Shule ya Sekondari Lilasia yafanya mahafali ya 6.
*Wataka kuwe na lugha maalum mashuleni
NA ANDREW CHALE
NJIA nyepesi ya kukabiliana na tatizo kubwa la ajira kwa vijana nchini ni kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye viwanda, sanjari na kuutazama upya mtaala wa kufundishia kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu, hususan kwenye eneo la lugha, imeelezwa
Akizungumza kwenye mahafali ya 6, ya Shule ya Sekondari Lilasia, iliyopo Kitunda, Dar es Salaam jana septemba 20, Mkurugenzi wa shule hiyo, Christina Lyimo, alisema kupitia viwanda vijana kwa maelfu yao wataajirika na kujiajiri kwa mtiririko wa fursa zitakazokuwepo, huku pato la taifa likizidi kukua.
"Sina shaka sana na rasilimali tulizonazo..zinatosheleza, tuna uchumi mkubwa, hebu kama serikali itanisikia niombe sasa tuwekeze nguvu kwenye viwanda, tupeleke surveyors wakapime maeneo, sababu tuna nguvu kazi kubwa, tuna rasilimali..tuanzie hapo," alisema Lyimo.
Aidha, Lyimo, ambaye kitaaluma ni mwalimu anayehudumu kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 25 sasa, ameshauri yafanyike mabadiliko ya mtaala hususan kwenye lugha ya kufundishia, huku akisisitiza ni wakati mwafaka sasa kwa taifa kuamua ni lugha ipi itumike kufundishia kama ni Kiingereza au Kiswahili, tofauti na ilivyo sasa kuchanganya changanya.
"Watoto wengi wanababaika kwenye mitihani kwa sababu ya Lugha..watoto wengine wanafeli kwa kushindwa kujieleza kwa lugha za kigeni!..shule ya msingi Kiswahili miaka saba..sekondari kiingereza kwa kweli inachanganya, tuamue basi kubadilisha kama ni medium basi ziwe kuanzia awali hadi vyuo vikuu, na kadhalika kama Kiswahili iwe hivyo," alisema
Hata hivyo, katika hatua nyingine, aliwaomba wafadhili kujitokeza kuchangia shule hiyo kwenye eneo la upatikanaji wa maabara ya kisasa, ikizingatiwa shule kwa sasa pamoja na mambo mengine inasomesha watoto yatima bure na kusaidia kwa kiasi utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitunda na kwingineko nchini
"Tunaomba pia serikali igeuzie macho kwenye shule hii, tuna watoto yatima hapa, itusukume kwenye kupata ruzuku sababu tunasaidia taifa na hata ada tunazopokea ni ndogo mno," alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Lilasia, Silas Kamando alisema katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 36 wakiwemo wanaume 17 na wasichana 19 wamehitimu kidato cha nne mwaka huu, na kwa sasa wanajiandaa na mtihani wao wa taifa unaotarajia kufanyika Novemba 3 mwaka huu, nchini kote
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa