Profesa Ibrahim Lipumba |
Chama
cha Wananchi (CUF) kimesema licha ya taifa kuwa na rasilimali nyingi
kama ardhi na madini mbalimbali wanaonufaika ni matajiri wachache
kutokana na kukosekana kwa uongozi imara.
Mwenyekiti
wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hayo jana
katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam katika mkutano wa
hadhara wa uzinduzi wa operesheni 'Mchakamchaka chinja hadi 2015
tunamaliza.'
Katika
operesheni hiyo, CUF inakusudia kutembelea mikoa sita ya Arusha,
Kigoma, Tabora na Kagera na mingine miwili itajulikana baadaye.
Alisema
Tanzania ina mapato makubwa lakini hayatumiki katika kukabiliana na
umaskini kwa kuwa yanatumika kuwanufaisha wachache kutokana na ukosefu
wa uongozi imara,hivyo nchi kurudi nyuma kimaendeleo hali ambayo
alisema ni aibu.
Akizungumzia
sera ya Kilimo Kwanza alisema inawanufaisha wakulima wakubwa tu kwa
kupora ardhi kubwa huku wakulima wadogo wakibakia kama vibarua kinyume
cha malengo ya sera ya kuwasaidia wakulima wadogo.
sehemu ya umati wa wafuasi na wanachama wa CUF |
Alisema
serikali imekuwa ikiibiwa na watu wachache wakiwemo mawaziri na
wakurugenzi kwa kuandaa miradi hewa ya kijanjajanja kwa lengo la
kujipatia fedha huku Watanzania wengi wakiendelea kuwa maskini wa
kutupwa na baadhi ya vijana kuwa bomu linalotarajiwa kulipuka wakati
wowote kutokana na kukosa ajira.
Profesa
Lipumba pia alizungumzia mauaji ya Mwandishi wa habari wa Kituo cha
Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, akiwa kazini kuwa ni aibu
kwa jeshi la polisi na taifa kwa ujumla kwani Tanzania haiko vitani.
Pia
alilaaini vikali mauaji hayo na kusema kuwa ni haki ya mwandishi
kupata habari bila kubugudhiwa kwa kuwa wao ni daraja muhimu kati ya
wananchi matukio yanayotokea nchini.
Naye
Haji Duni ambaye pia ni Waziri wa Afya katika Serikali ya Umoja wa
Kitaifa Zanzibar, alisema anashangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Mstaafu
Frederick Sumaye, kuwa Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa kupita
kiasi na kuua watu wakati yeye ndiye aliyeasisi polisi kuua raia wakati
akiwa madarakani kama waziri mkuu kwa kipindi cha miaka 10 chini ya
serikali ya awamu ya tatu.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa