KLABU ya Simba imesema itawapeleka mahakamani mashabiki wake waliofanya vurugu na kupelekea uharibifu wa baadhi ya magari ya viongozi wa klabu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mashabiki wa Simba hawakuridhishwa na sare ya bao 1-1 waliyopita dhidi ya JKR Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili iliyopita.
Kufuatia kutoridhika na sare hiyo, mashabiki waliwarushia chupa za maji wachezaji wakati wakitoka uwanjani, na kisha baadaye kuyarushia mawe baadhi ya magari ya viongozi nje ya uwanja.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema jana kuwa, wanafanya uchunguzi kuwabaini mashabiki hao kabla ya kuchukua hatua za kisheria.
“Tunalaani tukio hili lililofanywa na mashabiki wetu, lakini pia tunafanya uchunguzi ili kuwabaini na baada ya hapo tutawafikisha mahakamani,” alisema Kamwaga.
“Kitendo cha wachezaji kufanyiwa fujo na magari ya viongozi kupasuliwa vioo, hakiwezi kamwe kuvuliwa,” aliongeza Kamwaga.Kamwaga alisema uongozi haujafurahishwa na matokeo hayo, na jambo la msingi ni kuonyesha uvumilivu badala ya kufanya vurugu.
“Tunafahamu kwenye soka siyo kila siku ushinde, kwani wakati mwingine ni lazima kukubali matokeo tofauti hata kama hayatafuraisha.”
Wakati huohuo, Sh73.5 milioni zimepatikana kwenye mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na JKT Ruvu uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Kiasi hicho cha pesa kinatokana na watazamaji 12,984 kuingia uwanja kwenye mchezo namba 99, ambapo kiingilio cha chini kilikuwa Sh5,000 na cha juu20,000.Baada ya makato, kila klabu iliondoka na Sh17.4 milioni, huku Mamlaka ya Mapato (TRA) ikichota Sh11.2 milioni.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja Sh8.8 milioni, tiketi Sh3.1 milioni, gharama za mechi Sh5.3 milioni, Kamati ya Ligi Sh5.3 milioni, Mfuko wa Maendeleo ya Soka (FDF) Sh2.6 milioni na Chama cha Soka Dar es Salaam (DRFA) Sh2. milioni.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa