Mjasiriamali Bwana Katala Maganga mkazi wa Kawe aliyekopeshwa trekta akiwa juu kwenye trekta hilo baada ya kukabidhiwa. |
Diwani Kawe, Hitech watoa mkopo wa trekta, mashine kwa wajasiriamali
Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Kampuni ya Hitech International kwa kushirikiana Ofisi Diwani wa Kata ya Kawe, Mutta Rwakatare, imetoa mkopo wa trekta wenye masharti nafuu ikiwa ni juhudi za kuwajengea uwezo wananchi kujiajiri na kukuza uchumi.
Hitech na ofisi ya diwani huyo zimeingia mkataba wa kuhamasisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kumiliki mashine za kutengeneza bidhaa za aina tofauti ili kujiajiri na kukuza kipato chao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi trekta hilo, Mutta alisema kata yake kwa kushirikiana na sekta binafsi inatekeleza kwa vitendo ya uchumi wa viwanda kwa kuwawezesha wananchi kumiliki mashine zinazoongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha.
"Kwa udhamini wa ofisi yangu wananchi wa Kawe wanaweza kumiliki mashine waitakayo baada ya kulipa kati ya asilimia 10 mpaka 30 bila kuhitaji dhamana. Hii inasaidia kuondoa vikwazo vya kukuza mtaji vilivyopo kwenye taasisi za fedha na benki," alisema Mutta.
Kumiliki mashine kutoka Hitech, wananchi wanatakiwa kuwasiliana na ofisi ya diwani huyo ambayo itajiridhisha na makazi na uhalali wa biashara inayofanywa na mwananchi husika kabla hajatimiziwa haja za moyo wake.
Katala Mganga, mkulima wa mpunga aliyepata mkopo huo alisema anatarajia kwenda kuongeza ukubwa wa mashamba kwani gharama za kulima zitakuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa na atapata fursa ya kuwasaidia wakulima wengine.
Kwa miaka minne aliyojikita kwenye kilimo hicho, Mganga alisema alianza na eka 10 ammbazo aliziongeza mpaka eka 60 kabla hajapata trekta hilo ambalo anaamini litasaidia kuongeza ukubwa wa shamba lake.
"Ukiwa na trekta gharama za kulima eka moja ni Sh15,000 ilhali ukikodi utatakiwa kulipa zaidi ya Sh50,000. Naishukuru ofisi ya diwani imenisaidia trekta hili," alisema.
Mkurugenzi wa kampuni ya Hitech International Tanzania, Paul Mashauri alisema kampuni hiyo ina mpango wa kutengeneza ajira milioni tatu mapaka mwaka 2020 jambo litakalofanikiwa kwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini na kati kujiajiri na kuajiri wengine.
"Endapo kila familia itakuwa inaongeza thamani ya bidhaa moja au mbili ama kutengeneza chochote na kukiuza kwa jamii inayoizunguka hili litawezekana. Tunazo mashine za aina tofauti ambazo zinawafaa watu wenye ndoto ya kumiliki kiwanda," alisema.
Alisema licha ya Kawe, mikopo ya namna hiyo inatolewa Dodoma, Mbeya na Arusha ambako tayari mafunzo yamefanyika. "Kadri siku zinavyoenda tutawafikia wananchi wengi zaidi," alisema Mashauri.
Kw amujibu wa Mashauri, trekta hilo limegharimu kiasi cha Dola 29,000 za Marekani (zaidi ya Sh58 milioni).
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa