Na,Jumbe Ismailly,Singida March,04,2010 Nyaya
Kampuni ya simu Tanzania (T.T.C.L) Mkoani Singida imepata hasara ya shilingi 22,970,541/= kutokana na kuibiwa nyaya zake zenye urefu wa mita 1,400 katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009.
Meneja wa T.T.C.L. Mkoani Singida,Bwana Joseph Masanje alibainisha hayo kwenye taarifa yake ya kikosikazi kati ya jeshi la polisi na T.T.C.L. aliyotoa kwa mkuu wa jeshi hilo nchini,IGP.Said Mwema.
Aidha meneja huyo aliweka bayana kwamba katika kipindi hicho jumla ya matukio 11 yaliripotiwa,ambayo kati ya hayo saba yaliripotiwa kabla ya kuundwa kwa taskforce hiyo mwaka 2007, matatu yaliripotiwa mwaka 2008 na moja mwaka 2009.
“Baada ya kuona vitendo vya uhalifu wa miundombinu ya T.T.C.L. vinazidi kuongezeka,kampuni hiyo kwa kushirikiana na jeshi la polisi tuliunda Task Force ya kukabiliana na tatizo hilo ”alifafanua Masanje.
Hata hivyo Masanje hakusita kuweka bayana kwamba kutokana na matukio hayo,jumla ya kesi saba zilifikishwa mahakamani,na kwamba kati ya kesi hizo watuhumiwa wa kesi mbili walihukumiwa adhabu ya kifungo,kesi nne waliachiwa huru na kesi moja bado inaendelea.
Kwa mujibu wa meneja huyo wa t.t.c.l. baada ya kuundwa kwa Task Force hivi sasa matukio ya uharibifu wa nyaya za simu yamepungua sana,hakuna tukio lililoripotiwa katika kipindi cha miezi kumi kuanzia mei,2009 hadi feb,2010.
“Tunaushukuru sana uongozi wa jeshi la polisi Mkoani,Taifa, wananchi,wadau mbali mbali hapa mkoani ambao wamekuwa wakitoa ushirikiano wa karibu ikiwa ni pamoja na taarifa zinazowezesha kukabili vyema matukio haya yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu na watu wake”alisisitiza meneja Masanje.
Aidha Masanje hakusita kutumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Mkoa wa Singida kwa kupiga marufuku biashara ya vyuma chakavu,na kuongeza kwamba hivyo ni imani ya kampuni hiyo kuwa tiba ya tatizo hilo itapatikana na kuwa endelevu kwa taifa kiujumla.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa