Translate in your language

Friday, February 10, 2012

HATIMAE SERIKALI NA MADAKTARI WAFIKIANA

Tamko la Kamati: MAAZIMIO YA KIKAO CHA WAZIRI MKUU; MADAKTARI

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo wa Madaktari, Dkt. Stephen Ulimboka baada ya kuzungumza na madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es salaam, Februari 9, 2012. (Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu)
TAARIFA KWA UMMA NA MADAKTARI WOTE NCHINI JUU YA MAAMUZI YALIYOFIKIWA LEO FEBRUARY 9, 2012 KUFUATIA MKUTANO KATI YETU NA WAZIRI MKUU MHE. MIZENGO PINDA KATIKA UKUMBI WA CPL, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI

Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari nchini inapenda kuwajulisha madaktari wote pamoja na kada nyingine zote za afya nchini juu ya kile ambacho kimejiri katika siku ya leo ya tarehe 09.02.2012 ikiwa ni matokeo ya kikao wanataaluma wa kada za afya na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda na baadaye kufuatiwa na kikao kati ya madaktari na kada nyingine za afya.

Ifahamike kuwa kama Kamati tulipata mwaliko wa kushiriki katika Mkutano huo ambapo ilitarajiwa kuwa Mhe, Waziri mkuu atafika kwa nia ya kutoa mrejesho wa madai ya madaktari yaliyowasilishwa mezani kwake mnamo tarehe 23.01.2012. Madai yetu yalikuwa manane na Mh Wazizri mkuu aliweza kutoa maelezo ya dai moja baada ya lingine.

Miongoni mwa madai ambayo mpaka sasa yamepatiwa majibu ya kuridhisha ni pamoja na;

Kuwawajibisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wakiwemo Katibu Mkuu Mama Blandina Nyoni , na Mganga Mkuu wa Serikali Dr. Deo Mtasiwa. Aidha Mh waziri mkuu alisema kuwa ameshalifikisha kwa Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala zima la kuwawajibisha watendaji wa wakuu wa kisiasa wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao ni Waziri Mh Hadji Mponda na Naibu Waziri Mhe. Lucy Nkya. 


Kama sehemu ya maridhiano, Mh Waziri Mkuu pia aliahidi mbele ya mkutano kuwa hakutawepo na unyanyasaji au vitisho vya aina yoyote ile kwa wale wote walioshiriki katika kushinikiza Serikali kutatua kero hizo. Aidha kama sehemu ya maridhiano, Mh waziri Mkuu pia alifuta zuio la madaktari kutokufanya mikutano. Lakini pia, Mh waziri Mkuu alisema kuwa Serikali haina kusudio la kumfukuza kazi mtumishi yeyote wa afya yule kazi aliyeshiriki katika mchakato huu wa kuishikiniza Serikali kutafuta ufumbuzi madai ya madaktari nchini. 

Aidha, Mh waziri Mkuu amesema “Interns” wote waliokuwa wamehamishwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wamesharudishwa bila masharti katika hospitali hiyo ili kuendelea na program kama kawaida. Hili pia linaambatana na kulipwa na kupewa stahiki zao zote. 

Pia suala la madaktari na familia zao kuwa na Kadi ya Bima ya Afya ya kijani( Green Card) limekubaliwa na kwa sasa tusubiri utekelezaji.

Pia ilikubaliwa kuwa madaktari watapata fursa ya kukopeshwa magari kama watumishi wengine wa umma. 

Mbali na madai hayo, pia Mh. Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi juu ya madai yanayuhusu maslahi ya watumishi wa afya ikiwa ni pamoja na Mishahara na Posho na stahiki mbalimbali. Lakini hata, Mh waziri Mkuu hakutoa majibu ya moja kwa moja ya kiwango gani kitakachoweza kulipwa na Serikali kama mishahara, posho na stahiki mbalimbali kwa minajili kwamba bado zinafanyiwa kazi na kamati ya wataalamu aliyoiunda ili waweze kumshauri. Aidha, Mh waziri Mkuu alisema kuwa kwa wakati huu inaweza kupandisha “on call allowances” za kada mbalimbali za afya kutoka shilingi 3,000 – 10,000/= na kufikia kati ya shilingi 5,000 hadi 25,000. Madaktari bado wanaona ongezeko hili halilingani na ukubwa wa kazi ifanywayo pindi mtumishi wa afya anapokuwa “on call” na hivyo basi kuendelea kupendekeza kuwa “on call” allowance iwe ni 10% ya mshahara wa mtumishi husika.

Pia Mhe, Waziri Mkuu hakuweza kueleza kinagaubaga mkakati kazi wa uboreshaji wa huduma za afya wapatayo wananchi wa Tanzania.

Baada ya tamko hilo la Serikali kumalizika, Mh Waziri Mkuu na ujumbe wake waliondoka, na Mkutano huo ukaendelea kwa Kamati kufanya Mkutano na madaktari wote, lengo ikiwa kujadili tamko hilo na kutoa maazimio.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu, madaktari walikubaliana kwamba; kwa kuwa Serikali imeanza kuonyesha nia ya kutatua tatizo hili kwa kutekeleza baadhi ya maazimio yetu, wajumbe kwa niaba ya madaktari wote nchi nzima tulikubaliana na kuazimia yafuatayo;

Kurudi kazini mara moja kuanzia kesho tarehe 10.02.2012 bila masharti yeyote.

Kamati ya jumuiya ya madaktari kama sehemu ya MAT kuendelea kukaa mezani ya majadiliano na Serikali ili kuanza kupitia madai hasa yale yanayohusu maslahi. 

Kukutana tena tarehe 03.03.2012 ili kupata mrejesho wa kiwango cha utekelezaji wa madai hayo kwa mujibu wa vikao vya majadiliano na makubaliano na hatimae kuchukua hatua zaidi.

Kujadili utekelezaji juu ya Kuwawajibisha Waziri na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi na Jamii.

Mwisho kabisa Madaktari wote kwa ujumla wake walilaani na kukemea kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwahoji wanaharakati wa haki za kibinaadamu na mashirika ya kijamii wakiwemo Dr. Hellen Kijo-Bisimba na Mama Ananilea Nkya na wanaharakati wengine wote waliokumbwa na kamata kamata hiyo na hivyo basi tunalitaka jeshi hilo kuwaachilia huru mara moja bila masharti yeyoye. 

Pamoja Tunaweza

Imetolewa na Kamati ya muda ya kushughulikia madai ya madaktari Tanzania

Dr, Ulimboka Stephen
Mwenyekiti.

No comments :

Post a Comment

here u,re comments/acha ujumbe wako hapa

Kijiweni (nipe 5)