Ikiwa imebaki miezi michache kwa kinyang'anyiro cha uchaguzi, tayari homa imepamba moto huku baadhiya makada wa vyama vya Siasa wakipandwa na homa kali za uchaguzi pamoja na siasa chafu zenye chuki na lengo la kuwachafua baadhi ya watu waliotangaza kugombea ubunge katika Jimbo la Imelela Jijini Mwanza kupitia CCM, zimeanza kufanywa kwa ajili ya kuwapaka matope baadhi ya wagombea hao.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Mwanza, Kada maalufu wa Chama hicho tawala, ambaye pia alishatangaza kugombea ubunge jimbo la Ilemela, Samson Sigwa Maganga alisema mbinu chafu za kumpaka matope kwa jamii zimeanza kufanywa, na wahasimu wake.
Katika hilo , Maganga ambaye amewahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya CCM ikiwemo nafasi ya Uweka hazina wa CCM mkoani hapa, alisema moja ya mbinu zinazotumiwa na wabaya wake ni kumchafua kupitia vyombo vya habari.
Alisema wiki iliyopita alichafuliwa kwa maskusudi na gazeti moja linalotoka kwa wiki jijini hapa, kwa madai kwamba ameanza kampeni mapema kabla ya Tume ya Uchaguzi (NEC), kutoa idhini hiyo, jambo ambalo alisema si kweli..
"Sijaanza kampeni hata kidogo kama ilivyoandikwa na hili gazeti, taarifa hizi ni uzushi na porojo tupu! Tunafahamu mfa maji haachi kutapatapa, mie naheshimu kanuni na taratibu za CCM na nchi yangu", alikanusha Maganga.
Alisema, taarifa zilizochapishwa na gazeti hilo kwamba anatamba jimboni humo kwamba ametumwa na Rais wa nchi, Jakaya Kikwete si kweli, kwani yeye hana mahusiano yoyote ya kirafiki wala ukaribu na Rais Kikwete, bali anamfahamu kama kiongozi wa nchi.
Kwa mujibu wa Maganga, ameamua kujitosa kugombea ubunge katika jimbo hilo linalowasilishwa hivi sasa na mbunge anayemaliza muda wake, Anthony Mwandu Diallo kutokana na changamoto za ubovu wa miundombinu, sekta ya elimu na masuala ya kiuchumi, na kwamba hajatumwa na mtu yeyote kwenda kugombea.
"Mimi sijatumwa na mtu kwenda kugombea ubunge Ilemela, mtu anayesambaza uongo huo anapaswa kusutwa na jamii kumuona ni muongo na mchonganishi mkubwa", alisema mgombea huyo, Maganga.
Alitoa wito kwa Watanzania wote, wakiwemo wakazi wa jimbo la Ilemela kuhakikisha wanachambua pumba na mchele wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika 31 Oktoba mwaka huu nchini kote.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa