Wednesday, 15 August 2012 20:33 |
Waziri Kuvuli wa Fedha Zitto Kabwe wa Kambi ya Upinzani,akiwakilisha bajeti mbadala ya kambi hiyo Bungeni Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman
ZITTO ASEMA YUMO KIONGOZI WA JUU WA SERIKALI YA SASA,WENGINE NI WA AWAMU YA MKAPA, ATISHIA KUWAANIKA
Waandishi Wetu
TUHUMA kwamba baadhi ya vigogo Serikali wameficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi jana ziliibuka tena bungeni, huku Kambi ya Upinzani ikidai kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja ikiwa Serikali haitawataja.
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe aliitaka Serikali kuwataja kwa majina viongozi na wafanyabiashara wakubwa walioficha Sh315.5 bilioni nchini Uswisi, akisema kwamba watu hao "wanafahamika".
Juni mwaka huu, Benki Kuu ya Uswisi ilitoa taarifa inayoonyesha kuwapo kwa kiasi cha Sh315.5 bilioni zilizotoroshwa Tanzania na kufichwa nchini humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi bungeni jana, Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa wizara hiyo alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa Serikali za awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo.
"Kambi ya Upinzani bungeni imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya mawaziri wa awamu zilizopita ni miongoni mwa fedha hizi," alisema Zitto.
Pia aliitaka Serikali kuliambia taifa ni hatua gani itakazochukua kurejesha fedha hizo pia kuwataka wamiliki wake na kama ikishindwa, wao watawataja.
"Tunaitaka Serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa," alisema Zitto na kuongeza:
"Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha hizo iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi," alisisitiza.
Fedha hizo zinadaiwa kutokana na biashara (deals) zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kwenye Sekta za Nishati na Madini na kwamba sehemu kubwa ya fedha zililipwa na kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.
Baada ya Zitto kumaliza kuwasilisha hotuba yake, Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole-Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala hilo.
Sendeka alisema Zitto alisema miongoni mwa walioficha fedha hizo ni kiongozi wa juu wa Tanzania, lakini akashangaa Serikali kutohoji juu ya kauli hiyo.
"Mheshimiwa Naibu Spika, mheshimiwa Zitto amewatuhumu viongozi wa Serikali na kiongozi wa juu kabisa kuwa wameficha fedha Uswisi," alisema.
Alisema, lakini pamoja na tuhuma hizo, hakuna kiongozi wa Serikali aliyesimama na kutolea ufafanuzi hivyo akaomba mwongozi ili Zitto aruhusiwe kuwataja.
Sendeka alisema tuhuma hizo ni nzito na zimeichafua sura ya Serikali hivyo ni vyema ijulikane ni nani kati ya Serikali na Zitto atabeba mzigo wa kuwataja.
Naibu Spika, Job Ndugai alisema angetoa mwongozo huo baada ya kuipitia hotuba hiyo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuona kama ina matatizo. Hata hivyo, hakutoa mwongozo huo.
Oxford wabanwa Wakati huohuo, kambi hiyo rasmi ya upinzani imeitaka Serikali kuinyang'anya Kampuni ya Oxford University Press Tanzania (OUPTL), zabuni ya kuchapisha na kusambaza vitabu.
Zitto alisema kampuni hiyo imejihusisha kuwahonga maofisa wa Serikali katika kupata zabuni hiyo jambo linaloipotezea sifa kuendelea na zabuni hiyo.
Alisema Julai 3,2012 Benki ya Dunia ilitangaza kuifungia kampuni hiyo kutokana na vitendo vya rushwa ambavyo kampuni hiyo ilikiri kuhusika kwake.
Kampuni hiyo ilishinda zabuni ya kusambaza vitabu nchi za Afrika Mashariki katika miradi mbalimbali ya elimu iliyokuwa inafadhiliwa na Benki ya Dunia.
Alisema kampuni hiyo ilikiri kuhusika kuwahonga maofisa mbalimbali wa Serikali katika zabuni hiyo na kutakiwa kulipa benki hiyo Dola 500,000 za Marekani.
Kutokana na kukiri kwake huko, Mamlaka ya Ununuzi ya Umma ilitangaza kuifungia kampuni hiyo hapa nchini kwa kipindi cha miaka saba.
"Wakati ikifungiwa tayari tulishawapa zabuni ya kusambaza vitabu vilivyotokana na chenji ya rada ambazo ziliamuliwa kuwa zitaenda kununua vitabu," alisema.
Kambi hiyo imeitaka Serikali kuinyang'anya OUPTL zabuni hiyo ya kusambaza vitabu na badala yake kazi hiyo zipewe kampuni za ndani ya nchi.
Alisema tabia ya Serikali kufanya kazi na kampuni ambazo tayari zina dosari za kifisadi au kukiuka sheria inatoa picha mbaya kwenye uchumi.
Zitto alisema Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwachukulia hatua maofisa wote wa wizara waliohusika katika rushwa hiyo ya Oxford.
Ufisadi wa Sh70 bilioni Katika hatua nyingine Zitto alisema Serikali inatumia Sh70 bilioni kwa mwaka kulipa mishahara ya watumishi hewa fedha ambayo ingeweza kutumika kuwalipa walimu na madaktari na kumaliza migogo iliyopo.
Fedha hizo zinatosha kulipa mishara ya mwezi mmoja kwa walimu wa ngazi ya cheti wanaoanza kazi 286, 415 wanaokiwa kulipwa mshahara wa kiwango cha Sh244,400 kwa mwezi.
Zitto alisema Waziri wa Fedha na Uchumi alikiri mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi kwamba Februari mwaka huu Serikali ililipa jumla ya Sh5.1 bilioni zikiwa ni mishahara hewa.
"Hii ina maana kwamba Serikali hutumia zaidi ya Sh70 bilioni kwa mwaka kuwalipa mishahara watumishi hewa," alisema Zitto.
Alisema Waziri ausambaratishe mtandao huo wa wezi ili fedha wanazolipwa watumishi hewa zitumike kuwalipa walimu na madaktari kwa kuwa fedha hizo zinatosha kabisa kwa kazi hiyo.
"Siku zote Serikali imekuwa haitimizi matakwa ya wafanyakazi hasa kwenye sekta za afya na elimu kwa madai kwamba Serikali haina fedha wakati mabilioni hayo yanatumika kuwalipa watu wasiofanya kazi," alisema Zitto.
Akirejea taarifa ya Waziri wa Fedha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi ya Agosti 7, 2012, Zitto alisema uhakiki wa watumishi hewa uliofanyika Januari 2012 na kubaini majina 9,949 ya watumishi hewa kwenye halmashauri 133 na taasisi za Serikali 154.
"Idadi hii ya watumishi hewa ni sawa na idadi ya watumishi walioajiriwa katika sekta nzima ya madini kwenye migodi ya dhahabu hapa nchini," alisema Zitto.
Alisema watumishi hewa wanaokaribia 10,000 ni wengi na inaonyesha dhahiri namna Serikali isivyo makini katika suala ambalo linasababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Machi 31, 2009/10 inaonyesha kwamba Sh1.8 bilioni zililipwa kwa watumishi hewa.
Alisema, Waziri wa Fedha agawe taarifa za uhakiki wa wafanyakazi wa Serikali kwa wabunge na hatua zilizochukuliwa dhidi ya vinara wa mtandao huo wa watumishi hewa serikalini.
Sakata la rada Msemaji wa Kambi ya Upinzania katika Wizara ya Fedha, Zitto amesema mjadala wa rada bado mbichi na kwamba, Watanzania hawatauzima kwa kufurahia chenji iliyorudishwa na Waingereza.
Alisema wananchi wanataka kujua ni hasara kiasi gani imepatikana na hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya waliolitia hasara taifa.
"Umma unataka kufahamu ufisadi huu wa kimataifa umesababisha hasara gani na hatua stahiki za kisheria zilizochukuliwa dhidi ya wote walioliingizia taifa hasara," alisema.
Msemaji huyo alisema " Mjadala wa ununuzi wa rada hauwezi kuisha kwa kufurahia kurejeshewa chenji tu, mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka ukweli mtupu uelezwe bayana."
Alisema fedha za kununulia rada hiyo ambazo ni Dola za Marekani 40 milioni zilikopwa kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa riba ya asilimia 4.9.
"Kambi ya Upinzani inataka kufahamu kama mkopo huo umeshalipwa wote na jumla tulilipa kiasi gani cha fedha ikiwamo riba," alisema Zitto.
Mafuta yatafuna uchumi Msemaji huyo amesema fedha zote za kigeni zinazotokana na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani na korosho zinatumika kuagiza mafuta pekee yake.
Alisema hali hiyo ni mbaya kwa uchumi wa taifa kwani juhudi zote za taifa kuongeza mauzo ya nje zinaliwa na uagizaji wa mafuta ambao umepanda katika siku za hivi karibuni.
Alisema taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya dhahabu nje kwa mwaka 2011 yalikuwa kiasi cha Dola za Marekani 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7 ya mauzo yote nje, wakati mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa viwandani yalikuwa na jumla ya Dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4 ya mauzo yote ya nje.
Alisema mauzo ya mazao mbalimbali kama pamba, katani, korosho, chai, kahawa na mengineyo yalikuwa na thamani ya Dola 761.1 milioni kwa kipindi hicho cha mwaka 2012.
"Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa umeme wa dharura ambao umesababisha matumizi makubwa ya mafuta na takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inatumia zaidi ya Sh42 bilioni kila mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya umeme," alisema Zitto.
Habari hii imeandaliwa na Daniel Mjema na Habel Chidawali, Dodoma na Raymond Kaminyoge, Dar |
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa