Abubakar Marijani (50) maarufu kwa jina la Papaa Msofe pichani |
Papaa Msofe alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akimsomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai kuwa Novemba 6, 2011, mshtakiwa alimuua mfanyabiashara wa madini, Onesphory Kituli.
Tumaini alidai kuwa mauaji hayo aliyafanya nyumbani kwa marehemu Magomeni Mapipa, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili Kweka alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha Kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu, Sura ya 19 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
Hata hivyo, mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo inatazamiwa kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.
“Mshtakiwa hutakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hii haina uwezo wa kusikiliza mashauri ya mauaji,” alisema Hakimu wa Mahakama hiyo, Agnes Mchome baada ya Wakili Kweka kumaliza kumsomea shtaka hilo.
Wakili Kweka alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaiomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mchome aliamuru mshtakiwa arudishwe mahabusu hadi Agosti 23, mwaka huu wakati kesi hiyo itakapotajwa tena mahakamani hapo kwa kuwa shtaka linalomkabili halina dhamana.
Papaa Msofe alifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:30 asubuhi kwa kutumia gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi watatu, wawili kati yao wakiwa na silaha. Kwa siku kadhaa, mfanyabiashara huyo alikuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi Magomeni.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa hivi karibuni na jeshi la polisi Magomeni akituhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara mwenzake, marehemu Kituli.
Marehemu alikuwa akimiliki migodi Mererani, Arusha, na muda mrefu walikuwa na mgogoro wa kudaiana ambapo inadaiwa marehemu alikuwa anadaiwa na Papa Msofe Sh. milioni 30.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa