Sisi, wanachama wa Policy Forum, Mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali, tuliokutana tarehe 29 na 30 Aprili, 2015 katika mkutano wetu wa mwaka (AGM) Dar es salaam, tumesoma na kuchambua kwa kina Miswada ya Sheria ya Takwimu pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kwa lengo la kujieleimisha na masuala ya katiba na uchaguzi mkuu 2015.
1. SHERIA YA TAKWIMU NA SHERIA YA MAKOSA YA MTANDAONI
Tumebaini kuwa muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao unaoainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, pamoja na muswada wa Takwimu, pamoja na kitendo cha kupeleka miswaada hii bila kushirikisha wadau na wananchi ni ishara kamilifu kuwa sheria tarajiwa sio kwa lengo la kulisaidia Taifa bali ni kusudio la makusudi la kuzuia uhuru wa maoni, taarifa na maarifa na lenye madhara makubwa kwa maendeleo ya jamii yetu.
Moja ya madhara ya kuwa na sheria kama hizi, iwapo Mheshimiwa rais ataweka saini ni pamoja na:
1.1 Kuondosha kabisa uhuru wa upashanaji habari hivyo kuminya demokrasia ya ushiriki wa wananchi katika maendeleo yao.
1.2 Kuondosha kabisa uhuru wa vyombo vya habari na weledi katika habari hivyo kufanya fani ya habari kutokuwa ya ushindani.
1.3 Adhabu zinazotajwa katika miswada hazilengi kujenga jamii iliyostaarabika bali zinataka kujenga jamii inayoogopa na isiyojiamini.
1.4 Kufifisha weledi wa utafiti na upatikanaji wa matokeo ya utafiti na takwimu kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo katika ngazi zote na hivyo kudhoofisha taaluma ya takwimu na tafiti.
1.5 Kufifisha ukuaji wa teknolojia na ubunifu katika teknolojia ya habari (kwa mfano, social media) hivyo kuathiri nchi katika uwezo wake wa kushiriki katika uchumi unaotegemea utandawazi.
Hivyo, tunapotoa maoni yetu kuhusu upitishwaji wa miswaada hii miwili, tunasisitiza kuwa miswaada hii inahitaji kurejewa na kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia maoni ya wadau na wananchi ili iongeze tija katika kutoa uhuru zaidi wa maoni, habari, taarifa, takwimu na maarifa. Tunaamini kuwa huu ndio unapaswa kuwa msingi wa kuandikwa kwa miswaada hii.
WITO WETU:
1. Tunamsihi Mheshimiwa Rais asiweke saini katika miswaada hii bali atoe fursa kwa wadau zaidi kushiriki katika kuirejea na kuifanyia marekebisho
2. Kwa kuwa suala la takwimu na mitandao sio jipya hapa duniani, tunatoa rai kwa watendaji wa serikali kujifunza zaidi kutoka katika nchi zingine (best practices) ambazo zimekutana na changamoto kuhusu takwimu na mitandao na hasa jinsi ambavyo wenzetu hao walivyozishughulikia.
3. Zizalishwe nakala zaidi ili ziufikie umma mpana kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali wapate nafasi kutoa elimu na kupokea maoni ya wadau na umma mpana.
2. MASUALA YA KATIBA NA UCHAGUZI MKUU WA 2015
Vile vile, baada ya kutafakari kwa kina juu ya uchaguzi mkuu wa 2015 na mchakato wa Katiba, mkutano mkuu wa Policy Forum umezingatia umuhimu wa uchaguzi mkuu wa 2015 na shughuli za uandikishaji wa wapiga kura kwa njia ya BVR na uandikishaji wa vitambulisho vya uraia, hivyo tunapendekeza mambo yafuatayo:
2.1 Tunapendekeza upigaji kura ya maoni uahirishwe mpaka baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
2.2 Tunawahimiza watanzania kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la wapiga kura na wajitokeze kupiga kura siku itakapofika.
Israel Ilunde
Mwenyekiti wa Bodi, Policy Forum
Kny: Mkutano mkuu wa mwaka (AGM) 2015
Pia waweza kutembelea mtandao wao kupitia http://www.policyforum-tz.org
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa