Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Fedha na Uchumi, Omar Yusuf Mzee, amewataka wahitimu katika Chuo cha Ununuzi na Ugavi (IPS) kutokuwa wabadhirifu kazini, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa hawawatendei haki Watanzania.
Naibu waziri huyo alitoa rai hiyo juzi katika mahafali ya tatu ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo, Chanika, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema wahitimu hao wanapaswa kuwa waadilifu, kwani asilimia kubwa wamefadhiliwa masomo yao na serikali.
“Mnapaswa kuwa waadilifu katika kazi zenu, ili muweze kuwatumikia vema Watanzania ambao mmesoma kwa kodi zao.
“Sekta hii ni muhimu sana na tunaweza kunusuru pesa nyingi za walipa kodi kwa kutumia wataalamu wetu badala ya kutoka nje ya nchi,” alisema.
Aliwataka wahitimu hao kufahamu sheria ya ununuzi na ugavi ya mwaka 2004, ili wanapokwenda sehemu za kazi wawe wanaifahamu, hivyo kuweza kutekeleza majukumu yao vema.
Aidha, aliwashauri wanachuo waliohitimu katika ngazi ya cheti kujiendeleza zaidi katika elimu hiyo, ili wawe na ujuzi mpana zaidi kabla ya kutafuta kazi.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Dk. Didas Masaburi, alisema pamoja na chuo hicho kutoa elimu ya juu katika masuala ya ununuzi na ugavi, uhasibu, biashara na utawala, lakini bado hakijathaminiwa kwa kiwango kinachostahili.
“Tunakuomba uwe balozi wetu baada ya mahafali haya, uendelee kuzishauri serikali zetu na uambie kuwa leo tumezaa wataalamu hawa uliowaona ili wakachape kazi serikalini, katika mashirika ya umma na kwa watu binafsi,” alisema Masaburi ambaye pia ni Mbunge wa Afrika Mashariki.
Aidha, alizitahadharisha serikali kuwa wakati tunaelekea katika soko la pamoja la Afrika Mashariki, iwapo nchi isipokuwa makini bidhaa feki nyingi zikiwamo za huduma zitaingizwa nchini.
Jumla ya wahitimu 176 wa ngazi ya cheti, cheti cha juu, stashahada na stashahada ya juu walitunukiwa vyeti.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa