Monday, May 17, 2010

VITUKO VYA KAMBI YA WKI MOJA UVCCM-TAIFA

VIJANA WAPIKIWA UGALI KAMA WAFUNGWA WA KEKO

Picha  juu.> Baadhi ya wenyeviti  wa UV-CCM kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania bara na visiwani ambao  wapo kambi mkoani Iringa katika eneo la Ihemi  wakijiandalia chakula nje ya kambi hiyo baada ya kususia kambi hiyo kwa muda kwa madai ya mazingira machafu

Na Mwanablog wetu Iringa

KAMBI ya wiki moja ya  viongozi wa jumuiya ya  umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UV-CCM) Taifa ambayo imeanza jana katika chuo cha  vijana Ihemi katika wilaya ya Iringa vijijini limemeguka baada ya baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo kutoka mikoa mbali mbali  kugomea kambi  hiyo kwa muda.

Akizungumza n  kwa niaba ya wenzake mwenyekiti wa UV -CCM wilaya ya Muweza mkoani Tanga Sufian Mwedy  alkisema kuwa kambi hiyo ni kwa ajili ya semina ya mwenyeviti wa wilaya na makatibu wa wilaya pamoja na wenyeviti na makatibu kutoka Tanzania Bara na visiwani  na kuwa kimsingi kambi hiyo  imeandaliwa chini ya kiwango na ndio sababu ya wao kususia kambi hiyo.

Alisema kuwa  wameshangazwa na  kamati ya maandalizi ya semina  hiyo kwa viongozi hao wa vijana  kushindwa kuwaandalia chakula safi pamoja na mazingira mazuri ya  kufikia wakati maandalizi ya semina hiyo yalikuwepo kwa  kitambo kirefu.

Alisema kuwa  waliingia kambini Ihemi toka juzi jioni ila baada ya kufika katika  eneo hilo la kambi ya vijana kwa ajili ya semina  walikuta hali ya mazingira ya kambi hiyo ikiwa katika hali mbaya na hivyo kulazimika kuondoka katika kambi hiyo ili kwenda kujitegemea  wenyewe wakiwa nje ya kambi

Mwedy alisema kuwa  pamoja na kuwa sehemu ya kulala ilikuwa haijaandaliwa vya kutosha na kulazimika baadhi yao kulala bila kujifunika ila bado huduma ya chakula  walichoandaliwa kambini hapo  kilikuwa si chakula cha kuliwa na binadamu kutokana na ubora wa hali ya chini ambao chakula hicho kilikuwa kimeandaliwa.

"Kweli jambo la kusikitisha katika kambi yetu hata huduma ya vyoo vilivyopo vipo ila havina maji ....ila hata daktari wa kambi hayupo na huku kambini hapo ni mbali na hospitali ya mkoa wa Iringa"

Hata hivyo alisema kuwa  pamoja na kuwa kambi hiyo ni kwa ajili ya mafunzo kwa  viongozi wa wilaya na kambi ambayo itaenda sambamba na  baraza  kuu la vijana Taifa  ila kambi  hilo linaonyesha kuwa ni moja ya sehemu ya kuigawa jumuiya hiyo kutokana jinsi ambavyo  viongozi hao walivyojipendelea kwa kuishi katika hoteli za kisasa mjini Iringa huku viongozi wa ngazi za chini  wakiishi kwa shida kambini Ihemi.

"Sipindi viongozi wa juu wa mikoa na Taifa kulala mjini ila napingana na hatua ya wao kupitia mjini moja kwa moja na kulala huko bila hata kujua mazingira ya kambi yaliopo huku....hapa ndipo tunapojiuliza hivi vijana tutaanza  kujigawa hivi hadi lini"alihoji

Hata hivyo kwa upande wake  baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa umoja huo ambao hata hivyo hawakupenda  kutajwa magazetini walisema kuwa hatua ya kususia kambi kwa viongozi hao kuna mambo mengi ambayo wamekwazika nayo likiwemo la mwenyekiti wa CCM Taifa , Rais Jakaya Kikwete kushindwa kufika kufungua baraza hilo na badala yake kumtuma katibu mkuu wa CCM.

Kwani walisema hadi sasa  wamepatwa na bumbuwazi baada ya  kusikia mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Kikwete haji mkoani Iringa kufungua kambi  hiyo wakati taarifa za awali zilionyesha yeye ndie angekuwa mgeni rasmi.

Pamoja na  hilo pia walihoji sababu ya wahusika wa kambi hiyo kushindwa  kuandaa mapema kambi hiyo na badala yake  kufanya kazi ya zima moto dakika za mwisho ikiwa ni pamoja na uongozi wa wilaya ya Iringa  kuanza  kusembua barabara hiyo  kuelekea chuoni  kwa ajili ya ujio wa Rais Kikwete wakati chuo hicho kimekuwepo miaka yote bila barabara kutengenezwa.

Walisema kuwa moja ya mambo ambayo yamekuwa yakipelekea wapinzani kulalamika kuwa nguvu ya dola imekuwa ikitumika kutoa ushindi kwa CCM ni pamoja na hali kama hiyo ambayo inafanywa na viongozi wa serikali wa mkoa  wa Iringa kwa  kutegemeza miundo mbinu kwa ajili ya ziara za viongozi.

"Hivi kiukweli hata wewe kama mwandishi hebu jiulize hii barabara inayotengenezwa kuja huku chuoni Ihemi wakati huu bajeti yake inatoka wapi na mwanzoni walikuwa wapi  kutegeneza"

Kuhusu kambi  hiyo  alisema kimsingi inatakiwa  kufungwa  kutokana na kukosa huduma nyeti kwa wanakambi hao japo kambi hiyo imechangiwa mamilioni ya shilingi na wadau mbali mbali.

Kwani alisema ni aibu kwa viongozi hao wa UV -CCM kuishi kambini hapo kwa  kuomba chakula kutoka kwa majirani wa kambi  hiyo wakati  bajeti ya kuwaweka hapo ilitengwa siku nyingi.

Katibu wa UV -CCM mkoa wa Iringa Roda George aliulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na mapungufu hayo yaliyojitokeza katika kambi  hiyo alisema kuwa kwa upande wake si msemaji mkuu wa kambi  hiyo na kuwa anayeweza  kujibia suala hilo ni katibu mkuu wa UV-CCM Taifa Martine Shigella na si mtu mwingine.

"Samahani mwandishi sikujua kama unaniitia hilo la vijana  kususia kambi ...ukweli mimi sijui chochote na sio msemaji mkuu wa suala hili naomba uwasiliane na katibu mkuu nashukuru  kweheri"alisema katibu huyo na kuondoka kabisa eneo hilo.

Kwa upande wake katibu mkuu huyo Shigella alipotafutwa na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu hakuweza kupatikana huku mwenyekiti wake Hamad Yusuph Masauni akimwomba mwandishi wa habari hizi amtafute kesho (leo) jioni)

Kutokana na mvutano  huo uliojitokeza katika kambi hiyo ya UV-CCM mkuu wa mkoa wa Iringa Mohamed Abdulaziz  pamoja na viongozi mbali mbali wa chama ngazi ya mkoa walilazimika kufika katika eneo hilo la kambi ili kujua undani wa sakata hilo .

Pamoja na viongozi hao pia askari kanzu walimwagwa katika eneo hilo la kambi ya vijana huku mwandishi wa habari hizi akifukuzwa eneo hilo la kambi kwa madai amefika bila utaratibu wao.




No comments:

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa