya maambukizi toka kwa mnyama kwenda kwa binadamu tofauti na hapo awali. Kuanzia mwezi septemba 2012 hadi oktoba 2013 minofu ya mbuzi na kondoo 660 (15%)  waligunduliwa kuwa na vimelea vya TB na minofu ya mbuzi 3 walipelekea kukatazwa kuliwa na kutupwa kutokana na kutofaa kuliwa na binadamu 
Afisa mifugo akikagua nyama kabla ya kuthibitishwa kuwa salama kwa matumizi ya binadamu 

Nyama iliyokutwa na vimelea vya ugonjwa wa TB

*      Hali ya afya na kimazingira imeimalika na kuwa safi na rafiki kwa wasafiri, madereva na jamii inayopatikana eneo hilo
Wasafiri wakipata mlo katika mazingira safi na salama 

Eneo la kunawia mikono ikiwa na sabuni ya maji 


Changamoto zinazojitokeza:-

*      Ongezeko la wasafiri na watalii wanaohitaji huduma katika eneo hilo isiyolingana na uwezo wa kuwahudumia wote kwa pamoja
*      Upungufu wa maji yasiyopatikana kwa wakati wote wa kazi  
*      Kuwa na eneo pungufu la kuegeshea magari kulingana na watumiaji kuongezeka siku hadi siku
            



No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)