
Siku moja baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Jeshi la Polisi lilianza kampeni kubwa ya kujaribu kuficha ukweli juu ya kuhusika kwake, kwa kuhamishia lawama kwa watu wengine wasiohusika na mauaji hayo. Kwa mfano, Kamanda Kamuhanda alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba marehemu Mwangosi alifariki “kutokana na kitu kizito kilichotupwa na waandamanaji.” Aidha, siku iliyofuata Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja alidai kwamba baada ya ghasia kudhibitiwa, marehemu Mwangosi alikimbilia walipokuwa polisi na “kitu kama bomu kikarushwa na kundi la watu wanaokimbia hovyo na kumlipua Mwangosi.”
Njama hizi za kuficha ukweli zimeumbuliwa na Ripoti ya MCT/TEF inayobainisha kwamba marehemu Mwangosi “aliuawa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda.” Ripoti hiyo pia imeelezea kwa kirefu jinsi Jeshi la Polisi lilivyotoa taarifa zinazokinzana juu ya kuhusika kwake na mauaji ya Mwangosi. Hivyo, kwa mfano, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi alidai tarehe 4 Septemba 2012 kwamba marehemu aliuawa na bomu la machozi ambalo ‘halikulipuliwa kitaalamu na polisi’, Kamanda Kamuhanda alitokea kwenye televisheni siku iliyofuata “akitangaza habari za kuwatupia lawama wafuasi wa CHADEMA kwa kutupa kitu kizito kilicholipuka na kumuua Mwangosi....”
Mheshimiwa Spika,
Hata Taarifa ya Uchunguzi wa Kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Bw. Daudi Mwangosi, iliyoandaliwa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Nchimbi na kuongozwa na Jaji Stephen Ihema imethibitisha kuhusika kwa Jeshi la Polisi na mauaji ya Marehemu Mwangosi. Baada ya kuzunguka huku na huko ikijaribu kulisafisha Jeshi la Polisi kutoka kwenye lawama ya kumuua Marehemu Mwangosi, Taarifa ya Kamati hiyo inasema: “Hapakuwepo na uhalali wa kutumia Bomu la Kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia.” Aidha, Kamati hiyo inakiri kwamba “hapakuwepo umuhimu wa kutumia Bomu la Kishindo kwa sababu hata ingekuwa ukamataji tayari askari polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.” Kwa misingi hiyo, “… Kamati imeona kwamba … tukio la kuuawa Bw. Daudi Mwangosi na kuumizwa baadhi ya askari polisi halikustahili kabisa.”
Mheshimiwa Spika,
Kuna uthibitisho mkubwa kwamba Serikali hii ya CCM na Jeshi la Polisi wamekuwa wanawalenga kuwaua au kuwaumiza waandishi wa habari wanaoandika zisizowapendeza viongozi wa Serikali au Jeshi la Polisi. Kwa mfano, Ripoti ya MCT/TEF inaashiria kuwa sababu ya Marehemu Mwangosi kuuawa ni kwamba yeye “... ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC (Kamuhanda) ‘maswali magumu’ kiasi cha kumkera kiongozi huyo wa jeshi la polisi.” Ripoti hiyo inafafanua kwamba “baada ya mkutano huo na waandishi, ... baadhi ya polisi ... waliwaonya wasiende Nyololo kwa ajili ya kukusanya habari za shughuli za kisiasa za CHADEMA kutokana na uwezekano wa kutokea kwa hali hatarishi.” Aidha, “baada ya mkutano wa waandishi wa habari wa asubuhi katika ofisi za RPC (Kamuhanda), ... askari mmoja mpelelezi alimfuata Mwangosi na kumwambia: ‘Ina maana gani kwenda Nyololo kuandika habari za Chadema ambazo zinaweza kuishia na kifo chako?’” Vile vile, Ripoti ya MCT/TEF inabainisha, ni “... wazi kwamba Polisi walikuwa wanawawinda waandishi wa Iringa ambao walikuwa wakiwajua.”
Mheshimiwa Spika,
Siku tatu baada ya mauaji ya Daudi Mwangosi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai katika Jeshi la Polisi Robert Manumba alitoa kauli kwa vyombo vya habari kuhusu matukio ya kuuawa kwa waandishi wa habari ambapo alisema “….matukio ya aina hii yapo na yataendelea kuwepo.” Katika kuthibitisha kwamba Serikali hii ya CCM ina sera isiyo rasmi ya kulenga kuwadhuru waandishi wa habari wanaowaandika watawala vibaya na hata kuwaua, kauli ya DCI Manumba imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulongo wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka huu jijini Arusha. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Mkuu huyo wa Mkoa aliwatahadharisha waandishi kwa kuwaambia kwamba “unapoingia katika mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa Serikali unaiweka roho yako rehani…. Kuweni makini.”
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake kwenye mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliyaita matamshi ya DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo kuwa ni ‘matendo ya kigaidi’ kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi, 2002, ambayo inafafanua ‘matendo ya kigaidi’ kuwa ni pamoja na vitisho vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au majeraha makubwa kimwili, kuhatarisha maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa umma ambavyo vimelengwa au ambavyo kwa hulka au muktadha wake vinaonekana vimelengwa kutishia umma au sehemu ya umma.
Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama tafsiri hiyo ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ni sahihi au la. Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini DCI Manumba na Mkuu wa Mkoa Mulongo bado hawajakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi hadi sasa? Kama tafsiri hiyo sio sahihi, basi Serikali hii ya CCM itamke mbele ya Bunge lako tukufu kwamba ni sera yake rasmi kwamba waandishi wa habari wanaoiandika Serikali au viongozi wake vibaya ‘wanaweka roho zao rehani’!
Mheshimiwa Spika,
Kauli ambazo zimetolewa na Serikali hii ya CCM ndani ya Bunge lako tukufu zinathibitisha kuhusika kwa Serikali katika, kama sio kupanga basi angalau kubariki, mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama vya Serikali kwa waandishi. Na moja ya kauli za Serikali ambazo zimeifadhaisha na kuisikitisha sana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni ile iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, Mh. William Lukuvi pale alipomsifu Kamanda Kamuhanda wakati wa mjadala wa Wizara ya Mambo ya Ndani: “Katika kitabu hiki cha Kambi ya Upinzani, wamekutaja sana (Kamuhanda), hawawezi kukupongeza. Huko Iringa Kamanda unafanya kazi nzuri sana, usitetereke na makamanda wako wa huko Iringa.”
Ikumbukwe, Mheshimiwa Spika, kwamba mtu anayesifiwa kwa ‘kufanya kazi nzuri sana kule Iringa’ ni yule yule ambaye aliyelaumiwa na Tume ya Haki za Binadamu – ambayo Makamishna wake wote ni wateule wa Rais kwa mujibu wa Katiba – kuwa alikiuka sheria za nchi yetu na misingi ya utawala bora kufuatia tukio la mauaji ya Marehemu Mwangosi! Mtu anayeshauriwa na Waziri Lukuvi kwamba ‘asitetereke’ ni yule yule ambaye MCT/TEF imemhusisha na usimamizi wa moja kwa moja wa mauaji ya Mwangosi. Needless to say, mtu huyu bado yuko huru na hajachukuliwa hatua yoyote licha ya mshangao mkubwa kitaifa na kimataifa!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kauli ya Mheshimiwa Lukuvi kuhusu kuhusika kwa Kamanda Kamuhanda na Jeshi la Polisi katika mauaji ya Marehemu Mwangosi ndio msimamo rasmi wa Serikali hii ya CCM. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kuliambia Bunge lako tukufu ni nini msimamo wake rasmi juu ya Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Ripoti ya MCT/TEF kuhusu kuhusika kwa Jeshi la Polisi na Kamanda Kamuhanda katika mauaji ya Marehemu Mwangosi. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kimya cha Serikali hii ya CCM juu ya maswali haya muhimu ni ushahidi dhahiri kuwa mauaji haya ni sehemu ya mkakati ulioasisiwa na Serikali hii ya CCM wa kuwanyamazisha waandishi wa habari kwa nia moja tu: kufifisha uhuru wa kupata na kutoa habari muhimu zinazohusika kashfa za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka serikalini.
Mheshimiwa Spika,
Miezi sita baada ya Jeshi la Polisi kumuua Daudi Mwangosi, mwandishi mwingine mwandamizi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya nje ya nyumba yake baada ya nyendo zake kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa kuwa watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS). Badala ya kuchukua hatua za dhati kuwachunguza na kuwakamata wale wote waliohusika na tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, maafisa waandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu na viongozi waandamizi wa CCM chini ya Naibu Katibu Mkuu wake Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na baadhi ya waandishi habari maslahi, walianzisha kampeni kubwa ya kuipakazia CHADEMA na Mkurugenzi wake wa Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi kutokana na ushahidi wa kutunga!
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile njama dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuyatupilia mbali mashtaka ya ugaidi dhidi yake, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kutoa taarifa rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya waliohusika na jaribio la kumuua Bw. Kibanda. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya kuhusika kwa Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Ikulu na CCM katika kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya CHADEMA na Bw. Lwakatare ili kuwapumbaza Watanzania wasihoji shambulio la kigaidi dhidi ya Bw. Kibanda.
Kutoa taarifa ya uongo kwa lengo la kuanzisha mashtaka ya jinai mahakamani au kutengeneza ushahidi wa uongo kwa lengo la kuipotosha mahakama ni makosa ya jinai yenye adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa mujibu wa Sheria ya Adhabu ya Tanzania. Ni muhimu kwa ukweli wa jambo hili kujulikana sio tu kwa ajili ya kuwawajibisha kijinai wahusika, bali pia kwa lengo la kulinda demokrasia na utawala wa sheria katika nchi yetu. Kama alivyosema Chris Conybeare, Katibu Mkuu wa Chama cha Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC) katika ujumbe wake kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara juu ya mauaji ya Marehemu Mwangosi: “Waandishi wa habari wanapouawa demokrasia pia inakufa.”
3. MAELEZO NA UHURU WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
Idara ya Habari (MAELEZO) ilikasimiwa majukumu na mali za lililokuwa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) na Sheria ya Kufuta Shirika la Habari la Tanzania, Na. 7 ya mwaka 2000. Wakati SHIHATA ilikuwa na ukiritimba wa kukusanya habari pamoja na mamlaka ya kusajili waandishi wa habari, ukiritimba huo na mamlaka ya usajili wa waandishi wa habari yalifutwa kabisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Mfumo wa Chama Kimoja au Vyama Vingi vya Siasa Tanzania, 1991 (‘Tume ya Nyalali’), iliyobaini kwamba Sheria ya SHIHATA ilikuwa inakiuka misingi ya uhuru wa mawazo na uhuru wa habari.
Kwa sababu hiyo, majukumu mapya ya Idara ya Habari, kama yalivyofafanuliwa katika kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Kufuta SHIHATA, ni pamoja na kutoa, kuendeleza na kuhamasisha uanzishwaji na uendeshaji wa za kukusanyia na kusambaza habari; kukusanya na kusambaza habari na kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu usambazaji habari na utendaji wa mashirika ya habari. Idara ina ofisi katika baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Spika,
Tofauti na SHIHATA, Idara ya Habari haina na haijawahi kupewa jukumu la kisheria la kuwa msimamizi wa vyombo vya habari na wanahabari nchini. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa SHIHATA, Idara hii imekuwa inawauzia waandishi wa habari vitambulisho (press cards) ambavyo vimekuwa vinatumika kama vitambulisho cha kazi kwa waandishi wa habari hapa nchini. Vitambulisho hivyo vimekuwa vinauzwa kwa shilingi za Tanzania elfu ishirini, lakini Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba bei ya vitambulisho hivyo imepanda mwaka huu hadi kufikia shilingi elfu thelathini. Aidha, vitambulisho hivyo hutolewa kila mwaka katika Ofisi za MAELEZO Dar es Salaam na hivyo kusababisha gharama na usumbufu mkubwa kwa waandishi wa habari walioko mikoani.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi vya Idara ya Habari ni kinyume cha Sheria ya Kufuta SHIHATA. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu Idara ya Habari imetoa wapi mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya uandishi habari. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna masharti yoyote ya kisheria yanayolazimu waandishi wa habari wasajiliwe na MAELEZO kwa kupatiwa vitambulisho vya kazi na Idara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Idara ya Habari imejitwalia mamlaka ya kusajili waandishi wa habari kwa kuwalazimisha kununua vitambulisho vya taaluma yao, lakini pia imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa kupanuka kwa demokrasia na uhuru wa habari katika nchi yetu. Historia yake inaanzia miaka ya mwanzo ya utawala wa kikoloni wa Kiingereza wakati walipotunga Sheria ya Magazeti ya 1928. Chini ya Sheria hiyo, wakoloni walidhibiti ukuaji wa vyombo vya habari vya wenyeji wa Kiafrika kwa kuviwekea masharti ya kusajiliwa baada ya kutoa dhamana ya fedha taslimu.
Marekebisho ya Sheria hiyo yaliyofanywa mwaka 1952 yaliweka masharti magumu zaidi ya usajili wa magazeti pamoja na kuongeza kiwango cha dhamana kutoka pauni za Kiingereza 160 hadi pauni 520. Kwa mujibu wa Martin Sturmer katika kitabu chake The Media History of Tanzania, wakati magazeti ya Wamisionari na yale yaliyokuwa yanaunga mkono sera za utawala wa kikoloni katika Tanganyika hayakudaiwa kulipa dhamana, magazeti yaliyokuwa na mrengo wa upinzani wa sera za dola ya kikoloni yalilazimika kulipa dhamana hiyo.
Baadae mwaka 1955 dola ya kikoloni iliongeza udhibiti zaidi wa vyombo vya habari kwa kuingiza katika Sheria ya Adhabu vifungu vipya vilivyokataza uchapishaji wa jambo au taarifa yoyote lenye uwezo wa kuleta chuki dhidi ya serikali ya kikoloni au watendaji wake. Kama anavyosema Sturmer, kutokea hapo sheria hiyo ya uchochezi ndio imekuwa kizingiti kikubwa kwa uhuru wa magazeti katika Tanzania. Haiwezi kuwa ajabu kwamba wahanga wa kwanza wa sheria hiyo ya uchochezi walikuwa mabwana Kheri Rashidi Baghdelleh na Robert Moses Makange waliokuwa wahariri wa gazeti laMwafrika; na mhariri wa gazeti la Sauti ya TANU aliyejulikana kama Julius Kambarage Nyerere!
Mheshimiwa Spika,
Kitu cha ajabu ni kwamba sheria iliyotungwa na wakoloni wa Kiingereza kwa lengo la kuwadhibiti wenyeji wa Kiafrika wasidai uhuru au kuanika uchafu na uonevu wa dola ya kikoloni haikufutwa mara baada ya uhuru. Badala yake, sera za habari za dola ya uhuru sio tu zilipokea na kuzidisha masharti ya kisheria dhidi ya uhuru wa habari kwa kutunga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyoongeza makali ya sheria ya uchochezi, bali pia zilitaifisha magazeti na vyombo vingine vya habari binafsi vilivyokuwepo wakati wa uhuru.
Hivyo, kwa mfano, Shirika la Utangazaji la Tanganyika (TBC) lilitaifishwa kwa Sheria ya Bunge ya tarehe 16 Machi 1965 na kubatizwa jina jipya la Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Aidha, tarehe 5 Februari, 1970, gazeti binafsi la The Standard lilitaifishwa na Serikali. Na ilipofika tarehe 26 Aprili, 1972, The Daily News, gazeti jipya la Serikali lilianzishwa kwa kuunganisha The Standard na gazeti la The Nationalist lililokuwa linamilikiwa na TANU. Hivyo basi, kama anavyosema Sturmer katika historia yake ya vyombo vya habari Tanzania, “kufikia mwaka 1976 Serikali ya Nyerere ilishafanikisha lengo lake kuu la sera ya habari – kuwa na udhibiti juu ya vyombo vyote vikuu vya habari....”
Mheshimiwa Spika,
Utaratibu huu wa udhibiti juu ya vyombo vya habari kwa kutumia Sheria ya Magazeti ulishambuliwa na Tume ya Nyalali kwa kukiuka matakwa ya ibara ya 18 ya Katiba inayotoa uhuru wa mawazo na uhuru wa habari. Kwa maneno ya Tume hiyo, Serikali inakiuka uhuru wa mawazo na wa habari “... kwa kujihusisha na kuchuja habari zinazotolewa kwa wananchi.” Tume ilipendekeza marekebisho makubwa katika Sheria ya Magazeti “... ili kuruhusu uhuru mkubwa zaidi wa habari na wa mawazo na kulegeza uchujaji wa habari.” Mapendekezo haya ya Tume ya Nyalali hayajatekelezwa hadi leo hii, zaidi ya miaka ishirini na mbili tangu Tume hiyo iwasilishe Taarifa yake kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati Tanzania imebakia mateka wa sera za habari za kikoloni na za utawala wa kiimla wa chama kimoja, jirani zetu wa Kenya na marafiki zetu wa Zimbabwe wamepiga hatua kubwa katika kupanua uhuru wa habari. Hivyo, kwa mfano, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Zimbabwe iliyopitishwa kwa kura ya maoni ya wananchi wa nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu inatoa uhuru wa mawazo ambao unajumuisha uhuru wa kutafuta, kupokea na kusambaza mawazo na habari nyingine; uhuru wa mawazo ya kisanii na wa utafiti wa kisayansi na uhuru wa taaluma.
Aidha, Katiba hiyo inatoa uhuru wa habari ambao ni pamoja na ulinzi wa vyanzo vya habari vya waandishi wa habari; na uhuru wa uanzishaji wa vyombo vya utangazaji ambavyo havitakiwi kuwa chini ya udhibiti wa serikali au maslahi ya kisiasa au kibishara. Vile vile, Katiba Mpya ya Zimbabwe inavilazimu vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali kuwa huru kuamua mambo gani ya kutangaza; kutokupendelea na kutoa fursa sawa kwa ajili ya kutangaza maoni tofauti na mawazo yanayokinzana.
Mheshimiwa Spika,
Katiba Mpya ya Zimbabwe inatoa pia uhuru wa taarifa (access to information). Hivyo, kwa mfano, kila raia au mkazi wa kudumu wa Zimbabwe, ikiwa ni pamoja na makampuni na vyombo vya habari, ana haki ya kupatiwa taarifa yoyote inayodhikiliwa na Serikali au na taasisi au shirika lolote la serikali katika ngazi zote, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya maslahi ya uwajibikaji kwa umma. Zaidi ya hayo, kila mtu, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Zimbabwe, ana haki ya kupatiwa taarifa inayoshikiliwa na mtu yeyote, pamoja na Serikali, kama taarifa hiyo inahitajika kwa ajili ya kufurahia au kulinda haki yake. Kama ilivyo kwa Zimbabwe, Katiba Mpya ya Kenya nayo pia imetoa uhuru mpana wa habari kwa wananchi wa Kenya.
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni fedheha kwamba nchi yetu iliyokuwa ya kwanza kupata uhuru katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini inaelekea kuwa ya mwisho katika masuala ya uhuru wa habari kwa watu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM kulieleza Bunge lako tukufu ni lini italeta muswada wa sheria kwa lengo la kufuta urithi huu wa fedheha wa sheria za kikoloni ili Tanzania iendane na karne mpya ya uhuru wa habari na wa mawasiliano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sasa vyombo vya habari vya Serikali yaani, Radio na Television za Taifa ndio vinatoa matangazo kwa wananchi kuhusu kile kinachoendelea Bungeni. Kwa bahati mbaya ni kwamba Radio ya Taifa ambayo inasikilizwa na watanzania wengi wa hali ya chini na kati katika maeneo mengi ya mijini na vijijini wanashindwa kusikiliza mijadala inayoendelea Bungeni, kwani matangazo yanakatishwa pindi kipindi cha maswali na majibu kinapomalizika. Matangazo ya mjadala wa Bunge yanaendelea kurushwa kwenye Television ya Taifa hadi Bunge linapoahirisha shughuli zake kwa siku.
Mheshimiwa Spika,
Huku ni kutowatendea haki watanzania wengi kwa kuwapa fursa kusikiliza nini wawakilishi wao wanachokiongea katika mijadala mbalimbali Bungeni. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona sasa ni muda mwafaka kwa sekta binafsi nazo kufanyakazi hiyo ambayo inaonyesha imevielemea vyombo hivyo vya serikali na kuondoa ukiritimba uliopo wa kurusha matangazo ya Bunge.
3.2 Matangazo ya serikali kwenye vyombo vya habari
Mheshimiwa Spika,
Suala la matangazo ya serikali katika vyombo vya habari si kwamba limekuwa likitumika kuminya uhuru wa habari katika baadhi ya vyombo vya habari hususan vinavyoonekana kuwa vinafanya utafiti katika habari zake kwa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na hivyo kuweka hadharani mapungufu na uchafu wa Viongozi waliopewa dhamana na wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Suala hilo la matangazo badala ya kuviimarisha vyombo vya habari ili viweze kusimama na kufanyakazi bila ya kuingiliwa, sasa linatumika kama njia ya kufifisha uhuru wa kutafuta na kutoa habari na kuvifanya vyombo vya habari kuachana na uhandishi wa uchunguzi na hivyo kukiuka haki za walaji za kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya katiba ya 18 (d).
Mheshimiwa Spika,
1 comment :
Write more, thats all I have to say. Literally, it seems as though you relied on
the video to make your point. You clearly know what youre talking
about, why waste your intelligence on just posting
videos to your weblog when you could be giving us something
enlightening to read?
Feel free to visit my web page :: revitol review
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa