ELECTIONS COMMITTEE
                       TAARIFA  KWA VYOMBO YA HABARI
06 MACHI 2012
UFAFANUZI KUHUSU MAJUKUMU,  WAJIBU NA MAMLAKA YA KAMATI YA UCHAGUZI NA
 MAELEZO YA KINA KUHUSU MAAMUZI  YA KAMATI ZA UCHAGUZI ZA TFF KUHUSU MAOMBI 
YA NDG. MICHAEL RICHARD WAMBURA  KUGOMBEA UONGOZI KWENYE UCHAGUZI WA 
1.                   USIMAMIZI WA  CHAGUZI ZA WANACHAMA WA TFF
            Muundo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umeelezwa wazi  kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 18. Kamati ya Uchaguzi ya TFF ni moja kati ya  vyombo sita  vilivyoainishwa katika Muundo wa TFF. Majukumu, wajibu na mamlaka ya  vyombo vya TFF yameainishwa katika Katiba ya TFF na Kanuni zilizotungwa na  kuidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kuzingatia Ibara ya 34 ya Katiba  hiyo.
            Majukumu, wajibu na mamlaka ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF yameainishwa  kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 49 na kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF na Kanuni  za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Mbali na majukumu na wajibu wa kusimamia  uchaguzi wa TFF na chaguzi za wanachama wake na kuishauri Kamati ya Utendaji ya  TFF kuhusu Kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inao wajibu wa kulinda  Katiba na Kanuni za uchaguzi za TFF na Katiba ya FIFA na Katiba za wanachama wa  TFF kama ilivyotamkwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6 na Kanuni za  Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26. Uchaguzi  Mkuu wa TFF hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF. Chaguzi za  wanachama wa TFF na wanachama wao hufanyika kwa mujibu wa Kanuni za uchaguzi za  wanachama wa TFF na si vinginevyo. Kanuni hizi zimeainisha taratibu mbalimbali  ambazo lazima zizingatiwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa ukataji  rufaa katika ngazi mbalimbali za uchaguzi. Vyombo na Kamati zote za  TFF,  Wanachama wote wa TFF na wanachama wao, na wadau wote wa soka wanao wajibu wa  kuheshimu Kanuni mbali mbali za TFF ambazo ni pamoja na Kanuni za  Uchaguzi.
2.                   MAAMUZI KUHUSU  MAOMBI YA UONGOZI YA NDG. MICHAEL WAMBURA 
Kwa muda mrefu  pamekuwepo na taarifa mbalimbali kupitia vyombo vya habari zenye lengo la  kuwafanya wadau na wapenzi wa soka na umma wa watanzania kwa ujumla kuaminishwa  kuwa Ndg. Michael Wambura huonewa na vyombo vya TFF vinavyosimamia uchaguzi kila  anapoomba nafasi za uongozi katika TFF. Baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya  wapenzi wa soka wamesikika wakisema kwamba kuenguliwa kwa Ndg. Michael Wambura  kugombea uomgozi ni kutokana na kuogopwa na viongozi wa TFF. Kamati ya Uchaguzi  ya TFF inapenda kufafanua kwa kina maamuzi yote yaliyofanyika kuhusu maombi yote  ya uongozi ya Ndg. Michael Wambura na kuweka wazi vielelezo vilivyotumika  kufikia maamuzi hayo ili umma wa watanzania wafahamu kinagaubaga ukweli kuhusu  maamuzi hayo:
            UCHAGUZI MKUU  WA TFF 2008
            Kamati ya  Uchaguzi ya TFF ilimwengua Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Makamu wa  kwanza wa Rais wa TFF kwa kutokidhi matakwa ya uadilifu kwa mujibu wa Kanuni za  Uchaguzi na Katiba ya TFF. Ndg. Michael Wambura hakuridhika na uamuzi huo na  alikata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa ya TFF. Hata hivyo baada ya Kamati ya Rufaa  kupitia nyaraka mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Kamati hiyo ikiwa ni pamoja  na ripoti ya ukaguzi wa maheabu ya TFF/FAT kwa mwaka 2002, 2003 na 2004 rufaa  yake ilishindwa baada ya Kamati ya Rufaa kuridhika na kuweka bayana kuwa mwomba  rufaa, Michael Richard Wambura aliipa Zabuni kampuni yake iitwayo Min Investments & Commercial Services  Co. wakati akiwa Katibu Mkuu wa FAT/TFF na hivyo kushindwa kukudhi kigezo  cha uadilifu. Katika kufikia maamuzi  yake, Kamati ya rufaa pia ilibaini kuwa Ndg. Michael Richard Wambura alionyesha  kuwa alikuwa amechana na umiliki wa kampuni hiyo kuanzia tarehe 12 Novemba 2003  kwa mabadiliko yaliyotekelezwa tarehe 28 Februari 2007 kwa malipo ya Shs.  34,500/= ya “exchequer receipt No.  28173444’. Hata hivyo, Kamati ya Rufaa iliridhika kuwa utekelezaji wa  mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo ulichukua takribani miezi arobaini (40).  Baada ya majadiliano ambayo yalikuwa yamekitwa (pegged) kwenye uadilifu (integrity), Kamati ya Rufaa iliridhika  kuwa taswira inayojitokeza kwenye muktadha imegubikwa na wingu jeusi la mashaka  kuhusu “integrity” ya Muomba Rufaa  (Ndg. Michael Richard Wambura).
            Uthibitisho  kwamba mmilki wa Kampuni ya Min Investments & Commercial Services  Co ni Ndg. Michael Richard Wambura ulitolewa na Msajili wa Makampuni  (Business Registration and Licensing Agency-BRELA) kwa barua yenye Kumbukumbu  Na. MITM/RBN/93017 ya tarehe 16 Agosti 2006. Kampuni hiyo ilisajiliwa tarehe 17  Julai 1992.
            Kamati ya  Uchaguzi ya TFF inatoa sehemu ndogo tu ya ubadhirifu uliokuwa unafanywa kwa  kutumia Kampuni hiyo (Min Investments  & Commercial Services Co) ya Michael Wambura kinyume na utaratibu wa  utoaji tenda wa FAT/TFF na malipo aliyojilipa bila maelezo yoyote kama  ilivyoainishwa kwenye Ripoti ya Ukaguzi wa Mahesabu iliyowasilishwa na wakaguzi  tarehe 19 Septemba 2005 na Ripoti maalumu ya ukaguzi iliyowasilishwa Novemba  2006, kama ifuatavyo:
(i)       Tarehe 28  Julai 2004 Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alilipwa Dola za Kimarekani  16,548.00 (US$ 16,548 sawa na Tshs. 17,170,040 wakati huo) kwa ununuzi wa samani  (furniture) za Hosteli ya TFF. Pesa hizo zilizoombwa kulipwa kwa Michael Wambura  zimeonyeshwa kwenye fomu ya malipo ya TFF ya tarehe 28 Julai 2004. Pesa hizo  zilipokelewa na Kampuni ya Min  Investments & Commercial Services Co na kuthibitisha kupokelewa na  kampuni hiyo kwa risiti Na. 020 ya tarehe 21 Julai 2004 ya kampuni hiyo, ingawa  hapakuwa na maombi ya manunuzi (order) iliyokuwa imefanywa na TFF kwa kampuni  hiyo.  
(ii)     Baada ya  kujilipa pesa zilizotajwa hapo juu, kesho yake tarehe 29 Julai 2004 Ndg. Michael  Wambura akiwa Katibu Mkuu wa TFF alijilipa Dola za kimarekani 25,000.00 (US$  25,000.00 sawa na Tshs. 25,937,500 wakati huo), kama ilivyoonyeshwa kwenye vocha  ya malipo ya TFF Na. 5324 ya tarehe tajwa hapo juu, ikionyesha kuwa ni kwa ajili  ya malipo ya samani za Hosteli (US$ 15,000.00) na malipo ya awali ya Gari (US$  10,000.00). Ndg. Michael Wambura alithibitisha kupokea malipo hayo. Ripoti ya  Ukaguzi inabainisha wazi kuwa vifaa vichache vilivyonuliwa kwa hosteli ya TFF  thamani yake haikuainishwa na hapakuwa na gari lililolipiwa malipo ya awali  katika vitabu vya mahesabu ya TFF.
(iii)    Katika kipindi  cha mwaka 2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijikopesha jumla  ya Tshs. 36,850,750 bila idhini ya Kamati ya Utendaji.
(iv)    Tarehe 20 Mei  2002 Ndg. Michael Wambura akiwa Katibu Mkuu wa FAT alijilipa Tshs. 12,147,837  ambazo hazina maelezo yoyote.
(v)     Imebainishwa  wazi kuwa FAT/TFF ilikuwa mfilisi katika kipindi cha 2002-2004 (Nukuu: “The  Association was actually insolvent during the period.”)
            Kamati inaweka  wazi tena kwamba maamuzi yaliyofikiwa na Kamati ya Rufaa ya kumuengua Michael  Wambura kwenye uchaguzi Mkuu wa TFF yanaweza tu kubadilishwa na Mahakama ya  usuluhishi wa masuala ya michezo (CAS) endapo Michael Wambura atakata rufaa CAS  kupinga maamuzi hayo na kushinda rufaa, na si vinginevyo.
            MAAMUZI YA  MKUTANO MKUU WA TFF 2007
             Mkutano Mkuu wa TFF ambacho ndicho chombo cha juu kabisa cha TFF (Supreme Authority of TFF) katika kikao  chake mwaka 2007 kilipitia ripoti za ukaguzi wa mahesabu ya FAT/TFF kwa kipindi  cha mwaka 2002 hadi 2004 na baada ya kujiridhisha kuhusu ubadhirifu uliofanywa  na Ndg. Michael Wambura, Mkutano Muu wa TFF uliamua kwamba Ndg. Michael  Wambura afikishwe kwenye vyombo vya dola kwa ubadhirifu wa fedha za FAT/TFF  alioufanya kama ilivyoainishwa kwenye ripoti za ukaguzi wa Mahesabu.  Sekretarieti ya TFF mwaka 2007 ikitekeleza maagizo ya Mkutano Mkuu wa TFF na  suala hilo lilpelekwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi ilithibitisha maombi ya  TFF kwa barua  yake ya tarehe 18 Januari 2008 na kumfungulia jalada  Ndg Michael  Wambura kwa kosa la wizi  akiwa Mtumishi. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaheshimu  maamuzi ya Mkutano  Mkuu wa TFF na hadi sasa haijataarifiwa kwa maandishi na chombo chochote kama  suala hilo limefikia ukomo wa aina yoyote. 
            UCHAGUZI WA  KLABU YA SIMBA MWAKA  2010
            Ndg. Michael  Richard Wambura aliomba kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba. Hata  hivyo alikatiwa rufaa na Ndg. Daniel T. Kamna  kwa kutotimiza matakwa ya Ibara  ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF kama ilivyoamuliwa na Kamati ya  Uchaguzi ya TFF na pia Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 wakati alipoomba  kugombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF. Kamati ilikubaliana na  maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya TFF mwaka 2008  kwamba Bw. Michael R. Wambura  si mwadilifu  kama ilivyonyeshwa kwenye aya ya  2.1 na 2.2 hapo juu na hivyo hakukidhi matakwa ya Ibara ya 29(7) ya Katiba ya  TFF na Ibara ya 9 ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF.  Kamati ilimuondoa  kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Simba SC.
            Baada ya  maamuzi hayo ya Kamati, Ndg. Michael Richard Wambura alikwenda Mahakamani na  akafungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es salaam dhidi ya  Mwenyekiti wa Klabu ya Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike. Kwa  kufanya hivyo alivunja Katiba ya Klabu ya Simba na kukiuka Katiba ya TFF Ibara  ya 12(2) (e) na Katiba ya FIFA Ibara ya 64(2). Klabu ya Simba ilichukua hatua za  kikatiba, na katika kikao chake cha 5/5/2010, ilimsimamisha uanachama Ndg.  Wambura kwa kukiuka katiba ya klabu hiyo. Klabu ya Simba iliitaarifu TFF uamuzi  huo kwa barua yenye Kumbukumbu Na. SSC/MMKT/162/Vol.40/10 ya tarehe 06 Mei 2010  iliyoambatanishwa na Muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanya  uamuzi huo. Uamuzi wa kumrudishia uanachama unafanywa na Mkutano Mkuu wa Klabu  ya Simba. TFF haijapokea taarifa yoyote kutoka Klabu ya Simba kwamba Mkutano  Mkuu wa Klabu hiyo ulikwisha msamehe. Kwa hali hiyo taarifa ya kusimamishwa  kwake iliyotumwa TFF mwezi Mei 2010 itaendelea kuzingatiwa hadi hapo Klabu ya  Simba itakapo ijulisha TFF mabadiliko ya maamuzi hayo.
3.                   MAAMUZI KUHUSU  UCHAGUZI WA FAM
            Kamati ya  Uchaguzi ya TFF ilimuondoa Ndg. Michael Wambura kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa  FAM kwa kuwa alifungua kesi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es  salaam dhidi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba akiwa ni mwanachama wa Klabu ya  Simba kuzuia uchaguzi wa klabu ya Simba usifanyike, jambo ambalo ni uvunjaji wa  Katiba ya Klabu ya Simba, ukiukwaji wa Katiba ya FAM, TFF na FIFA. 
            Pia, Kamati ya  Uchaguzi ya TFF iliweka wazi kama ilivyobainisha kwenye uchaguzi wa Klabu ya  Simba kwamba suala la uadilifu wa Ndg. Wambura lilishafanyiwa maamuzi na Kamati  ya Rufaa ya TFF mwaka 2008 kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa TFF. Kwa  mujibu wa Kanuni za Uchaguzi huo na Katiba ya TFF Mamlaka pekee inayoweza  kutengua uamuzi huo ni Mahakama ya Usuluhishi wa masuala ya Michezo (CAS) iliyo  na makao yake Lausanne, Switzerland.
            Baada ya  uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia baadhi ya vyombo vya TFF  vikishughulikia masuala ya uchaguzi kinyume na matakwa ya Katiba ya TFF na  Kanuni za Uchaguzi, kama ifuatavyo:
(i)       Katika hali  isiyozingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF, Kamati ya Nidhamu ilipokea  malalamiko ya Ndg. Michael Wambura yaliyoitwa ‘rufaa’. Kwa kuwa hakuna utaratibu  wa masuala ya uchaguzi kukatiwa rufaa kwenye Kamati za nidhamu katika ngazi zote  za uchaguzi na hivyo pia kutokuwepo ada ya ‘rufaa’ za aina hiyo, mlalamikaji  alilazimisha kupokelewa ada ya Tshs 300,000/= ambayo ni ada inayotumika kwa  rufaa za Ligi Kuu ya Vodacom ambayo  imeainishwa katika Ibara ya 17 ya  kanuni za mashindano hayo. Ada hiyo iliwekwa (deposited) kwenye Akaunti ya TFF  bila ridhaa ya TFF. Pamoja na mapungufu hayo “rufaa’ hiyo ilisikilizwa na Kamati  ya Nidhamu na kutolewa maamuzi. Mlalamikaji hakuridhika na maamuzi ya Kamati  hiyo na aliamua kukata ‘rufaa’ katika Kamati ya Rufaa ya TFF. 
(ii)     Kamati ya  Rufaa ya TFF ilipokea na kusikiliza ‘rufaa’ ya Ndg. Michael Richard Wambura,  kinyume na matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kwa kuwa kwa  mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF hakuna rufaa inayokatwa kwenye  Kamati hiyo, hivyo kutokuwapo ada yoyote kwa “rufaa” ya aina hiyo, ili kutimiza  azma ya kusikiliza ‘rufaa’ hiyo, palifanyika juhudi za kulazimisha kupokelewa  ‘ada’ ya Shilingi 500,000/= ambayo ni ada ya rufaa za mashindano ya Ligi Kuu ya  Vodacom ambayo imeainishwa pia katika Ibara ya 17 ya kanuni za mashindano ya Ligi  Kuu ya Vodacom. Hata hivyo, ada hiyo ambayo si halali, haikupokelwa na  Sekretarieti ya TFF  baada ya kushindikana kuainisha ada ya mashindano ya Ligi  Kuu ya Vodacom na masuala ya Uchaguzi.  Bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za  wanachama wa TFF na Katiba ya TFF Ibara ya 47(4) inayotamka na kuikataza Kamati  ya Rufaa  kusikiliza rufaa kwa mambo yaliyowekewa ukomo na Kanuni husika; Ibara  hiyo inatamka; ‘The Appeal Committee  shall be responsible for hearing appeals against decisions from the Disciplinary  Committee that are not declared final by relevant regulations as well as  decision passed by the players’ Status Committee concerning the eligibility of  players for the teams’, Kamati hiyo ilisikiliza malalamiko ya Ndg. Michael  Richard Wambura na kutoa uamuzi bila kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za wanachama  wa TFF ambazo ni ‘relevant regulations’ na Ibara ya 12(4) ya Kanuni hizo kutamka  wazi kuwa;  ‘The decisions of the TFF  Elections Committee are final and conclusive and shall not be monitored by any  other body’.
(iii)     Kamati ya  Uchaguzi ya TFF inatamuka wazi kuwa utaratibu mzima uliotumika kupokea rufaa  hiyo toka Kamati ya Nidhamu hadi ya Kamati ya Rufaa haukufanyika kwa mujibu wa  taratibu za ukataji rufaa zilizoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za wanachama  wa TFF.  Ukataji rufaa huo uliongozwa zaidi na hila kuliko dhamira ya kuheshimu  taratibu zilizowekwa. Mbali na kutumia kanuni za Ligi kuu ya Vodacom kusikiliza  ‘rufaa’ hizo, uthibitisho mwingine wa hila na ujanjaujanja ni pale mlalamikaji  alipokwenda kuweka kwenye akaunti ya TFF ada ya rufaa ya mashindano ya Ligi Kuu  ambayo haitambuliki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi na kutumia vyombo vya  habari kutangaza kitendo hicho, lakini baada ya kutolewa maamuzi na Kamati ya  Rufaa alienda kimya kimya TFF kuchukua ada hiyo ambayo ni ya rufaa kwa  mashindano ya Ligi kuu.
(iv)    Kamati ya  Uchaguzi ya TFF, kwa mamlaka yaliyo kasimiwa kwake na Katiba ya TFF Ibara ya  49(1) , Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 6, Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa  TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(4) na 26(2), na pia kwa mamlaka yaliyoainishwa  katika Katiba za wanachama wa TFF kuhusu uchaguzi, katika kikao chake  kilichofanyika 03 Desemba 2011 iliamua na inatamka wazi kuwa maamuzi  yaliyofanywa na Kamati ya Rufaa ni BATILI kwa kuwa hayakuzingatia Kanuni za  Uchaguzi za wanachama wa TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaziagiza Kamati zote  za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao kuendelea kuzingatia Kanuni za  Uchaguzi katika utendaji wa kazi zao za kuendesha na kusimamia chaguzi zote za  vyama vya mpira wa miguu nchini, ikiwa ni pamoja na kutozingatia maamuzi yoyote  ya uchaguzi yatakayofanyika kinyume na Kanuni za Uchaguzi.
4.                   TAARIFA ZA  UDANGANYIFU KUTOKA KWA BAADHI YA WAGOMBEA UONGOZI KWENYE VYAMA WANACHAMA WA  TFF.
            Kamati ya  Uchaguzi inapenda kuwakumbusha wadau wote wa soka wenye nia ya kugombea uongozi  TFF na vyama wanachama wa TFF kuwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF ibara  ya 25(8) na Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF Ibara ya 26(8)  ni makosa  kuwasilisha taarifa za udanganyifu kwenye Kamati ya Uchaguzi. Kanuni hizo  zinatamka kuwa; During the election  process any person or member who contravenes this code or provides false  particulars or qualification, may be penalized to a fine not exceeding five  hundred thousand shillings or be barred to participate in the election process  for 2 years or for both a fine and such barring, provided that the General  Secretary lodges a complaint to the TFF judicial organ for disciplinary  action.
            Kamati  imebaini kuwa baadhi ya wagombea walifanya udanganyifu kuhusu vyeti halisi  walivyowasilisha kwenye uchaguzi wa FAM na pia baadhi ya waombaji uongozi katika  uchaguzi wa klabu ya Villa. Kwa mfano mwombaji aliyeomba kugombea nafasi ya  Mwenyekiti wa Klabu ya Villa cheti chake cha Elimu ya Msingi alichowasilisha  kwenye Kamati ya Uchaguzi kina utata. Vyote hivyo viko katika hatua za uhakiki  kwenye mamlaka husika, uhakiki utakapokamilika Kamati itachukua hatua kwa mujibu  wa Kanuni tajwa hapo juu.
            Kamati  imebaini na kujiridhisha kuwa Ndg. Michael Wambura alitoa taarifa zinazokinzana  kwenye Kamati ya Uchaguzi kuhusu umri wake. Katika Uchaguzi wa Klabu ya Simba  mwaka 2010, aliwasilisha taarifa kwamba amezaliwa mwaka 1967 lakini katika  uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara aliwasilisha taarifa kwamba  alizaliwa mwaka 1965. Taarifa za umri zinazokinzana za mwombaji uongozi  zinashiria mashaka ya umakini na uadilifu wa mgombea hasa ikizingatiwa kuwa  nafasi ya uongozi ya mwenyekiti kwa vyama wanachama wa TFF na  Rais wa TFF zina  ukomo wa wa umri. Kamati itachukua hatua zilizoainishwa kwenye Kanuni za  Uchaguzi tajwa hapo juu.
5.                    KAULI ZENYE LENGO LA KUVURUGA CHAGUZI ZA WANACHAMA WA  TFF.
             Katika siku za karibuni Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeshuhudia kauli  amabazo si za  kiwanamichezo zenye lengo la kuleta vurugu katika michakato ya Uchaguzi. Kwa  mfano  kauli za kuwahamasisha wadau wa soka kwenda mahakamani kwa masuala ya michezo,  hususan, kupinga michakato ya uchaguzi ni uvunjaji wa Kanuni za Uchaguzi na  Katiba ya TFF na FIFA. Kamati inawataka wadau wote wa soka kuheshimu na  kuzingatia Kanuni na taratibu za uchaguzi na Katiba ya TFF, vinginevyo Kamati  haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi.
Deogratias J.  Lyatto
MWENYEKITI
KAMATI YA  UCHAGUZI
SHIRIKISHO LA MPIRA  WA MIGUU TANZANIA
 
 
 
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa