Aichapa Yanga 4-3, Mgosi apiga 2 .Akabidhiwa mwali kwa raha zake .Dalali, wachezaji walia kwa furaha
Na Makuburi Ally
Na Makuburi Ally
TIMU ya Simba, jana ilifanya mambo mawili kwa mpigo yanayoweza kubaki katika rekodi za timu hiyo na soka la Tanzania: kukabidhiwa rasmi ubingwa wa Ligi Kuu bara bila kupoteza mechi huku ikimchapa mtani wake Yanga mara zote mbili katika ligi hiyo iliyoanza Agosti 23, mwaka jana.
Simba jana ilimfunga mtani wake mabao 4-3 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kama ilivyokuwa katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu pale Simba iliposhinda bao 1-0 katika mechi ya Oktoba 31, mwaka jana.
Ushindi huo umeifanya Simba kutwaa ubingwa wake wa 17 na Yanga ikifanya hivyo mara 22 tangu mwaka 1965 huku mechi ya jana ikiwa ya 92 kwa timu hizo. Simba imeshinda mara 25; Yanga mara 28 na sare mara 29
Katika mechi ya jana, Simba waliuanza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya tatu likipachikwa wavuni na Uhuru Selemani, akimzidi mbinu beki wa Yanga, Amir Maftah, na kuujaza mpira wavuni.
Bao hilo liliongeza kasi ya mashambulizi ingawa Yanga ilifanya shambulizi kali katika dakika ya nane pale Abdi Kassim alipofumua shuti ambalo liliwababatiza mabeki wa Simba kabla ya kutoka nje.
Simba waliendea kuishambulia Yanga na katika dakika ya 11, beki Salum Kanoni alipiga shuti kali ambalo hata hivyo lilipaa juu ya lango na dakika moja baadaye, Uhuru aliwapiga chenga mabeki wa Yanga ambao walitoa mpira na kuwa kona.
Yanga walisawazisha bao katika dakika ya 31 likifungwa na Kiggi Makasi aliyeunganisha mpira ambao ulitokana na faulo baada ya Shadrack Nsajigwa kuangushwa na Juma Jabu.
Mabao hayo yalidumu hadi mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza alipopuliza filimbi ya mapumziko; timu hizo zilitoka uwanjani zikiwa zimefungana bao 1-1.
Kipindi cha pili, Simba walirejea kwa kasi na kufanikiwa kufunga bao la pili katika dakika ya 53, likifungwa na Mussa Hassan Mgosi akiunganisha pasi ndefu ya Emanuel Okwi na kuukwamisha mpira wavuni.
Mwamuzi wa mechi hiyo, alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Wisdom Ndlovu, baada ya kumchezea vibaya Okwi ambapo awali alionyeshwa kadi mbili za njano.
Kutolewa kwa Ndlovu, kuliongeza kasi ya ushambuliaji kwa Yanga iliyopata bao la pili katika dakika 67, safari hii likifungwa na Jerry Tegete aliyeunganisha pasi ya Abdi Kassim; Tegete aliingia baada ya Ambani.
Katika dakika ya 74, Mgosi alirejea mara ya pili katika nyavu za Yanga na kuifungia timu yake bao la tatu akiunganisha krosi safi ya Okwi na kuukwamisha mpira wavuni na kushangiliwa kwa staili ya kipekee ya kuimba CCJ… CCJ… CCJ… CCJ. CCJ ni chama kipya cha siasa.
Katika dakika ya 86, beki wa Yanga Amir Maftah alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa Juma Nyoso hivyo Yanga kuwa na pengo la wachezaji wawili.
Dakika ya 88, kipa wa Simba Juma Kaseja alimdaka mguu kiungo Abdi Kassim ndani ya maguu 12, hivyo mwamuzi Akrama kuamuru penalti ambayo ilikwamishwa wavuni kwani licha ya Kaseja kuicheza, alijikuta akiisindikiza wavuni.
Baada ya kufungwa bao hilo, Kaseja aliangua chozi kwa uchungu hali ambayo ilisababisha wachezaji wenzake kumsihi kutolia badala yake arejee kwenye mchezo.
Katika dakika ya 90, Hilary Echessa, nyota wa kimataifa wa Kenya, alishindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Yanga kwa kufunga bao la nne akiunganisha pasi safi ya Emanuel Okwi.
Baada ya kufunga bao hilo, Echesa alishangilia kwa kuvua jezi, hivyo kulimwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje kwa kadi nyekundu, hivyo Simba kuwa na pengo la mchezaji mmoja na Yanga wachezaji wawili.
Katika dakika hizo za majeruhi, Kaseja aliumizwa vibaya na mshambuliaji Mrisho Ngassa hadi kupoteza fahamu, lakini alitibiwa na kuendelea na mchezo.
Baada ya mchezo huo, mwenyekiti anayemaliza muda wake, Hassan Dalali, alimwaga machozi ya furaha hali ambayo ilisababisha wachezaji wengine kumwaga machozi.
Tukio la Dalali na wachezaji kuangua chozi la furaha lilikwenda sambamba na wachezaji wa timu hizo kubadilisha jezi kuashiria uungwana katika michezo (fair play) kwani michezo ni furaha na afya.
Kwa upande wa vituko, wakati mechi ikiendelea walionekana njiwa wawili ambapo mmoja alirushwa jukwaani na mwingine mweusi akishindwa kuruka na kubaki karibu na benchi la Yanga , hivyo kufanya baadhi ya wachezaji kumpiga mateke, hata hivyo alishindwa kuondoka.
Baada ya mechi hiyo, Simba walikabidhiwa kombe lao na wadhamini wa Ligi Kuu Tanzania bara, Vodacom huku Yanga wakipewa kombe la mshindi wa pili.
Simba: Juma Kaseja, Salum Kanoni, Juma Jabu/Ulimboka Mwakingwe, Joseph Owino, Kelvin Yondani, Nico Nyagawa, Uhuru Selemani, Hilary Echessa, Mohamed Banka/Juma Nyoso, Mussa Hassan Mgosi na Mike Barasa/ Emanuel Okwi.
Yanga: Obren Curcovic, Shadrack Nsajigwa, Amir Maftah, Wisdom Ndlovu, Nadir Haroub Canavaro, Nurdin Bakari/Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa, Abdi Kassim, Athumani Iddy, Boniface Ambani/Jerry Tegete na Kiggy Makassy/Steven Bengo.
Mwisho
Wigan yaitandika Arsenal 3-2
LONDON, England
HESABU za kocha wa timu ya Arsenal, Arsene Wenger, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England, zimezidi kutibuka baada ya jana kuchapwa mabao 3-2 na Wigan katika mechi iliyopigwa kwenye dimba la DW Stadium.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya ushindani mkubwa, Arsenal ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 41 lililofungwa na Theo Walcott ambalo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.
Katika kipindi cha pili, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa nguvu, lakini Arsenal wakionekana kutulia zaidi na kupanga mashambulizi ya nguvu na kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 48.
Bao hilo lilifungwa na Mikael Silvestre kwa kichwa akiunganisha mpira uliokuwa umetokana na kona.
Licha ya kuwa nyuma, Wigan wakicheza mbele ya mashabiki wao, walijipanga upya na kufanikiwa kupata mabao matatu ya haraka ndani ya dakika 10.
Bao la kwanza lilifungwa katika dakika ya 80 na Ben Watson kabla ya Titus Bramble kupiga bao la pili katika dakika ya 89.
Mabao hayo yalionekana kuwapa nguvu Wigan ambao walianza kulisakama lango la Arsenal na kufanikiwa kupiga bao la ushindi katika dakika ya 90, likifungwa na Charles N'Zogbia, hivyo hadi filimbi ya mwisho, Wigan walitoka kifua mbele kwa mabao 3-2
Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kubaki nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 71 nyuma ya Chelsea inayoongoza ligi kwa pointi 77, baada ya juzi kuchapwa 2-1 na Tottenham huku Manchester United ikifuatia kwa pointi 76.
Mwisho
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa