Waziri Mwakyembe alipotembelea ukarabati wa Mabehewa ya huu mradi wa Dar es salaam |
Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakyembe amesema huduma za treni Dar es salaam kwa kuanzia zitakua kutoka stesheni ya reli Dar es salaam hadi Ubungo maziwa ikiwa ni kilomita 12 pamoja na Mwakanga hadi Kurasini kupitia stesheni ya Dar es salaam kilomita 34.5.
Amesema “kazi ya ukarabati wa njia na injini tatu za treni na mabehewa 14 ya abiria imeanza na inatarajiwa kukamilika oktoba 2012 ambapo huduma hii itaanza kwa kuwa na treni mbili ambazo zitatoa huduma asubuhi na jioni kuanzia jumatatu mpaka jumamosi”
Dr Mwakyembe ambae amepata pongezi kubwa pia baada ya kufichua uozo kwenye shirika la ndege Tanzania, amesema Treni hizo zitasimama kwenye vituo sita ambavyo ni stesheni ya Dar es salaam, Kamata, Buguruni kwa Mnyamani, Tabata Matumbi, Mabibo na Ubungo Maziwa na kila treni itakua na mabehewa sita yenye uwezo wa kubeba abiria waliokaa na waliosimama elfu moja kila safari na inakisiwa treni hizo zitaweza kusafirisha watu elfu kumi na sita kwa siku.
Baada ya kusema hayo, Dr Mwakyembe amewasihi wafanyabiashara kuwekeza kwenye mradi wa maegesho ya magari kwenye eneo la eka nne Ubungo lililotengwa kwa ajili ya watu wanaotoka Kibaha, Kimara, Kiluvya, Mbezi Luis na kwengine kwa ajili ya kupaki magari yao Ubungo kisha kupanda treni kwenda stesheni ya Dar es salaam.
Kwa upande wa reli ya Tazara ukarabati wa injini tatu na treni za mabehewa 14 unaendelea na unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu ambapo huduma hiyo ya treni itakua na njia mbili, Mwakanga kwenda Yombo mpaka stesheni ya Tazara ikichukua dakika 30 alafu njia ya pili Mwakanga kwenda Yombo mpaka Kurasini ikichukua dakika 40, itakua na vituo 14 ambavyo ni stesheni ya Tazara, kwa fundi umeme, Yombo, Kwa Limboa, Lumo, Kigilagila, Barabara ya Kitunda Kipunguni B, Moshi Bar, Majohe, Shule ya sekondari Magnus, Mwakanga, Chimwaga, Maputo, Mtoni relini, Kwa Aziz Ally relini hadi Kurasini.
Akisoma bajeti mpya ya wizara ya Uchukuzi, Dr Mwakyembe amesema ili kuimarisha na kuboresha utendaji wa TRL Wizara imetenga shilingi bilioni 104 kwenye bajeti ya 2012/2013 zitakazotumika kwenye miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzijenga upya injini 8 za treni, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa treni mpya 13, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa Mabehewa mapya ya abiria 22, kukarabati mabehewa mabovu ya mizigo 125, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya mizigo 274, kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa mabehewa mapya ya breki 34 na ukarabati wa karakana za Tabora na Dar es salaam ambapo katika fedha hizo shilingi bilioni 18.9 zimetengwa kwa ajili ya kulipa madeni ya kimkataba na IFC ya Uganda na wadai wa hapa nchini.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa