Translate in your language

Sunday, April 18, 2010

PAMBANO LA WATANI WA JADI

SIMBA VS YANGA LEO

 

KITENDAWILI cha nani zaidi katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2009/2010 baina ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga kitateguliwa leo katika Uwanja wa Taifa kwa wakali hao kukutana katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miamba hiyo iliyoteka hisia za mashabiki wengi wa soka nchini inakutana katika mechi ya mzunguko wa mwisho wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 23, mwaka jana na itakayofikia tamati Aprili 21, huku Simba ikiwa bingwa licha ya kusaliwa na mechi nne mkononi.

Aidha, hadi inatwaa ubingwa, Simba ilikuwa haijafungwa mechi hata moja, isipokuwa sare mbili dhidi ya Lyon na Kagera Sugar, hivyo Simba leo itakuwa ikitaka kushinda kulinda heshima yake na kuweka rekodi ya kutofungwa.

Mbali ya hilo, Simba iliyoasisiwa 1936, mwaka mmoja baada ya Yanga, leo itakuwa ikipambana kushinda ili kuendeleza ubabe kwani katika mechi ya raundi ya kwanza iliyopigwa kwenye uwanja huo Oktoba 31, mwaka jana, Simba ilishinda bao 1-0, likifungwa na Mussa Mgosi.

Wakati Simba ikitaka kufanya hivyo, Yanga waliojihakikishia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf), itakuwa ikipambana kushinda ili kulipa kisasi na kumtibulia mtani wake radha ya ubingwa hasa ikizingatia leo ndiyo siku ya kukabidhiwa taji.

Kwa mantiki hiyo, licha ya timu hizo kutopigania ubingwa, mechi ya leo ambayo Yanga ndio wenyeji, inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kwani kila timu itakuwa ikisaka ushindi kwa nguvu zote kwa malengo tofauti.

Mbali ya kutaka kulipa kisasi cha Oktoba 31, Yanga itakuwa ikipambana vilivyo kulipa kisasi, pia kutibua rekodi ya mtani wake ya kutofungwa huku Simba nayo ikitaka kudhihirisha ubora wake uliomfanya akatwaa ubingwa.

Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega alisema mapema wiki hii kuwa watapambana kufa au kupona kuhakikisha leo wanalitia mchanga pilau la Simba kwani kama watafungwa, watakuwa wamefanikiwa kutibua radha ya ubingwa.

Simba nayo itacheza kufa na kupona ili kulinda heshima yake ya kutofungwa katika ligi hiyo, pia kuendeleza ubabe wa kuitambia Yanga katika msimu huu  na tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hassan  Othman 'Hassanoo' ametamba kuifunga Yanga.

Kabla ya kukutana, timu hizo zimekuwa katika maandalizi kama kawaida yake ambapo Simba imekuwa Visiwani Zanzibar kwa muda mrefu hata kabla ya kuanza kwa ligi hiyo ikiamini kambi ya huko imekuwa yenye manufaa kwake.

Yanga wao waliamua kubaki jijini wakijichimbia katika hoteli ya Southern Sun, ingawa mapema wiki hii walikwenda Zanzibar kupata baraka kwa mlezi wao, Mama Fatma Karume, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume aliyefariki Aprili 7, mwaka 1972.

Kwa upande wa wachezaji wa vikosi vyote, hali zao ni imara hivyo kazi itabaki kwa makocha kuamua nani aanze, lakini wachezaji wa kila timu wametamba kuwaadhiri wenzao katika mchezo wa leo.

Hata hivyo, Simba inashuka dimbani bila ya kocha wake mkuu, Patrick Phiri, aliyekwenda kwao kwa matatizo ya kifamilia, hivyo mikoba kukabidhiwa kiungo wa zamani wa timu hiyo, Suleiman Matola akisaidiana na Kocha Msaidizi, Amri Saidi, aliyewahi kucheza na Matola.

Yanga wakiwa chini ya Kocha Mserbia, Kostadin Papic akisaidiwa na Medic Moma, wamekamia kushinda ili kulinda hadhi ya timu hiyo hasa kujifariji baada ya kuutema ubingwa wa Ligi Kuu ambao iliushikilia kwa misimu miwili, wakati huo chini ya Kocha Dusan Kondic.

Viingilio katika mechi hiyo itakayoanza kupigwa saa 10.30 jioni ni sh 40,000 kwa Jukwaa la  VIP A, Jukwaa la VIP B sh 30,000,  Jukwaa VIP C sh 20,000, Orange Straight sh 15,000,  Orange curve  sh 10,000, Blue  sh 7,000 na green sh 5,000.


No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)