Translate in your language

Friday, June 8, 2012

Maandamano ya Waislam yapigwa ‘stop’



 Na Waandishi Wetu, \Gazeti la Mwananchi
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limezuia maandamano ya Shura ya Maimamu Tanzania yaliyopangwa Jijini la Dar es Salaam kupinga Baraza la Mitihani la taifa (Necta) kutokana na kasoro iliyojitokeza katika mtihani wa dini hiyo wa kidato cha sita mwaka 2012.
Maandamano hayo yalipangwa kuanzia sehemu mbalimbali za jiji hilo na kuishia viwanja vya Kidongo Chekundu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alisema jeshi hilo halioni sababu ya kufanyika kwa maandamano hayo badala yake amewataka wahusika kufanya  mkutano peke yake katika viwanja hivyo.
Alisema sababu za kusitisha maandamano hayo ni ugumu kwa jeshi la polisi kutoa ulinzi kwa sababu waumini wanatokea katika misikiti mbalimbali, hivyo wangeshindwa kuyadhibiti, endapo pangetokea vurugu.

Mapema, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliwataka wananchi kutoshiriki maandamano hayo kwa sababu suala walilokuwa wakilalamikia limeshafanyiwa kazi na Wizara pamoja na Necta.
“Kwa kuwa suala hili limeshapatiwa ufumbuzi, nawasihi wananchi wajiepushe na maandamano hayo kwa sababu suala la msingi lililowafanya watake kuandamana limeshatolewa maelezo. Hivyo maandamano hayo hayatakuwa na tija,” alisema Dk Kawambwa.
Dk Kawambwa mbali na kumpongeza Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako kwa kushughulikia tatizo hilo kwa wakati, alisema wizara itaunda tume ya kufuatilia suala hilo kwa undani ili lisijitokeze tena.
Baadhi ya wajumbe watakaounda tume hiyo, pamoja na idara nyingine watatoka Idara ya Elimu Sekondari, Baraza la Shule za Kiislam, Ukaguzi na Mjumbe kutoka katika idara inayotunga mitaala ya somo la Maarifa ya Uislam( Islamic Knowledge).
Alisisitiza kuwa, tatizo lililotokea ni kasoro za kibinadamu na halikulenga kundi lolote, kwa kuwa mfumo wa usahihishaji hauwezi kumpendelea mtu kwa namna yoyote ile.
Dk Ndalichako ambaye pia alikuwa katika mkutano huo wa waandishi wa habari, alisema mbali na kufanya uchunguzi juu ya somo la Maarifa ya Uislam, pia walitazama masomo mengine na kukuta yapo sawa.
Necta mwaka jana ilibadili utaratibu wa kufanya mitihani mitatu ya Maarifa ya Uislam na kuwa miwili, lakini mfumo wa kompyuta wa kujumlisha matokeo ukasahaulika.
Kauli ya waislamu
Awali, waislamu kupitia Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Sheikh Issa Ponda maandamano hayo walipanga kuandamana kupinga kile walichoita hujuma za Necta dhidi ya wanafunzi wa kiislamu nchini.
Juzi Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) lilimtaka Katibu Mkuu wa Necta, Dk Ndalichako ajiuzulu kufuatia kashfa hiyo.
Imeandikwa na Zaina Malongo, Fredy Azzah na Nora Damian

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)