Translate in your language

Monday, February 4, 2013

Samata, Ulimwengu watua jana, Eto`o leo


Mbwana Samatta
Nahodha wa timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto'o anatarajiwa kutua nchini leo kwa ajili ya kuiongoza timu yake katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji timu ya Tanzania (Taifa Stars) utakaofanyika keshokutwa jioni kwenye Uwanja wa Taifa.

Tayari nyota wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walishatua nchini jana saa 11:10 jioni na kujiunga na kambi ya Stars kwa ajili ya kuivaa Cameroon katika mechi hiyo ya kalenda ya kimataifa ya FIFA itakayoanza saa 11:00 jioni.
 
Mbali na Eto'o ambaye ni balozi la malaria, nyota wengine wa kikosi hicho maarufu Indomitable Lions watakaotua leo saa 3:45 asubuhi ni pamoja na Herve Tchami anayecheza Budapest ya Hungary, Nicolas Nkoulou (Marseille-Ufaransa), Jean Paul Yontcha (OS Olhanense-Ureno na daktari wa timu, Boubakary Sidik.
 
Taarifa ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ilisema kuwa kocha wa timu hiyo, Jean Paul Akono, atawasili leo saa 4: 40 akitokea Afrika Kusini alikokuwa akifuatilia fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazoendelea.
Wachezaji wengine watakaotua leo usiku ni pamoja na Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, Fabrice Olinga (Mallaga-Hispania), Allan Nyom (Udinese - Italia) na Henri Bedimo Montpellier ya Ufaransa.
 
Nyota wengine waliobaki akiwamo Alexandre Song wa Barcelona watatua jijini kesho na kukamilisha msafara wa watu 36, ambapo kati yao viongozi ni 12.
Kundi la kwanza la wachezaji wa Cameroon lilitarajiwa kutua nchini jana usiku wakati wenyeji wao wakiongozwa na kocha Kim Poulsen wanatarajia kuanza mazoezi leo baada ya kikosi kamili alichokiita kukamilika.
 
Wakati huo huo, waamuzi kutoka Rwanda wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiyo watakaochezesha mechi hiyo baina ya Stars na Cameroon.
Mwamuzi wa katikati atakuwa Munyemana Hudu wakati wasaidizi wake ni Simba Honore na Ndagizimana Theogine wakati mwamuzi wa mezani ambaye pia anatambuliwa na FIFA atakuwa Oden Mbaga wa Tanzania.
 
Hudu na wenzake watawasili nchini kesho (Februari 4 mwaka huu) saa 12.40 jioni kwa ndege ya RwandAir na wamepangiwa kufikia kwenye hoteli ya JB Belmont. Mechi ambayo ni moja kati ya nyingi zitakazochezwa siku hiyo (FIFA Date) itafanyika kuanzia saa 11 kamili jioni.
SOURCE: NIPASHE

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)