Kama utapenda kumsaidia Yusra piga simu namba 0715 773366
YUSRA RAJABU |
Na Florence Majani
JUZI, Agosti 8, mtoto Yusra Rajabu, ametimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwake. Kwa hakika, huu ni umri mdogo mno kimaisha.
Lakini, kwa masikitiko makubwa ni kuwa Yusra hakuweza kuisherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa mwenye furaha na afya kama wafanyavyo watoto wengine, na badala yake siku hiyo imemkuta akiwa amelazwa wodini Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Juma moja lililopita, madaktari waligundua kuwa Yusra ana saratani ya damu (leukemia). Maradhi hayo hushambulia chembe hai nyeupe za damu na kusababisha damu kukauka mara kwa mara huku mwili ukishambuliwa na maradhi kila uchao.
Mama mzazi wa Yusra, Asha Kondo anasema mtoto wake huyo alizaliwa akiwa mwenye afya tele kwani hakupata matatizo yeyote wakati alipozaliwa.
Alizaliwa akiwa na kilo nne na nusu, na hakukawia kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Afya ya Yusra haiendelea kuwa nzuri kwa muda mrefu, kwani akiwa na miezi mitatu tu, homa zilimwandama na hazikutaka kumwacha.
Maradhi hayo yamemfanya Yusra asiwe na makuzi kama ya watoto wengine kwani bado hajaanza kutembea kama iwapasavyo watoto wa umri wake.
“Haipiti wiki bila mtoto huyu kuugua homa, tunaitibu homa baada ya siku mbili tatu, anaanza kuumwa tena alitakiwa awe anatembea sasa, kwani alikwishaanza kutambaa lakini akaacha baada ya kuanza kuumwa,” anasema mama yake (Asha).
Anasema awali madaktari walihisi mambo mengi, wengine walisema mkojo mchafu, wengine walidai pengine ni homa ya ini, lakini bado afya ya Yusra haikutengamaa.
‘Ilichukua muda mrefu kugundua maradhi yanayomsumbua mtoto huyu, kila mtu alisema lake, kwa sababu homa hazikuwa zikimwacha,” anasema mzazi wake,
Anaongeza kuwa sema baada ya homa hizo kudumu kwa kipindi kirefu na kufikia hatua ya kulazwa mara kwa mara, tatizo jipya liliibuka. Tatizo hilo lilikuwa ni Yusra kukaukiwa damu.
“Baadaye akaanza kupungukiwa damu, na hilo lilijionyesha hata kwa nje, kwa sababu ngozi yake ya mwili ilikuwa na weupe usio wa kawaida, kucha na macho vilikuwa vyeupeee,” anasema
Anasema madaktari waliwapa vidonge vya kuongeza damu pamoja na ushauri wa kutumia mboga za majani na matunda kwa wingi, lakini hilo halikuwa suluhisho.
“Pamoja na dawa hizo, na matunda kwa wingi, bado hakupata nafuu. Zikipita siku mbili, tatu, anaanza kuumwa tena, akipimwa … damu hamna mwilini,” anasema
Familia hii iliendelea kuhangaika kwa muda mrefu huku hali ya Yusra ikiendelea kuwa mbaya, ilidhaniwa pengine ni homa ya ini na akapimwa lakini haikuwa hivyo.
Ilidhaniwa ugonjwa wa mapafu, lakini bado halikuwa tatizo hilo na madaktari walifanya juhudi za kupima chochote walichohisi bila kugundua tatizo.
Rufaa aliyopewa kwenda Muhimbili ilizaa matunda kwani madaktari bingwa wa watoto walishauri apimwe saratani ya damu na vipimo hivyo vilipopelekwa nje ya nchi, ikabainika kuwa kweli Yusra ana saratani ya damu.
“Hivyo ndivyo daktari alivyotueleza kuwa Yusra ana kansa ya damu, na amesema pengine ni ya kurithi,” anasema Asha
Mama huyu anajaribu kuvuta kumbukumbu, hata hivyo hakumbuki kuwepo mtu mwenye maradhi hayo iwe katika ukoo wake au wa mume wake.
Hata baada ya kuyafahamu maradhi hayo, changamoto kubwa ilikuja baada ya daktari kuwaeleza tiba inayofaa kutibu maradhi ya mtoto wao.
Asha, anasema daktari anayemtibu Yusra amewaeleza kuwa yusra anahitaji sindano maalum 12 kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.
Daktari huyo amesema kuwa sindano hizo kwa sasa hazipatikani nchini na zinatakiwa kuagizwa kutoka nje ya nchi na gharama ya sindano moja ni Shilingi 80,000.
“Ili apate nafuu anatakiwa achome sindano 12 na sindano moja ni Sh 80,000, hivyo ili akamilishe dozi ya kwanza anahitaji Sh960,000,” anasema kwa huzuni.
Anaeleza kuwa hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwake kama mama ambaye anahitaji kumwona binti yake akiwa na afya, lakini ni mtihani mkubwa zaidi kwa baba mzazi wa Yusra, Rajab Maulid ambaye kipato chake hakimwezeshi kugharimia matibabu hayo.
Rajab, anasema kipato chake kidogo kitokanacho na shughuli za ujenzi hakimwezeshi kugharimia matibabu hayo.
“Yusra ni mtoto wangu wa tatu, wengine wawili nao ni wakubwa na wanasoma, mke wangu ni mama wa nyumbani, hivyo familia yote hii inanitegemea mimi,” anasema
Anasongeza kuwa ni vigumu kwake kumudu kulipia sindano hizo ambazo Yusra anatakiwa kuchoma kila baada ya siku mbili.
“Kwa mfano, nikiweza kulipia sindano moja, nikashindwa nyingine ina maana afya ya Yusra itakuwa shakani,” anasema
Saratani ya damu ni nini?
Saratani ya damu au leukemia ni saratani inayoshambulia tishu za mwili zinazohusika na utengenezaji wa damu zikiwemo uboho katika mifupa (bone marrow) na mfumo wa lymph (lyphatic system).
Kuna aina mbalimbali za leukemia, nyingine zikiathiri watoto na nyingine zikiathiri zaidi watu wazima.
Kwa kawaida leukemia huanzia kwenye chembe nyeupe za damu yaani ‘white blood cells’, ambapo mwili huzalisha kiwango kikubwa cha seli zenye maumbo mabaya(abnormal) ambazo hazina uwezo wa kufanya kazi zake sawasawa.
Kazi ya chembe nyeupe za damu ni kulinda mwili dhidi ya vimelea waletao maradhi mbalimbali.
Leukemia husababishwa na nini?
Bado chanzo cha uhakika cha ugonjwa huu hakijajulikana lakini wanasayansi wanadai kuwa leukemia hutokea kutokana na sababu kadhaa ikiwemo sababu za vinasaba au kurithi.
Mambo ambayo yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya damu ni pamoja na kupata matibabu ya saratani hapo kabla, kutumia au kupigwa mionzi aidha kwa kufanya kazi katika viwanda vinavyowaweka karibu na mionzi au mabomu.
Sababu nyingine ni uvutaji sigara kwa kiasi kikubwa na kutumia kemikali za viwandani kwa mfano kemikali za kuyeyusha vyuma au kutengeneza magurudumu.
Wengine huipata kwa kurithi katika familia, iwapo mmoja wa wazazi wa mtu anayeugua saratani aliwahi kuugua saratani ya aina hii au kuwa na ndugu mwenye ugonjwa huu, basi ni rahisi kwa mtoto takayezaliwa kuwa na ‘leukemia’
CHANZO: MWANANCHI
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa