Translate in your language

Friday, October 4, 2013

..Kizungumkuti cha majira ya saa, nchi inapojiongezea muda wa siku..


na mwandishi wetu: Ezekiel kamwaga
gazeti: Raia mwema
 
ILI kuelewa mada yangu ya leo, pengine ningefanya vizuri kama ningeanza na swali la kufikirika tu. Hebu fikiria kwamba sasa hivi Rais Jakaya Kikwete atangaze kwamba ameongeza saa tatu mbele kutoka katika muda wa kawaida wa Tanzania.
Muda huu, ninapoandika makala hii, ni saa nne kamili asubuhi. Kwa amri hiyo ya Kikwete (ya kufikirika tu), mara moja itakuwa saa saba kamili mchana.
Kwa sababu nimezoea kula chakula cha mchana muda huo, itabidi sasa nitoke ofisini niende kupata chakula changu cha mchana kwenye sehemu ninapopenda kula.
Lakini, tayari nilikuwa nimekunywa chai takribani saa mbili tu zilizopita. Na kwa vile utaratibu ni kwamba huwa nakula change cha usiku majira ya saa mbili usiku, sasa itabidi nile saa tano usiku.
Kwa amri hiyo ya Kikwete, itabidi nianze kuingia kazini majira ya saa tano kamili asubuhi (saa mbili ya sasa). Muda wa kutoka kazini utakuwa saa mbili usiku badala ya saa kumi na moja jioni.
Haya ndiyo maisha ambayo raia wa Hispania wanaishi hivi sasa. Na aliyesababisha yote hayo ni aliyekuwa mtawala wa nchi hiyo, Dikteta Francisco Franco, ambaye mwaka 1942 alibadili saa za taifa hilo.
Kutokana na uhusiano wake na utawala wa Kinazi wa dikteta mwenzie, Adolf Hitler, Franco aliamua kwamba muda wa Hispania utakuwa sawa na ule wa Ujerumani.
Lakini nchi hizo mbili zilikuwa katika nyakati tofauti kutokana na namna mchoro wa mstari wa tarehe ulivyochorwa.
Tangu wakati huo, Hispania imekuwa ikifuatisha muda huo ambao sasa baadhi ya wana harakati wameanza kuulalamikia.
Mmoja wa wanaharakati hao, Enrique Mendozza, amelalamika kwamba tangu wakati huo (mwaka 1942), taifa lao limekuwa kwenye usingizi kwa vile wananchi wake wanalala wamechelewa, wanaamka wamechoka na hawafanyi kazi kwa ufanisi.
Kutokana na mabadiliko hayo ya Franco, Hispania sasa iko nyuma ya muda wa kawaida wan chi nyingi barani Ulaya kwa saa moja wakati wa majira ya baridi na saa mbili wakati wa majira ya joto.
Ndiyo maana, wapenzi wa soka hapa nchini wamezoea kuona mechi za Hispania usiku sana. Mechi zinaweza kuanza kuanzia saa tano usiku.
Kutokana na kupata muda mdogo wa kulala, Wahispania wakaja na kitu kinaitwa Siesta yaani muda mfupi wa kulala baada ya chakula cha mchana.
Kwa kawaida, wafanyakazi wa Hispania hupewa saa mbili za kula chakula cha mchana na wengi hutumia muda huo kula na kulala kidogo.
Hata hivyo, wapinzani wa muda huo mrefu wa kupumzika mchana wanasema hiyo ndiyo sababu uchumi wa taifa lao umelala.
"Kwanza miye binafsi silali mchana. Na kwa kawaida, situmii zaidi ya saa nzima kula na mara nyingi huwa nakula mchana. Saa zote mbili za nini?" Anahoji Alejandro Martinez katika mahojiano yake aliyofanya na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Ubishani mkubwa zaidi unazidi kuongezeka kuhusu nini hasa faida za kufuata muda uliowekwa mwaka 1884 katika mkutano maarufu wa Merridian.
Katika mkutano huo wa kihistoria, wakoloni walitengeneza mstari wa kufikirika wa tarehe ambao hesabu zake zilianzia kwenye longitudo 0' ambayo ilipewa mji wa Greenwich uliopo England.
Kuanzia hapo, wakubwa waliuchorachora mstari huo kupita karibu katika mabara na nchi zote duniani, chini ya dhana kwamba siku moja itakuwa na saa 24 zinazoanza na kumalizika saa sita usiku.
Matokeo ya maamuzi hayo ni kwamba nchi kama China ambayo ni moja, ilijikuta ikiwekwa katika nyakati tofauti tano (time zones).
Ilibidi utawala wa Mao Ze Dong uingilie kati mara baada ya Uhuru wa China miaka 64 iliyopita ambapo aliamua kwamba nchi nzima itakuwa inatumia muda mmoja.
Nchi kubwa kama iliyokuwa Urusi, ilijikuta ikiangukia katika saa 11 tofauti –kwa lugha rahisi kabisa kwamba kama Mwanza ni saa nne asubuhi, Kigoma inaweza kuwa saa saba mchana, Dar es Salaam ikawa saa moja asubuhi na Mbeya saa tisa alasiri. Nchi moja hiyo.
Wakubwa wa Urusi wameanza kupambana na hali hiyo na sasa wamepunguza tofauti hiyo hadi kufikia kanda (zones) sita tofauti kutoka 11 za awali.
Miaka michache iliyopita, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Samoa, alifanya maamuzi makubwa zaidi baada ya kuirusha nchi yake kutoka Alhamisi hadi Jumamosi ili ifanane na muda wa majirani zake.
Ingawa inaweza kuonekana ni jambo rahisi, lakini uamuzi huo ulikuwa na madhara. Ngoja nikupe madhara ya kawaida kabisa kwanza.
Kwa mfano, kama siku hiyo ilikuwa ni Januari 12 na ghafla ikageuzwa kuwa Januari 14, maana yake ni kwamba mtu ambaye angetakiwa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa siku ya Januari 13 atakuwa ameikosa fursa hiyo.
Kwa wenzetu, sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa inaheshimika sana. Fikiria jambo la pili. Kama mtu alikuwa amehukumiwa kunyongwa Januari 13, maana yake hatanyongwa siku hiyo na itabidi apangiwe siku nyingine.
Unaweza kujiuliza pia kwamba kama umepangiwa kufanyiwa upasuaji (operation) muhimu sana siku ya Januari 13 na ndiyo ikarukwa ghafla, sijui utafanyaje.
Au, najaribu kufikiri tu, kama utakuwa una kesi mahakamani siku ya Januari 13 na ndiyo ikawa imerushwa kupitia mfumo huu wa muda sijui itakuaje.
Aliyekuwa Rais wa Venezuela, hayati Hugo Chavez, aliwahi kurudisha muda nusu saa zaidi nyuma ili kuwapa wananchi wake fursa ya kupata muda wa kufanya kazi zaidi.
Hispania wanaweza kuamua kuongeza saa nzima katika muda wao ili wafanane na wenzao wa Uingereza na Ureno lakini anaweza kuja kiongozi mwingine na kubadili.
Binafsi, natatizwa kweli na mabishano haya kuhusu wakubwa wakati Mwenyezi Mungu ametupa jua la bure kabisa ambalo ni saa inayojitegemea.
Linakupa saa 12 za mwanga na saa 12 za giza. Saa la kwanza kwa jua kuchomoza ingepaswa kabisa kuchukuliwa kama saa moja asubuhi.
Ingekuwa rahisi sana kama nchi zote zingeamua kufuata jua linachoamua. Lakini, rafiki yangu wa kwenye facebook, Evance Lang, wa China aliwahi kuniambia ya kuwa aliwahi kukaa wiki nzima nchini Iceland pasipo kuona jua.
Sasa watu wanaoishi nchi kama hizi sijui watafanyaje. Nashukuru Mungu kwamba nimezaliwa Tanzania ambako kuna jua saa 12 na giza saa 12. Naweza kutumia jua tu na nikaishi bila matatizo ya muda. Taabu ya nini?

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)