LEO ni Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambapo wafanyakazi nchini wanaungana na wenzao duniani
kuadhimisha siku hiyo. Wafanyakazi wakiwa wanaadhimisha kwa maandamano
kama ilivyo desturi yao, lakini wataadhimisha siku hii huku wakiwa na kilio kwa serikali zao kutaka kuboreshewa maslahi yao, na pia kuwekewa mazingira bora na salama ya kazi. Nchini, kitaifa maadhimimisho hayo yanafanyika Mbeya kama itakavyokuwa pia katika mikoa na wilaya zingine kote nchini.
Hii ni siku muhimu kwa wafanyakazi hasa kutokana na kuitumia kupaza sauti zao kwa Serikali kuhusu masuala ambayo yanaonekana kuwa kero kwa wafanyakazi.
Kwa miaka mingi sasa nchini wafanyakazi wa umma na hata wa sekta binafsi wamekuwa wakilalamikia kiwango kidogo cha mshahara wanacholipwa ambacho hakiendani na hali ngumu ya maisha inayowakabili sasa.
Kwa maana rahisi ni kuwa mishahara wanayolipwa wafanyakazi wengi nchini haiwezi kumudu gharama za maisha kwa mwezi, hivyo wengi wanaishia kuishi maisha ya dhiki na ya kubahatisha. Tatizo hili hasa limekuwa likiwaathiri zaidi wafanyakazi wa ngazi za chini ambao ndio wengi hivyo kuwapotezea ari ya kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya nchi yetu.
Mbali na mishahara, madai mengine ambayo wafanyakazi nchini wamekuwa wakilalamikia kila mwaka na kwa muda mrefu ni kodi kubwa inayotozwa kwenye mishahara hasa kutokana na serikali kuona ndio sehemu rahisi ya kukusanyia kodi hiyo.
Ikiwa leo tunaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani ni vyema Serikali ikajibu kero zinazosumbua wafanyakazi ili waweze kufanya kazi kwa ari na kutambua kuwa serikali yao inatambua mchango wao.
Natambua kuwa Serikali haiwezi kuwa na uwezo mkubwa wa kumaliza tatizo la viwango vidogo vya mshahara mara moja, lakini kwa kiasi fulani inaweza kupunguza matatizo haya hata kwa zaidi ya nusu hivyo kuleta matumaini mapya kwa wafanyakazi.
Kuna haja ya kuangalia kero hizi hasa ikizingatiwa kuwa miaka ya hivi karibuni mfumuko wa bei nchini umekuwa
ukipanda kwa kasi, jambo ambalo linafanya bei ya bidhaa kupanda na kufanya maisha ya mfanyakazi kuzidi kuwa magumu.
Mfanyakazi huyo wa Tanzania mbali na kodi anayokatwa kwenye mshahara, lakini pia amekuwa akilipia kodi zingine kwenye bidhaa na huduma anazopata kutoka kwa wafanyabiashara, hivyo kuwafanya kila wanachopata kuishia mikononi mwa wafanyabiashara na wao maisha yao kuendelea kuwa ya kubahatisha kwani mshahara umekuwa ukiisha hata kabla ya kupokea.
Hivyo basi tunaona ni wakati mwafaka kwa matatizo ya wafanyakazi yafanyiwe kazi, ikiwa ni pamoja na Serikali kutafuta maeneo mengine ya kukusanya kodi badala ya kutegemea mishahara midogo ya watu wa kipato cha chini.
Naamini kuwa endapo kilio cha wafanyakazi kitasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi, hata migongano ya hapa na pale kati ya vyama vya wafanyakazi na Serikali itakuwa historia kwa manufaa ya kusukuma mbele maendeleo ya nchi.
chanzo: habari leo
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa