WANAWAKE wilayani Temeke wametakiwa kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu Oktoba kwa hoja bila ya kupoteza upendo waliokuwa nao awali.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dar es Salaam, Zarina Madabida, kwenye kikao cha Baraza la UWT wilayani humo.
Alisema kipindi hiki ndicho watu huanza kupakana matope kwa kurushiana kashfa mbalimbali na kujenga chuki miongoni mwa wanawake, hivyo ni vema wakawa makini kwani vitendo hivyo vinaweza kuwarudisha nyuma kimaendeleo.
Alisema wanawake kutoka kwenye vyama vingine wataweza kujiunga na umoja huo endapo utaonekana una maendeleo lakini kama watu wataendekeza chuki zitakazotokana na kampeni za uchaguzi ni wazi kwamba hawatataka hata kuisikia UWT.
Kama vile haitoshi aliwataka wanawake hao kasi yao ya kuhamasisha watu kujiandikisha kupiga kura waliyoanza nayo iendane sambamba na kujitokeza wenyewe katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
"Pia katika hili naomba nisisitize jamani pale anapojitokeza mwanamke mwenzetu kugombea nafasi yoyote ni vema tukaunga naye urafiki, ili kuweza kumsaidia kushinda kwa kishindo badala ya kumbeza jambo ambalo litamvunja moyo na nafasi hiyo kuchukuliwa na mwanaume," alisema mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UWT, wilaya ya Temeke, Shadya Mtoro, alisema wataendelea kuhamasisha Jumuiya ya UWT kuanzia ngazi ya mashina kuingiza wanachama kwa wingi.
Kwa upande wake Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwataka kina mama hao kupendana na kushirikiana.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa