Hatimae kamati ya kusimamia mdahalo wa urais uliopangwa kufanyika usiku wa leo imewashirikisha wagombea wengine wawili waliokwenda mahakamani kuzuia mdahalo huo usifanyike.
Mjadala huo unaotokana na juhudi za vyombo vya habari nchini humo unatarajiwa kufuatiliwa na mamilioni ya watu ndani na nje ya mipaka ya Kenya kupitia pia njia za mitandao ya kijamii pamoja na magazeti, huku vituo vinane vya televisheni vituo 34 vya redio vikitegemewa kuutangaza moja kwa moja tukio hilo.
Kwa awamu hii ya kwanza, mdahalo huo utajikita kwenye masuala ya uongozi, huduma za kijamii, afya na elimu pamoja na usimamizi wa rasilimali bila ya kuliacha nyuma suala la usalama.
Wagombea wanane wa urais - Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Musalia Mudavadi, Martha Karua, Peter Kenneth James Ole Kiyiapi ,Paul Muite na Mohammed Dida- wanatarajiwa kupambana kujibu masuali na kujieleza juu ya walivyojiandaa kuyatatua matatizo ya Wakenya katika ajenda zitakazojadiliwa.
Watangazaji ambao watahusika kuwabana wagombea hao kujibu masuali yaliyoandaliwa na jopo maalum la waandalizi wa mdahalo huo ni Linus Kaikai kutoka kituo cha televisheni cha Nation na Julie Gichuru akiwa ni mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Citizen jijini Nairobi.
Mdahalo huo unatarajiwa kuanza saa 1:30 magharibi kwa saa za Afrika Mashariki katika ukumbi wa shule ya kimataifa ya Brookehouse jijini humo.
Uwezekano wa duru ya pili ya uchaguzi
Mdahalo huo unatarajiwa kufanyika katika wakati ambapo tafiti za maoni zilizofanywa na mashirika mbalimbali zikionesha kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 4 Machi yatakuwa ni ya kukaribiana kabisa, hasa kati ya wagombea wakuu wawili - Raila Odinga kutoka muungano wa CORD na Uhuru Kenyatta akishikilia bendera ya muungano wa Jubilee - huku ikitajwa kuweko uwezekano mkubwa wa kufanyika duru ya pili.
Kutokana na hayo, kwa hivyo, mdahalo unaofanyika leo unaweza kujenga au kubomoa ndoto za wagombea.
Kwa mujibu wa mashirika ya kukusanya maoni ya Ipsos Synovate na Infotrack wapiga kura ambao watafuatilia kwa makini zaidi mdahalo huo ni wale ambao hadi sasa hawajaamua ni nani anayestahili kupigiwa kura kuliongoza taifa hilo kubwa kiuchumi katika eneo la Afrika Mashariki.
Wadadisi wa mambo wanasema mdahalo huo wa kwanza kabisa kuwahi kufanyika nchi humo unaweza kuwa chachu muhimu kwa wapiga kura juu ya mtu wa kumpigia kura, ingawa mtazamo utakaojitokeza baada ya mdahalo juu ya vipi matokeo ya uchaguzi yanavyoweza kuwa ni suala litakalotegemea mambo mengi.
Lakini, juu ya hilo, wakati zikiwa zimesalia wiki tatu tu kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu na kukitarajiwa mdahalo wa pili tarehe 25 Februari, ni wazi mdahalo huo unaweza kabisa kuwashawishi wapiga kura wengi kujitokeza kuitafuta hatma ya nchi yao.
Mwandishi: Saumu Mwasimba - DW
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa