Jaji 1 Cheka pointi 99 Maugo pointi 98 Jaji 2 Cheka pointi 100 Maugo pointi 98 Jaji 3 Cheka pointi 99 Maugo pointi 99 SOSTHENES NYONI, MOROGORO BONDIA mahiri nchini,Francis Cheka ameendeleza ubabe wake baada ya kumnyuka mpinzani wake Mada Maugo kwa pointi katika pambano lao la raundi 10 la uzani wa middle lililofanyika juzi Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Awali mabondia hao walikutana ulingoni jijini Dar es Salaam mwezi Machi katika pambano ambalo pia Cheka alimdunda Maugo kwa pointi. Tofauti na lile la awali, safari hii pambano baina ya wababe hao lilionekana kuwa na upinzani mkubwa pengine kutokana na maandalizi ya uhakika ya mabondia wote wawili na hivyo kuwafanya mashabiki washindwe kutabiri mshindi hadi pale majaji walipomtangaza Cheka. Katika pambano hilo lililoanza majira ya saa 4 za usiku, mabondia hao walionekana kugawana vipindi, kwani katika raundi nne za mwanzo, Maugo alionekana mwiba mkali akimshushia makonde mazito mazito mpinzani wake kitendo kilichosababisha mashabiki waliojazana uwanjani hapo waanze kuguna wakiamini enzi za utawala wa Cheka zinabadilika. Hali ya hewa ilianza kubadilika raundi ya tano baada ya Cheka kuanza kujibu mashambulizi akitumia mbinu ya kukaa mbali na Maugo aliyekuwa akitumia mbinu ya kurusha ngumi na kumkumbatia mpinzani wake na kumtungua ngumi za kudokoa na kuamsha shangwe miongoni mwa mashabiki wake waliofurika uwanjani hao. Cheka aliendelea kutawala raundi ya sita na saba pamoja na ile ya nane kabla ya Maugo kurejea na nguvu mpya kurudisha mashambulizi katika raundi ya tisa na kumi za pambano hilo. Kimsingi ushindi wa Cheka ulipatikana kwa Jaji namba moja Neema Kavisha pointi 99 kwa Cheka dhidi ya 98 za Maugo wakati jaji namba mbili Boniface Wambura alitoa pointi 100 kwa Cheka na 98 kwa Maugo huku jaji wa tatu, George Sabuni akitoa pointi 99 kwa Cheka na 99 kwa Maugo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya pambano hilo kumalizika, Cheka alijitapa kuwa alitegemea kupata ushindi licha ya kwamba aliamini pambano litakuwa gumu ambapo pia alimlaumu mpinzani wake kwa kumkumbatia mara kwa mara akisema aliharibu ladha ya mchezo, huku Maugo akiwalaumu majaji kwa kile akichodai hawakumtendea haki. Hata hivyo pambano hilo nusura lisifanyike kutokana kile kilichoelezwa kuwa Cheka alipinga pambano hilo kuwa chini ya usimamizi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa(TPBC) wakati yeye akitaka Chama kingine cha masumbwi ya kulipwa (PST) ndio kichukue jukumu hilo, tukio ambalo lilichukua takribani dakika 30 kabla ya Cheka kukubali kupanda ulingoni baada ya kubembelezwa sana na waandaaji. |
▼
No comments:
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa