Waandamanaji Uganda wavua mashimoni
Wakazi kutoka mji mkuu wa Uganda, Kampala wamekuwa wakipinga hali ya barabara kwa kuvua samaki kwenye madimbwi.
Waandamanaji hao wamesema hali duni ya barabara husababisha ajali na kuongeza hali ya msongamano wa magari.
Mwandishi wa BBC Joshua Mmali amesema barabara za Kampala zina hali mbaya kiasi ambacho mji huo umepewa jina la utani la "Kampothole" yaani Kampala yenye mashimo.
Mji wa Kampala ni wenye wafuasi wengi kutoka upinzani na meya wa mji huo ameiambia BBC hajapewa kodi ya mapato ya kutosha kukarabati barabara.
Meya Nasser Ntege Ssebagala amesema, " Kuweka kilomita moja ya lami katika barabara inahitaji uwe na dola za kimarekani milioni moja." " Hii ni tatizo kubwa."
Aibu
Waandamanaji hao wachache wamesema Juni 8 ingetakiwa kuwa siku ya kitaifa ya mashimo.
Aliyeandaa maandamano hayo Godfrey Birimumaaso ameiambia BBC, " Tunawasihi wahusika wasuluhishe hili tatizo."
Amesema, " Ni aibu, tuko Kampala, kitovu cha Uganda."
Waandamanaji hao waliigiza kama wachuuzi , wakiuza samaki kutoka kwenye mashimo makubwa na mabimbwi yaliojaa maji.
Waliwapigia kelele kwa waliopita na magari, " Samaki wa shilingi elfu tano (dola 2) moja kwa moja kutoka Ssebagala, meya wa Kampala."
Mwandishi wetu amesema kundi hilo lilifanya kasheshe katika jaribio la kuiabisha halmashauri ya jiji la Kampala.
Madereva wa mabasi na pikipiki waliokuwa wakipita walishangilia kuonyesha kuwaunga mkono.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa