RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema serikali yake itaendelea kutekeleza mpango kazi wa kufikisha huduma za jamii vijijini kwa lengo la kufanikisha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa wananchi wake (Mkuza).
Dk. Shein alisema hayo jana baada ya kuizindua Shule ya Msingi Kidagoni, iliyopo Shehia ya Kidoti, Jimbo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema miongoni mwa huduma hizo ni za sekta ya elimu, afya, maji, umeme na nyinginezo ambazo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Alisema hayo yote yanawezekana iwapo wananchi wataanzisha miradi yao ya maendeleo na hatimaye serikali kuwaunga mkono.
Wakati huo huo, Dk. Shein alizindua SACCOS ya Potoa na kusifu juhudi zao wanazozichukua katika miradi mbalimbali wanayoiendesha zikiwamo ushonaji, ufumaji, uuzaji wa dagaa, kilimo na shughuli nyingine za maendeleo.
Aliwasifu kwa kuanzisha ofisi yao ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi na kufurahishwa na malengo waliyojiwekea ya muda mrefu katika kuikuza Saccos hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza watoto wao wakiwemo wanafunzi wa maeneo hayo.
Katika uzinduzi huo, Dk. Shein alifanya harambee ambapo viongozi mbalimbali walitoa ahadi na fedha taslimu sh milioni 6.3 huku Dk. Shein akichangia sh milioni 3.7.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, alisema ujenzi huo una azima ya kuanza utaratibu wa wanafunzi badala ya kufanya mitihani kwenye madarasa wafanye kwenye kumbi ili kuepuka mambo mbalimbali ya udanganyifu.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa