.CD ya wimbo wa Taifa yagoma
.Viingilio vyawaacha wengi nje
WAANDISHI wa kigeni walioambatana na timu ya Brazil nchini, jana walionja adha ya 'Bongo', baada ya vibaka kuwahadaa na kufanikiwa kuwachomolea pochi wakati wakiwa katika kazi yao nje ya Uwanja wa Taifa.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, wakati waandishi hao wakipiga picha nje ya uwanja, wakati huo watu wakiwa katika harakati za kuingia uwanjani kuzishuhudia Taifa Stars na Brazil .
Walichofanya vibaka hao ni kuwahadaa waandishi hao kwa kuwatisha kuwa kwanini wanapiga picha katika eneo hilo, wakati wakijaribu kujieleza, kibaka mmoja aliyekuwa nyuma ya mwandishi mmojawapo, akachomoa pochi na kukimbia.
Licha ya kuwapo askari eneo la nje ya uwanja, vibaka hao walitumia mbinu kali na kufanikiwa kutokomea, licha ya juhudi kubwa za askari polisi.
Tukio jingine ambalo nalo litabaki kama kumbukumbu isiyopendeza, ni kugoma kwa 'CD' ya wimbo wa taifa kwa kuimbwa nusu yake, tofauti na ule wa Brazil ambao uliimbwa hadi mwisho.
Hii imedhihirisha jinsi Tanzania ilivyo nyuma, kwani licha ya kuwapo kwa njia nyingi za kiteknolojia, lakini wimbo ya taifa hadi leo bado unahifadhiwa kwenye mfumo wa CD.
Baada ya CD hiyo kugoma, maelfu ya mashabiki waliokuwa uwanjani walishindwa kuvumilia kuonyesha hasira zao wazi, wakaamua kuzomea. Yote haya yanapaswa kuwa funzo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na serikali kwa ujumla.
Kwa kuwa mechi ya Brazil ni ya kihistoria kwa Tanzania, hata maandalizi yake yalipaswa kuwa ya kiwango cha juu, tofauti na ilivyokuwa jana.
Kwa nini 'brass band' isingeimba wimbo huo badala ya CD?
Kero nyingine katika mechi ya jana ni miundombinu mibovu ya uwanja, ikiwamo baadhi ya vyoo kukosa umeme, hali ambayo iliwalazimu watu kutumia mwanga wa simu, huku hofu ya vibaka ikitawala.
Aidha, viwango vikubwa vya kiingilio katika mechi hiyo jana vilionekana wazi kuwa kikwazo kwa mashabiki wengi kuingia uwanjani, hivyo watu wengi kubaki nje walau kujifariji kwa mayowe ya waliokuwa wamebahatika kuingia.
Hili ni funzo kubwa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo liliamua kuweka kiingilio kikubwa zaidi kwa kisingizio cha gharama kubwa za kuileta timu hiyo, bila kujali hali ya kipato kwa Watanzania wengi.
Mechi hiyo iliyomalizika kwa Brazil kushinda mabao 5-1, itabaki kukumbukwa kwa mengi, lakini kero zilizojitokeza zinapaswa kufanyiwa kazi na mamlaka husika ili kuiepushia nchi yetu aibu.
Mwisho
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa