Leo ni siku ya kimataifa ya kupinga hukumu ya kifo, ambapo
ingawa nchi nyingi duniani zinajiepusha kutekeleza hukumu hiyo, bado
kuna mataifa 57 ambayo bado yanaendelea nayo, ikiwemo Gambia
inayolaumiwa vikali duniani.
Miongoni mwa maandamano ya kupinga hukumu ya kifo nchini Marekani.
Licha ya taifa hilo la Afrika ya Magharibi kufahamika kwa uvunjaji wa haki za binaadamu chini ya utawala wa Rais Yahya Jammeh, lakini kuwanyonga wafungwa tisa kwa wakati mmoja kuliushitua ulimwengu.
“Watu huhukumiwa kifo kwa makosa ya kisiasa na uhaini, ambapo ni kinyume na viwango vya kimataifa. Tumesikia kuhusu kuwapo kwa mateso dhidi ya wanaohukumiwa kifo. Pia Gambia kuna ukandamizaji dhidi ya uhuru wa maoni. Hivyo, kuna masuala mengi ya haki za binaadamu ya kutia wasiwasi." Anasema Lisa Sherman Nicholas, mtaalamu wa masuala ya Gambia katika shirika la Amnesty International.
Rais Jammeh aliingia madarakani mwaka 1994 kwa mapinduzi ya kijeshi. Miongoni mwa wapinzani wake, huwaweka kwenye gereza liitwalo “Kituo cha Maili Mbili”, ambalo mwenyekiti wa Asasi za Kiraia wa Gambia, Banka Manneh, analiita “mtego wa mauti”:
“Hali kwenye Kituo cha Maili Mbili ni mbaya mno kiasi ya kwamba aidha unakufa ndani ya jela hiyo, au unakufa baadaye kutokana na madhara utakayoyapata ukiwa kifungoni. Mara nyingi wanajeshi au vikosi vya usalama ndio huhukumiwa kifo au vifungo vya maisha, lakini mfumo wa jela hiyo ni huu: chakula chake ni kibaya sana kiasi ya kwamba mwili wako unavimba na unakufa kifo kibaya sana.”
Miongoni mwa walionyongwa mwezi Agosti, kulikuwa na wawili wenye uraia wa Senegal, na hivyo nchini Senegal kukafanyika maandamano makubwa dhidi ya hatua hiyo.
Kwa mujibu wa Manneh, hata hivyo, hukumu hiyo imechochea uthubutu miongoni mwa wananchi, ambao sasa wanajiuliza ikiwa ni sahihi kuendelea kutishwa na serikali wakatishika.
Jumuiya ya kimataifa ilitishia kuiwekea vikwazo Gambia na kumtolea wito Rais Jammeh kuheshimu viwango vya kimataifa. Mashirika ya haki za binaadamu pia yalilaani njia iliyotumika kuwanyonga watu hao.
Kampeni ya kupinga hukumu ya kifo inayoendeshwa na Amnesty International.
Huenda shinikizo la kimataifa lilisaidia kidogo, kwani watu 38 waliokuwa wanyongwe katikati ya mwezi Septemba hawakunyongwa tena. Msemaji wa Rais wa Gambia alisema kwamba hukumu hizo zimesitishwa kwanza, hatua ambayo Manned aliilaribisha, lakini bado ana shaka nao.
“Ni habari njema, lakini serikali imeuita kuwa ni uamuzi wa muda, maana yake nĂ kuwa wanaweza kurudia kunyonga wakati wowote wakitaka. Na kwa kuzingatia yote aliyokwishayafanya Rais Jammeh, hajui kuyathamini maisha ya mwanaadamu. Anaweza tu kuamka asubuhi moja na kuamua kuanza tena kunyonga.” Anasema Manneh.
Ama ikiwa Umoja wa Ulaya unaiwekea Gambia vikwazo baada ya kusitisha kuwanyonga watu wake, bado ni suala lisilo jawabu. Lakini katika siku ya leo ya kupambana na hukumu hiyo duniani, wataalamu wa Umoja wa Ulaya na Afrika wanakutana na watatoa mapendekezo yao kwa mawaziri wa Umoja wa Ulaya. Kwa mujibu wa msemaji wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Ulaya, inaweza kuchukua muda mrefu kabla ya uamuzi kufanyika.
Mwandishi: Sarah Steffen/Eric Segueda/Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Daniel Gakuba
chanzo: idhaa ya kiswahili ujerumani
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa