Translate in your language

Friday, May 14, 2010

Kifo cha ndugu yetu Nsega Ntobi kisihusishwe na siasa

Kifo cha ndugu yetu kisihusishwe na siasa: 

Na mwanablog wetu Mwanza
Mwanza.
 
FAMILIA ya marehemu Nsega Ntobi aliyefariki juzi (jana) katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), ya Jijini Mwanza, imesema kifo hicho kisihusishwe na masuala ya kisiasa.
 
Imesema, kifo hicho kimetokana na matatizo ya ugonjwa wa akili aliyokuwa nayo marehemu Nsega ambaye alikuwa akitajwa kutaka kugombea ubunge Jimbo la Busega Wilayani Magu mkoani hapa kupitia chama tawala, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kaka wa marehemu Nsega, Leonard Bugomora alisema, ndugu yao huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili, na alikuwa amelazwa hospitali ya Bugando tangu Mei 5 mwaka huu.
 
"Napenda kukanusha habari zilizoandikwa na gazeti la Nipashe la leo (jana), kuhusu ndugu yetu...dada yangu Nsega alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa kwa muda wala hajachezewa kisiasa", alisema Bugomora.
 
Aidha, Bugomora ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Usalama na Maadili CCM mkoa wa Mwanza, na ni mwenyekiti wa Shirika la Nyanza (NCU), mkoani hapa, aliwaonya wanasiasa kutotumia mwanya wa kifo cha ndugu yao huyo kujinadi majukwaani.
 
"Kifo cha dada yetu naomba wanasiasa wasikitumie kujinadi...haya ni matatizo ambayo hata sisi familia yake tulikuwa tunayafahamu, hatutaki iwe hivyo", alionya kaka yake huyo.
 
Marehemu Nsega ambaye alikuwa bado hajatangaza nia yake rasmi ya kugombea ubunge, alifariki juzi katika hospitali ya Bugando, baada ya kulazwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili.
 
Katika taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo la Nipashe, ilidaiwa kwamba, kifo cha marehemu Nsega kimechangiwa na mkono wa mtu, jambo ambalo familia imelikanusha vikali.

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)