Ifuatayo ni taarifa ya mratibu wa uanzishwaji wa benki hiyo katika wilaya ya Mafia, Nd Salum Maulidi
 |
Salum Maulid - Mratibu wa uanzishwaji wa
benki ya wananchi Mafia |
TAARIFA YA UTEKELEZAJI YA UANZISHWAJI WA BENKI
YA WANANCHI MAFIA.
UTANGULIZI:
Mradi wa MACEMP Uliikasimu SCCULT (1992)LTD Kufanya Utafiti na Kubaini Chanzo na Kiini kwa nini Miradi na Biashara ndogo ndogo na kati za wananchi katika wilaya ya Mafia kutokua ipasavyo na Mpaka Sasa Hali ya Utekelezaji ni Kama Ifuatavyo:-
HALI YA UTEKELEZAJI:
1. Mnamo Mwaka 2008 Mwishoni SCCULT kwa Kushirikiana Na Halmashauri Ya Wilaya Ya Mafia tulifanya Utafiti na Kubaini Kiini kwa Nini Miradi Na Biashara ndogo ndogo na Za Kati Za Wananchi katika Wilaya Ya Mafia Kutokuwa Ipasavyo.
Utafiti Uibaini Yafuatayo:-
• Mtiririko wa vipato si wa uhakika(Irregularity in income flows).
• Kiwango cha juu cha kutokujua kusoma na kuandika(High level of illiteracy).
• Kutegemea shughuli za uvuvi zaidi katika kuendesha maisha.
• Kushiriki Kidogo katika kilimo.
• Upungufu wa mali(Low asset base).
• Elimu ndogo ya Fedha(Low level of financial literacy).
Hali hiyo imepelekea kubaini kuwa Mafia kuna huduma chache za kifedha kwani inakadiriwa ni asilimia mbili tu(2%) ya wananchi wanapata huduma za kifedha.
Washauri Elekezi(SCCULT) walitoa ushauri wa kuunganisha nguvu za pamoja kati ya wananchi,SACCOS,VICOBA,AMCOS, Vyama vya uvuvi,Makampuni,Wafanyabiashara wakubwa na wadogo na Halmashauri ya wilaya ya Mafia kwa ujumla kuanzisha Benki Ya Wananchi Wa Mafia jambo ambalo MACEMP wameliafiki.
Mradi wa Macemp umekubali kutoa jengo na miundombinu ya kibenki ikiwa ni pamoja na samani,mitambo ya ulinzi,vitendea kazi,kama kompyuta,software pamoja na kulipa mishahara ya watumishi kwa miezi sita ya mwanzo.
2. Katika robo ya mwisho ya mwaka 2009,Halmashauri tukishirikiana na washauri elekezi tulifanya mikutano na wananchi,vyama vya ushirika kama vile SACCOS,VICOBA na Vyama Vya Uvuvi na walihamasika na kuonyesha nia ya kushiriki katika kuchangia Mtaji ili kuanzisha Benki Ya Wananchi Mafia kulingana na Masharti na sheria za mabenki na Taasisi za kifedha(Banking and Financial Institutions Act of 2006) kulingana na sheria hii mtaji wa kuanzisha Benki ya Wananchi kwa sasa ni Tshs 250,000,000/= Mtaji ambao wananchi wa mafia ni jukumu letu.
3. Kikao cha Wadau Kilichoongozwa na na Mkuu Wa Wilaya wa Mafia Mhe.MANZIE O.MANGOCHIE kilifanyika kikihudhuriwa pia na mbunge wa Jimbo Mhe.ABDULKARIM E.SHAH,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mafia William Shimwela,Madiwani na wakuu wa idara kujadili na kupanga Mikakati ya uanzishwaji wa Benki ya Wananchi wa Mafia.
4. Kamati ya Uanzishwaji Wa Benki ya wananchi imeundwa chini ya maelekezo ya SCCULT ambaye ni mshauri Elekezi (CONSULTANTS).
5. Kamati imeandaa “Memorandum and Articles of Association” na kupitishwa BRELA na kupata usajili Na.76724 yenye jina MAFIA COMMUNITY BANK LTD (MCB).
6. Kamati Imefungua Akaunti Benki ya NMB Mafia Akaunti Na 2156600051. Akaunti hii ni kwa ajili ya kuhifadhia hisa zinazouzwa kwa wananchi.
7. Kikao cha Wananchi Wa Mafia waishio Dar es salaam kimefanyika mwezi novemba 2010 Ukumbi wa Landmark Hotel na Hisa Zipatazo 50,000/=ziliahidiwa kununuliwa.
8. Uzinduzi wa Ununuzi Wa Hisa Umefanyika tarehe 02/12/2010 na mpaka sasa hisa zipatazo 67,880 sawa na Tshs 33,940,000/=zimenunuliwa.Hisa moja ina thamani ya Tshs 500/= uuzwaji wa hisa unaendelea Mtu/Taasisi/Kampuni/Kikundi inaruhusiwa kununua Hisa 40 zenye Thamani Ya Tshs 20,000/= hadi 50,000,000/=.
9. Kikao baina ya kamati ya uanzishwaji wa benki ya wananchi,uongozi wa wilaya na meneja wa Macemp na timu yake kimefanyika tarehe 19/07/2011 katika ofisi ya mkuu wa wilaya kimefanyika kujadili kuzorota kwa ukamilishwaji wa uanzishwaji wa benki ya wananchi mafia.
10. Kikao cha Mkakati wa uanzishwaji wa Benki wananchi Mafia na Kilwa kimefanyika Dar es salaam Ukumbi wa Baraza la Maaskofu Chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi wa Uvuvi Kikihudhudhuriwa na uongozi wa MACEMP Taifa,SCCULT Na wawakilishi wa wilaya mbili kupanga mikakati mbalimbali ya ukamilishwaji wa Benki hizi mbili.
11. Jengo kwa Ajili ya shughuli za Benki ya Wananchi wa Mafia (MCB) lipo katika hatua za mwisho kuweka katika Mfumo wa kibenki.
12. Kamati Imetembelea Benki ya kwanza ya Wananchi Tanzania Mufindi Community Bank (MuccoBa) ili kusoma mbinu walizotumia wao kuweza kuanzisha Benki ya na ikapelekea Mafanikio Makubwa.
13. Kamati imefanya kikao baina yao,uongozi wa wilaya na wamafia wanaoishi Zanzibar kwa ajili ya kuwashawishi kununua hisa za Mafia community Bank, Hisa zenye thamani ya Tshs 39,400,000/= zimeahidiwa kununuliwa.
14. Kupitia Mwenge wa uhuru na sherehe za serikali za mitaa kamati imehamasisha wananchi wa Mafia kununua hisa za benki ya wananchi wa Mafia.
15. Kikao maalum kwa ajili ya kupitia mpango wa biashara(Business plan) kimefanyika na mpango wa biashara uko tayari kwa ajili ya kuhamasisha watu maalum na taasisi mbalimbali.
16. Vitendea kazi kwa ajili ya Benki ya Wananchi Mafia kama vile furniture na stationery tayari vimenunuliwa.
CHANGAMOTO:
1. Mwitiko hafifu wa wananchi wanaojitokeza kununua hisa kwa ajili ya Benki hii.
2. Elimu ndogo ya uwekezaji
3. Wadau wengi walioko nje ya Mafia kuwa na Mashaka hasa katika hatua ya kuanza wengi wanasubiri ianze kwanza.
4. Mtaji Duni
5. Vyama vya ushirika vingi vilivyopo Mafia havina Nguvu/Uwezo wa kifedha wa kununua hisa.
6. Ukosefu wa Mashirika/Taasisi /Kampuni zilizowekeza Mafia ambazo zingeweza kuwa mmoja wa wawekezaji wakuu.
7. Wengi walioahidi kununua hisa mpaka sasa hawajakamilisha ahadi zao
MIKAKATI:
1. Kupanua Wigo wa kuwafikia wadau wengi zaidi waliopo nje ya Mafia.
2. Kuzifikia Taasisi/Mashirika/Kampuni zinazofanya au zenye nia ya kufanya kazi Mafia na kuwahamasisha ktk ununuzi wa Hisa.
3. Kufanya Uhamasishaji zaidi kwa wananchi uhamasishaji utakaoenda sambamba na utoaji wa elimu kuhusu Manufaa ya Benki hiyo.
4. Kubainisha na kuwafikia watu Mashuhuri na wenye mwitiko chanya na kuchangia shughuli za maendeleo na kuwaomba kuchangia Mtaji wa benki.
5. Kuviimarisha Vyama vya ushirika vilivyopo ili navyo viweze kuwa sehemu ya wamiliki wa benki kwa kununua hisa.
6. Kutafuta Mashirika wahisani wanaoweza kuboresha huduma za kibenki vijijini na kuwaandikia Miradi ya kuomba kufanya Maboresho katika maeneo wanayoweza kusaidia.
HITIMISHO:
Ukiwa kama mdau muhimu wa maendeleo ya Mafia unaombwa kuchangia mtaji kwa ajili ya uanzishwaji Benki kwa ajili ya Maendeleo yetu na Mafia yetu kwani ukwamishaji wa hili unasababishwa na sisi wenyewe wamafia kwa kutokamilisha ahadi zetu kwa ajili kufikia lengo kwa ajili ya mtaji ambao unahitajika na Benki kuu ili kulikamilsha hili.
Naomba kuwasilisha.
Ahsante,
SALUM A.MAULID
MRATIBU-UANZISHWAJI WA BENKI YA WANANCHI MAFIA.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa