Translate in your language

Thursday, March 11, 2010

KUCHINJWA KAMA KUKU

Kuchinjwa

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti Mkoani Singida,likiwemo la mfanyabiashara mmoja kuchinjwa kama kuku na kisha kunyang’anywa fedha taslimu shilingi 1,300,000/=.

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini hapa,Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani hapa,Ssp Peter Midelo alisema kwamba tukio hilo lilitokea march,04,mwaka huu saa tisa alasiri katika Kijiji cha Tyegelo,tarafa ya Kisiriri,wilayani Iramba.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa jeshi mfanyabiashara huyo Shimiti Juma (28) amechinjwa na kitu chenye ncha kali hadi akafariki dunia.

Aidha kaimu kamanda huyo kwamba siku ya tukio mfanyabiashara huyo akiwa na mwenzake Bwana Masanja Rashidi (27) walikuwa wakisafiri kwa kutumia usafiri wa baiskeli kwenda wilayani Igunga, Mkoani Tabora kwenda kununua bidhaa mbali mbali za dukani kwake.

Alitanabaisha kuwa watu hao walipofika kwenye eneo la tukio licha ya watu hao wasiofahamika kuwavamia watu hao,pamoja na kumchinja mfanyabiashara Shimiti,lakini walimwacha bila hata kumgusa Masanja Rashidi.

Aidha Midelo aliweka wazi kuwa kutokana na mauaji hayo mpaka sasa wanamshikilia Masanja Rashidi pamoja na Frank Emmanueli (41) mkazi wa Kijiji cha Kidaru, kuhusiana na mauaji hayo.

“Tuna wasi wasi na Masanja kwa sababu katika purukushani hiyo, yeye hajaguswa kabisa hata kidogo na ndiye aliyetoa taarifa ya kuuawa kwa Shimiti kwa kuchelewa sana ”alisisitiza kaimu kamanda huyo.


Katika tukio jingine, kamanda Midelo alimtaja mwanamke Kiya Masule (32) kuwa ameuawa kwa kupigwa kichwani na kitu kizito na kisha kufariki dunia papo hapo.

Kaimu kamanda huyo alifafanua kwamba  tukio hilo limetokea Machi,06,mwaka huu saa 11:00 jioni katika kijiji cha Kisanii, Tarafa ya Chikola,Wilayani Manyoni na kwamba marehemu Kiya pamoja na Magreth Maduka (29) walikuwa wemeolewa ukewenza na Tinde Pambe.

Kaimu Kamanda huyo alisema kufuatia tukio hilo wanamshikilia Magreth Maduka mke mwenza na marehemu Kiya kuhusiana na mauaji hayo.

Hata hivyo alisema jeshi hilo bado linaendelea kumsaka mume wa marehemu huyo kutokana na kumuhusisha na mauaji hayo  ambaye alitoroka mara tu baada ya tukio hilo .

Kwa mujibu wa Midelo uchunguzi wa awali unaonyesha wazi kwamba kwa kiasi kikubwa mauaji hayo yamechangiwa na wivu wa kimapenzi.

MWISHO.
 

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)