Translate in your language

Saturday, September 3, 2011

Francis Cheka amkata maini Maugo



Bondia Mada Maugo aliyeinama akiweka mikono usoni kuzuia konde
 lililorushwa na Francis Cheka lisimpate wakati wa pambano lao
 lililofanyika juzi Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani
 Morogoro. Cheka alishinda kwa pointi.












Jaji 1
Cheka pointi 99
Maugo pointi 98

Jaji 2
Cheka pointi 100
Maugo pointi 98

Jaji 3
Cheka pointi 99
Maugo pointi 99

SOSTHENES NYONI, MOROGORO
BONDIA mahiri nchini,Francis Cheka ameendeleza ubabe wake baada ya kumnyuka 

mpinzani wake Mada Maugo kwa pointi katika pambano lao la raundi 10 la uzani wa
 middle lililofanyika juzi Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Awali mabondia hao walikutana ulingoni jijini Dar es Salaam mwezi Machi katika

 pambano ambalo pia Cheka alimdunda Maugo kwa pointi.

Tofauti na lile la awali, safari hii pambano baina ya wababe hao lilionekana kuwa

 na upinzani mkubwa pengine kutokana na maandalizi ya uhakika ya mabondia
 wote wawili na hivyo kuwafanya mashabiki washindwe kutabiri mshindi hadi pale
 majaji walipomtangaza Cheka.

Katika pambano hilo lililoanza majira ya saa 4 za usiku, mabondia hao walionekana

 kugawana vipindi, kwani katika raundi nne za mwanzo, Maugo alionekana mwiba
 mkali akimshushia makonde mazito mazito mpinzani wake kitendo kilichosababisha
 mashabiki waliojazana uwanjani hapo waanze kuguna wakiamini enzi za utawala wa
 Cheka zinabadilika.

Hali ya hewa ilianza kubadilika raundi ya tano baada ya Cheka kuanza kujibu

 mashambulizi akitumia mbinu ya kukaa mbali na Maugo aliyekuwa akitumia
 mbinu ya kurusha ngumi na kumkumbatia mpinzani wake na kumtungua ngumi 
za kudokoa na kuamsha shangwe miongoni mwa mashabiki wake waliofurika uwanjani hao.

Cheka aliendelea kutawala raundi ya sita na saba pamoja na ile ya nane kabla ya

 Maugo kurejea na nguvu mpya kurudisha mashambulizi katika raundi ya tisa na kumi
 za pambano hilo.

Kimsingi ushindi wa Cheka ulipatikana kwa Jaji namba moja Neema Kavisha pointi 99

 kwa Cheka dhidi ya 98 za Maugo wakati jaji namba mbili Boniface Wambura alitoa
 pointi 100 kwa Cheka na 98 kwa Maugo huku jaji wa tatu, George Sabuni akitoa pointi 
99 kwa Cheka na 99 kwa Maugo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya pambano hilo kumalizika, Cheka

 alijitapa kuwa alitegemea kupata ushindi licha ya kwamba aliamini pambano litakuwa
 gumu ambapo pia alimlaumu mpinzani wake kwa kumkumbatia mara kwa mara akisema 
aliharibu ladha ya mchezo, huku Maugo akiwalaumu majaji kwa kile akichodai hawakumtendea
 haki.

Hata hivyo pambano hilo nusura lisifanyike kutokana kile kilichoelezwa kuwa Cheka alipinga

 pambano hilo kuwa chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa(TPBC) wakati
 yeye akitaka Chama kingine cha masumbwi ya kulipwa (PST) ndio kichukue jukumu hilo,
 tukio ambalo lilichukua takribani dakika 30 kabla ya Cheka kukubali kupanda ulingoni baada
 ya kubembelezwa sana na waandaaji.

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)