Translate in your language

Tuesday, July 16, 2013

UBAGUZI WA RANGI ITALIA WATIA FORA ....!!!

MASUALA YA JAMII

Ubaguzi wa Rangi Italia wajichipuza

Mbunge wa ngazi ya juu,amemfananisha waziri wa kwanza mweusi nchini Italia Cecile Kyenge na nyani katika tukio la hivi karibuni linaloonyesha uhasama utokanao na ubaguzi wa rangi nchini humo
Cecile Kyenge ambaye  ni raia wa Italia lakini mzaliwa wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo amekuwa akilengwa mara kwa mara katika hujuma za ubaguzi wa rangi  tangu alipoteuliwa kuwa waziri wa utangamano nchini Italia mwezi Aprili mwaka huu.
Makamu wa rais wa baraza la Senate Roberto Calderoli mnamo siku ya Jumamosi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Treviglio alisema kuwa anapenda wanyama lakini akimuona Kyenge katika fikra zake, anaona mfano wa aina fulani ya nyani ajulikanaye kama Orangutan.
Calderoli aliongeza kusema mafanikio ya Kyenge yamechochea wahamiaji haramu kuingia nchini Italia wanaoota kuwa wataikuta Marekani nchini Italia na kwamba anastahili kuwa waziri katika nchi yake ya Congo.
Mbunge wa Italia Roberto Calderoli aliyetoa matamshi ya ubaguzi wa rangiMbunge wa Italia Roberto Calderoli aliyetoa matamshi ya ubaguzi wa rangi
Wanasiasa wakiwemo hata wa kutoka katika chama chake wamemshutumu Calderoli huku wengine wakimtaka ajiuzulu kama makamu wa rais wa Senate.
Calderolii ashutumiwa vikali
Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta kupitia mtandao wake rasmi wa twitter amemshutumu Calderoli na kuyataja matamshi yake yasiyokubalika,kwani yanavuka mipaka yote na kuongeza kuwa anamuunga mkono Kyenge anapoendelea na kazi zake na za taifa.
Calderoli alisema hana nia ya kujiuzlu na kuomba msamaha.Alisema hakumaanisha kumuudhi Kyenge lakini matamashi yake yalikuwa ni hotuba ya kisiasa inayomulika kwa mapana sera anazosimamia waziri huyo ambazo ndizo alizokuwa akizishutumu.
Lakini baada ya kushutumiwa kutoka kila pande na sio Italia pekee kwani hata vyombo vya habari vya kimataifa vimeangazia matamshi hayo ya ubaguzi wa rangi,Calderolli alimpigia simu waziri Kyenge na kumuomba radhi.
Kyenge anapigania sera zitakazorahisisha mfumo wa wahamiaji kupata uraia na anaunga mkono sheria itakayomfanya kila  mtoto anayezaliwa Italia kuwa mara moja  raia wa nchi hiyo.
Waziri Cecile Kyenge(Kushoto) katika sherehe ya kuapishwa kwa mawaziri wa Italia Aprili 2013Waziri Cecile Kyenge(Kushoto) katika sherehe ya kuapishwa kwa mawaziri wa Italia Aprili 2013
Mwezi uliopita,Kyenge ambaye amekuwa akiishi Italia tangu mwaka 1983, alipokea vitisho dhidi ya maisha yake kabla ya kuzuru eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambayo ndiyo ngome ya chama cha Calderoli.
Si mara ya kwanza Kyenge kutishiwa
Chama hicho cha Nothern League kilimpiga marufuku mwanasiasa mmoja  baada ya kupendekeza kupitia Facebook kuwa mtu anapaswa kumbaka Kyenge ili afahamu jinsi waathiriwa wa uhalifu wanavyohisi.Viongozi wa chama hicho chenye misimamo mikali wanawalaumu wahamiaji kwa uhalifu wa kimabavu nchini Italia.
Hii si mara ya kwanza kwa Calderoli ambaye alihudumu mara mbili kama waziri katika serikali ya Silvio Berlusoni kuzua mihemko kutokana matamshi yake.Mwaka 2006 alilazimika kujiuzulu baada ya kuvalia fulana iliyokuwa ikimdunisha mtume Mohammed katika kituo cha televisheni cha kitaifa.
Mwaka huo huo,wakati Italia iliposhinda kombe la dunia la soka aliibeza timu ya soka ya Ufaransa kwa kudai kuwa walishindwa kwasababu wachezaji wake ni watu weusi,waislamu na wakomunisti.
Kyenge ambaye ni daktari na ameolewa na muitaliano,amesema Italia inapaswa kuanzisha desturi dhidi ya ubaguzi wa rangi kwani ni chuki na uwoga wa kilicho tofauti na kumtaka Calderoli kutafakari kile anachotaka kuwakilisha kupitia matamshi yake kwani ni kiongozi.
Mwandishi: Caro Robi/ap/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu 

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)