Translate in your language

Monday, October 13, 2014

KAMPENI YA CHANJO YA SURUA RUBELLA 2014

Sehemu ya kwanza

Mtoa wa chanjo akitoa chanjo kwa mtoto 
Kampeni ya chanjo dhidi ya surua na rubella
UTANGULIZI
Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika mikakati ya kupunguza vifo vya watoto ili kufikia lengo la nne (4) la milenia la kupunguza vifo vya watoto. Mojawapo ya mikakati hiyo ni utoaji wa chanjo kwa watoto ili kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo ina utaratibu madhubuti wa kufanya kampeni za kitaifa za utoaji wa chanjo. Kampeni ya mwaka 2014 ina lengo la kutoa chanjo ya Surua Rubella, matone ya Vitamini A. Vilevile Kingatiba za Minyoo, Mabusha na Matende kwa kutumia dawa za Albendazole na Ivermectin zitatolewa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeandaa kampeni ya kitaifa ya kutoa;
  • Chanjo ya Surua Rubella kwa watoto wote walio katika umri wa miezi 9 mpaka chini ya miaka 15
  • Kutoa vidonge vya vitamin A kwa watoto wote wenye umri wa miezi 6 mpaka 59
  • Kutoa dawa za minyoo aina ya Mebendazole kwa watoto wote wenye umri wa miezi 12 hadi 59.
  • Kutoa dawa za minyoo aina ya Albendazole kwa umri wa miaka 5 na kuendelea kwa mikoa husika.
  • Kutoa dawa ya Ivermectin na Albendazole zinazokinga Usubi, Minyoo ya Tumbo, Matende na Mabusha kwa umri wa miaka 5 na kuendelea kwa mikoa husika.

Kampeni hii itafanyika kwa utaratibu wa watoto wote wenye umri chini ya miaka kumi na tano kupelekwa katika vituo vya kutolea huduma vilivyoandaliwa. Pia kampeni hii itahusisha watoto walio shuleni na wale wasio shuleni na watu wa umri wa zaidi ya miaka 15 kwa dawa za Albendazole na Ivermectin

SIKU ZA KAMPENI
Kampeni itafanyika kitaifa kwa siku saba (7) kuanzia tarehe 18 mpaka 24, Octoba, 2014.

AINA ZA VITUO:
Kampeni ya hii itafanyika katika vituo vya uchanjaji vya aina mbili
·         Vituo vya kudumu – Timu za uchanjaji zitakuwa kwenye kituo kwa siku saba (7) kuanzia saa 1asubuhi hadi saa 11 jioni.
·         Vituo vya muda na kuhama hama - timu za uchanjaji huduma kwa tarehe zilizopangwa na zikimaliza walengwa katika eneo husika zinahamia sehemu nyingine iliyopangwa.

LENGO LA KAMPENI YA KITAIFA
·            Kuna uthibitisho wa kitaalamu kwamba ni asilimia 85 tu ya watoto wanaopata chanjo ya surua wakati wanapotimiza miezi 9 wanapata kinga kamilifu ya ugonjwa wa surua.
·         Kuna watoto wengine ambao hawajapata kabisa huduma ya chanjo na kuna vituo ambavyo havijafikia lengo la kuwachanja watoto kwa asilimia 100. Mlundikano wa watoto hawa wasio na kinga kila baada ya miaka 3 hadi 4 huweza kusababisha milipuko ya ugonjwa wa surua.
·         Tafiti zilizofanyika nchini zinaonesha kwamba ugonjwa wa Rubella upo na umeathiri watoto wengi wanaozaliwa na pia unaleta madhara ya kudumu kwa watoto hawa. Kwa sababu hiyo ni muhimu chanjo itolewe kuzuia ugonjwa huu na madhara yake.

·         Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Surua Rubella itawafikia watoto wote wale ambao hawakupata chanjo ya surua kabla na wale ambao hawakupata kinga kamilifu ili kuzuia milipuko ya ugonjwa wa surua Rubella.

·         Tafiti mbalimbali zimethibitisha kuwa watoto wengi walio na umri chini ya miaka mitano wanakosa virutubisho vya vitamin A ambavyo ni muhimu kujenga na kuulinda mwili.  Vile vile mazingira wanayocheza husabibisha wapate minyoo kwa urahisi na kusababisha kudhoofika katika ukuaji na kupungukiwa damu.Utoaji wa vitamin A na dawa za minyoo utahakikisha watoto walio chini ya miaka mitano wanapata vitamin A na dawa za kuua minyoo.
·         Kuna uthibitisho kuwa kila wilaya nchini ina maambukizi ya magonjwa ambayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele. Magonjwa haya ni pamoja na Ukoma,Tauni,Kichaa cha Mbwa,Matende, Mabusha,Trakoma,Kichocho,Usubi,Homa ya Dengue, Minyoo ya Tumbo,Homa ya Malale na Homa ya Ini. Magonjwa haya yanasabisha ukuaji duni kwa watoto, ulemavu, upunguzu wa damu mwilini, upofu,uharibfu wa ngozi, saratani  ya kibofu n.k

·         Inakadiriwa takribani watu milioni 40 wapo katika hatari ya kuambukizwa na watu million 5 wameathirika na magonjwa haya nchini Tanzania. Magonjwa haya hudhibitiwa kwa njia mbalimbali ikiwamo ugawaji wa dawa (Kinga-Tiba) kwa jamii nzima.Kampeni hii imelenga pia kudhibiti Matende,Mabusha,Usubi na Minyoo ya Tumbo kwa kutumia  dawa za Albendazole na  Ivermectin katika  mikoa ya Dar-es-salaam, Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Morogoro, Tanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Mtwara, Lindi, Pwani, Manyara, Singida, Dodoma.

Tuungane sehemu ya pili kujua kwa undani magonjwa haya surua na rubella ikiwemo kinga, tiba, madhara yake nk.


No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)