Translate in your language

Wednesday, March 20, 2013

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Furaha

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Furaha kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2012 kwa kutambua umuhimu wa furaha kwa ustawi wa maisha ya mwanaadamu na kufikia malengo ya ustawi wake.
Furaha ni moja ya msingi wa juhudi za binadamu kuishi katika hali nzuri ya uhai wake, kwa maana nyengine furaha hurefusha umri. Katika kutambua umuhimu wa furaha na ustawi kama malengo na matarajio katika maisha ya binadamu, mwaka 2012 baraza la Umoja wa mataifa ilitangaza Machi 20 kuwa siku ya kimataifa ya furaha.
Katika hotuba yake ya kuadhimisha siku ya kwanza ya furaha ulimwenguni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amewataka watu kushinikiza ahadi ya umoja wa maendeleo ya binadamu na kuanza upya juhudi ya kusaidia wengine. Amesema watu wanapata baraka wanaposaidia kufanya mambo mazuri. Ameeleza kuwa huruma inasaidia kukuza furaha na pia inasaidia kujenga maisha tunayoyataka.
Dunia yahitaji furaha
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu furaha na afya njema, Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema dunia inahitaji dhana mpya ya kiuchumi ambayo inatambua usawa kati ya mihimili mitatu ya maendeleo endelevu. Amesema ustawi wa kiuchumi, kijamii na kimazingiza hazigawanyiki, na kuwa vitu hivyo vitatu pamoja vinaashiria furaha ya kimataifa.
Mkutano ulifanyika nchini Bhutan, nchi ambayo inatambua umuhimu wa furaha kitaifa kwa kufungamanisha furaha na pato kitaifa tangu miaka ya 1970.
Umoja wa Mataifa umezitaka nchi wanachama, mashirika ya kimataifa na kimikoa, na pia mashirika ya kijamii, yakiwemo mashirika yasio ya kiserikali na mashirika ya kibinafsi, kusherekea siku hii ya kwanza ya furaha duniani kwa njia nzuri, ikiwa ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha jamii.
Ban Ki-Moon katika ujumbe wake pia ameeleza kuwa watu duniani wanatamani kuishi maisha ya furaha na amani bila uwoga.
Katika mkutano wa mwaka jana wa maendeleo endelevu uliofanyika Rio De Jenairo, nchini Brazil, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, zilikubaliana kuhusu umuhimu wa kushughulikia suala la maendeleo endelevu kwa kuunganisha mihili yake mitatu, ambayo ni ukuaji wa kiuchumi, maendeleo ya kijamii, na uhifadhi wa mazingiza. Nchi hizo zinatambua kwamba ili kuboresha sera, hatua pana zaidi za maendeleo zinahitajika kutokana na pato kubwa zaidi la taifa.
chanzo: DW
Mwandishi: Dalila Athman/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)