VIJANA WAPIKIWA UGALI KAMA WAFUNGWA WA KEKO
Picha juu.> Baadhi ya wenyeviti wa UV-CCM kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania bara na visiwani ambao wapo kambi mkoani Iringa katika eneo la Ihemi wakijiandalia chakula nje ya kambi hiyo baada ya kususia kambi hiyo kwa muda kwa madai ya mazingira machafu
Na Mwanablog wetu Iringa
KAMBI ya wiki moja ya viongozi wa jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UV-CCM) Taifa ambayo imeanza jana katika chuo cha vijana Ihemi katika wilaya ya Iringa vijijini limemeguka baada ya baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo kutoka mikoa mbali mbali kugomea kambi hiyo kwa muda.
Akizungumza n kwa niaba ya wenzake mwenyekiti wa UV -CCM wilaya ya Muweza mkoani Tanga Sufian Mwedy alkisema kuwa kambi hiyo ni kwa ajili ya semina ya mwenyeviti wa wilaya na makatibu wa wilaya pamoja na wenyeviti na makatibu kutoka Tanzania Bara na visiwani na kuwa kimsingi kambi hiyo imeandaliwa chini ya kiwango na ndio sababu ya wao kususia kambi hiyo.
Alisema kuwa wameshangazwa na kamati ya maandalizi ya semina hiyo kwa viongozi hao wa vijana kushindwa kuwaandalia chakula safi pamoja na mazingira mazuri ya kufikia wakati maandalizi ya semina hiyo yalikuwepo kwa kitambo kirefu.
Alisema kuwa waliingia kambini Ihemi toka juzi jioni ila baada ya kufika katika eneo hilo la kambi ya vijana kwa ajili ya semina walikuta hali ya mazingira ya kambi hiyo ikiwa katika hali mbaya na hivyo kulazimika kuondoka katika kambi hiyo ili kwenda kujitegemea wenyewe wakiwa nje ya kambi
Mwedy alisema kuwa pamoja na kuwa sehemu ya kulala ilikuwa haijaandaliwa vya kutosha na kulazimika baadhi yao kulala bila kujifunika ila bado huduma ya chakula walichoandaliwa kambini hapo kilikuwa si chakula cha kuliwa na binadamu kutokana na ubora wa hali ya chini ambao chakula hicho kilikuwa kimeandaliwa.
"Kweli jambo la kusikitisha katika kambi yetu hata huduma ya vyoo vilivyopo vipo ila havina maji ....ila hata daktari wa kambi hayupo na huku kambini hapo ni mbali na hospitali ya mkoa wa Iringa"
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na kuwa kambi hiyo ni kwa ajili ya mafunzo kwa viongozi wa wilaya na kambi ambayo itaenda sambamba na baraza kuu la vijana Taifa ila kambi hilo linaonyesha kuwa ni moja ya sehemu ya kuigawa jumuiya hiyo kutokana jinsi ambavyo viongozi hao walivyojipendelea kwa kuishi katika hoteli za kisasa mjini Iringa huku viongozi wa ngazi za chini wakiishi kwa shida kambini Ihemi.
"Sipindi viongozi wa juu wa mikoa na Taifa kulala mjini ila napingana na hatua ya wao kupitia mjini moja kwa moja na kulala huko bila hata kujua mazingira ya kambi yaliopo huku....hapa ndipo tunapojiuliza hivi vijana tutaanza kujigawa hivi hadi lini"alihoji
Hata hivyo kwa upande wake baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa umoja huo ambao hata hivyo hawakupenda kutajwa magazetini walisema kuwa hatua ya kususia kambi kwa viongozi hao kuna mambo mengi ambayo wamekwazika nayo likiwemo la mwenyekiti wa CCM Taifa , Rais Jakaya Kikwete kushindwa kufika kufungua baraza hilo na badala yake kumtuma katibu mkuu wa CCM.
Kwani walisema hadi sasa wamepatwa na bumbuwazi baada ya kusikia mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Kikwete haji mkoani Iringa kufungua kambi hiyo wakati taarifa za awali zilionyesha yeye ndie angekuwa mgeni rasmi.
Pamoja na hilo pia walihoji sababu ya wahusika wa kambi hiyo kushindwa kuandaa mapema kambi hiyo na badala yake kufanya kazi ya zima moto dakika za mwisho ikiwa ni pamoja na uongozi wa wilaya ya Iringa kuanza kusembua barabara hiyo kuelekea chuoni kwa ajili ya ujio wa Rais Kikwete wakati chuo hicho kimekuwepo miaka yote bila barabara kutengenezwa.
Walisema kuwa moja ya mambo ambayo yamekuwa yakipelekea wapinzani kulalamika kuwa nguvu ya dola imekuwa ikitumika kutoa ushindi kwa CCM ni pamoja na hali kama hiyo ambayo inafanywa na viongozi wa serikali wa mkoa wa Iringa kwa kutegemeza miundo mbinu kwa ajili ya ziara za viongozi.
"Hivi kiukweli hata wewe kama mwandishi hebu jiulize hii barabara inayotengenezwa kuja huku chuoni Ihemi wakati huu bajeti yake inatoka wapi na mwanzoni walikuwa wapi kutegeneza"
Kuhusu kambi hiyo alisema kimsingi inatakiwa kufungwa kutokana na kukosa huduma nyeti kwa wanakambi hao japo kambi hiyo imechangiwa mamilioni ya shilingi na wadau mbali mbali.
Kwani alisema ni aibu kwa viongozi hao wa UV -CCM kuishi kambini hapo kwa kuomba chakula kutoka kwa majirani wa kambi hiyo wakati bajeti ya kuwaweka hapo ilitengwa siku nyingi.
Katibu wa UV -CCM mkoa wa Iringa Roda George aliulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na mapungufu hayo yaliyojitokeza katika kambi hiyo alisema kuwa kwa upande wake si msemaji mkuu wa kambi hiyo na kuwa anayeweza kujibia suala hilo ni katibu mkuu wa UV-CCM Taifa Martine Shigella na si mtu mwingine.
"Samahani mwandishi sikujua kama unaniitia hilo la vijana kususia kambi ...ukweli mimi sijui chochote na sio msemaji mkuu wa suala hili naomba uwasiliane na katibu mkuu nashukuru kweheri"alisema katibu huyo na kuondoka kabisa eneo hilo.
Kwa upande wake katibu mkuu huyo Shigella alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu hakuweza kupatikana huku mwenyekiti wake Hamad Yusuph Masauni akimwomba mwandishi wa habari hizi amtafute kesho (leo) jioni)
Kutokana na mvutano huo uliojitokeza katika kambi hiyo ya UV-CCM mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz pamoja na viongozi mbali mbali wa chama ngazi ya mkoa walilazimika kufika katika eneo hilo la kambi ili kujua undani wa sakata hilo .
Pamoja na viongozi hao pia askari kanzu walimwagwa katika eneo hilo la kambi ya vijana huku mwandishi wa habari hizi akifukuzwa eneo hilo la kambi kwa madai amefika bila utaratibu wao.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa