Licha ya Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) kueleza kusikitishwa kwao na
uchaguzi wa marudio Zanzibar kufanyika bila kuwapo maelewano ya pande
zinazokinzana, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kususia kushiriki,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema iko tayari kufa njaa
kuliko kukubali kuingiliwa uhuru wake.
Juzi, Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alimtangaza Dk. Ali
Mohamed Shein, mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyuika Jumapili
iliyopita, kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4, hatua iliyozifanya
balozi mbalimbali nchini kueleza maskitiko yao na kusisitiza kuwa ni
lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati
matakwa ya watu.
Tamko la mabalozi hao lilitolewa na wawakilishi
wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa,
Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden,
Switzerland, Uingereza na Marekani.
Wakati kauli ya mabalozi hao
ikizua hofu kuwa huenda Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ikakatiwa
misaada na mikopo kutoka nje, kwa madai ya kupindishwa kwa demokrasia,
SMZ imetoa msimamo kwamba haitazipigia magoti nchi wahisani na kwamba
imeanza kujipanga kujitegemea kwa mapato ya ndani katika bajeti yake.
Msimamo huo wa SMZ, ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, na
Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omary Yusuph Mzee, walipozungumza kuhusu
msimamo wa EU, Marekani na washirika wao kusikitishwa na kurudiwa
uchaguzi kabla ya kupatikana muafaka wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka
jana.
Aboud alisema uchaguzi wa marudio umefanyika Zanzibar ikiwa
utekelezaji wa masharti ya katiba na sheria na haikuwa muafaka kwa
wahisani kuhoji kufanyika kwake.
“Kitendo wanachokifanya
washirika wetu wa maendeleo hakikubaliki katika misingi ya utawala wa
sheria. Wanaingilia mambo ya ndani wakati Zanzibar ni nchi huru,”alisema
Aboud.
Alisema uchaguzi wa Zanzibar unaendeshwa kwa kufuata
masharti ya katiba na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984 na si
maridhiano ya vyama, kama wanavyotaka wahisani.
Aboud alisema
Zanzibar iko tayari kushirikiana na washirika wa maendeleo, lakini
lazima misaada izingatie utu na heshima ya nchi kwa manufaa ya Zanzibar
na wananchi wake.
“Zanzibar ni nchi huru na itaendelea kuwa huru.
Tuko tayari kupokea misaada inayozingatia utu na heshima kwa Zanzibar
na wananchi wake kinyume cha hivyo tuko tayari kufa njaa,” alisisitiza.
Naye Mzee kwa upande wake, alisema jana ofisini kwake, Vuga, visiwani
hapa kuwa hategemei hilo kutokea katika kipindi cha miaka mitano kuanzia
sasa.
Alisema lengo la serikali kwa sasa ni kuhakikisha
inaondokana na utegemezi wa wafadhili na kwamba imeanza kuweka mikakati
maalum, kuhakikisha inajitosheleza kwenye bajeti yake.
Alisema
miongoni mwa mikakati inayotarajiwa kufanywa kutimiza lengo hilo ni
kuanza kuiga mfumo anaoutumia Rais John Magufuli wa kufuta safari
zisizokuwa za lazima kwa viongozi wa serikali.
Aliongeza kuwa
mikakati mingine ni kuhakikisha wagonjwa wanaotakiwa kwenda kutibiwa nje
ya nchi, wanapata huduma hiyo nchini kwa kuandaa mipango maalum ya
kuleta madaktari.
Mzee ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema Zanzibar inatarajia kutumia
mapato yake ya ndani kujitosheleza kwenye bajeti yake.
Alisema
Rais Dk. Shein juzi alitoa msimamo wa serikali wa kutaka iwekwe mikakati
itakayowezesha Zanzibar kujiendesha kwa bajeti yake bila wafadhili.
Mzee alisema Zanzibar inategemea asilimia 20 ya misaada kwa ajili ya
kukamilisha bajeti yake kila mwaka pamoja na mikopo kutoka taasisi za
fedha, zikiwamo benki za nje.
Alisema bajeti ya Zanzibar
inategemea asilimia 26 hadi28 ya mapato yanayotokana na sekta ya utalii
wa ndani na nje na kwamba bado kunahitajika mikakati ili kupanua wigo wa
kupata fedha.
Kwa mujibu wa Mzee, Zanzibar inapokea watalii
kati ya 300,000 na 400,000 kwa mwaka na kwamba wanatarajia kuongezeka
baada ya kufungua ofisi
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa