Translate in your language

Friday, January 3, 2014

Korti Yaizuia Chadema kumjadili Zitto

Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe akiwa na Mwanasheria wake,Albert Msando(katikati)na Mwanasheria wa Chadema,Peter Kibatara(kushoto) wakiwa nje chumba cha Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam jana wakisubiri maamuzi ya Jaji kuhusu madai ya Zitto ya Kupinga Kamati Kuu ya Chama hicho kumjadili.Picha na Fidelis Felix 
Mahakama Kuu Tanzania, imeizuia kwa muda Kamati Kuu ya Chadema kujadili ajenda zozote zinazomhusu aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe hadi ombi lake la rufaa litakaposikilizwa.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji John Utamwa baada ya kupokea maombi ya Zitto kupitia kwa Wakili wake, Albert Msando kutaka rufaa yake aliyoiwasilisha Baraza Kuu kusikilizwa kwanza kabla ya kufanyika uamuzi mwingine.
Kamati Kuu ya chama hicho, ilipanga kukutana leo ikiwa na ajenda kuu tatu; kupanga mpangokazi wa chama kwa mwaka 2014, kupokea utetezi wa wanachama watatu kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwao na kupokea taarifa kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Zuio la Mahakama
Zuio hilo lilikuja pia baada ya kutupiliwa mbali maombi ya pingamizi la Chadema lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Katiba na Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Peter Kibatala.
Akizungumza jana baada ya uamuzi huo wa Mahakama, Mwanasheria Mkuu Chadema, Tundu Lissu alisema hakuna jinsi zaidi ya kukubaliana na uamuzi huo... “Tumekubali kutokumjadili Zitto lakini tuliomba Mahakama iruhusu kuhojiwa kwa Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.
Zitto alifungua kesi Mahakama Kuu akiiomba iizuie Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Katibu Mkuu pamoja na Kamati Kuu ya Chadema kumjadili, kumchukulia hatua yoyote kuhusu uanachama wake hadi hapo rufaa yake aliyoikata Baraza Kuu la Chadema itakaposikilizwa.
Pia katika maombi yake, Zitto alitaka Mahakama kuzuia kwa njia yoyote, Kamati Kuu kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake ya Ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Mbali na ombi hilo, pia aliiomba Mahakama kumwamuru Katibu Mkuu wa Chadema ampatie nakala ya mashtaka na maelezo ya uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu Novemba 22, 2013 wa kumwondolea nyadhifa zake ili aweze kuwasilisha rufaa yake Baraza Kuu la Chadema kupinga uamuzi huo.
chanzo ni mtandao wa gazeti la mwananchi:  kwa taarifa zaidi bofya hapa 

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)