KESI ya msanii wa fani ya filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu Lulu, imeahirishwa hadi Agosti 20 mwaka huu, kutokana na Jaji anayeisikiliza, DK Fauz Twaib, kuwa na majukumu mengine.Akiahirisha kesi hiyo jana, Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Amir Msumi, alisema Jaji DkTwaibu, anakabiliwa na majukumu mengine.
“Jaji Twaib ni Mwenyekiti wa Baraza la Kodi na pia ni Mwalimu wa Sheria katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivyo kwa sasa anatekeleza majukumu mengine katika nafasi hizo.Kwa hiyo kesi hiyo inaahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu,” alisema Msumi.
Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, yanayodaiwa kufanyika April 7 mwaka huu nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kesi hiyo ya msingi haijaanza kusikilizwa, tayari imeshafikia ngazi ya Mahakama ya Rufani, baada ya kuibuka kwa utata wa umri wa mshtakiwa huyo.
Utata huo uliiobuka baada ya mawakili wanaomtetea msanii huyo, kuomba kesi isikilizwe katika Mahakama ya Watoto kwa madai kuwa mteja wao bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama, inavyoonyesha katika hati ya mashtaka.
Katika kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo la mawakili watatu, Kennedy Fungamtama (kiongozi wa jopo), Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tangantyika(TLS) Peter Kibatala na Fulgence Massawe wa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Juni 11 mwaka huu, Mahakama Kuu ilikubali maombi ya mawakili hao, kuhusu kufanya uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa, baada ya Mahakama ya Kisutu kuyakataa.
Mahakama Kuu ilitarajiwa kuanza uchunguzi huo wa umri halali wa mshtakiwa Juni 25 mwaka huu kwa kusikiliza hoja za kila upande na kupitia vielelezo mbalimbali kuhusu umri wa mshtakiwa.
Hata hivyo hatua hiyo ilikwama na kulazimika kusimama baada ya upande wa mashtaka, kuitaarifu mahakama kuwa, umewasilisha katika Mahakama ya Rufani, maombi ya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu, kuhusu kukubali kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo, kama ulikuwa sahihi.
Kwa mujibu wa kiapo kinzani, wakijibu maombi ya Jamhuri kwa Mahakama Rufani, mawakili hao wanadai kuwa Mahakama Kuu ilichukua hatua sahihi kulingana na mazingira ya kesi kwa ajili ya kutenda haki na kwamba haikupotoka katika kuamua kushughulikia suala hilo.
Vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa mshtakiwa katika Mahakama Kuu ni pamoja na hati za viapo vya wazazi wa mshtakiwa (mama, Lucresia Augustin Kalugila na baba, Michael Kimemeta), cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vya mshtakiwa vinaonyesha kuwa ana umri wa miaka 17.
Vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16 mwaka1995 katika Kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23 mwaka 2004.
Lakini vielelezo ya upande wa mashtaka navyo vinaonyesha kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa zaidi ya miaka 18 yaani miaka 21. Vielelezo ni pamoja na maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa