Translate in your language
Saturday, June 30, 2012
Ulimboka sasa aitesa Serikali *Yashindwa kutoa tamko la waliogoma *Madaktati ICU wapigania maisha yake Ulimboka sasa aitesa Serikali *Yashindwa kutoa tamko la waliogoma *Madaktati ICU wapigania maisha yake
Na Waandishi Wetu, Dodoma, Dar (kwa msaada wa Majira)
SERIKALI imekiri kuchanganywa na tukio la kutekwa na kujeruhiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka, ambapo Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, jana alishindwa kutoa tamko la Serikali kuhusu madaktari waliogoma bungeni mjini Dodoma, kama alivyoahidi juzi.
Bw. Pinda aliahidi kutoa tamko hilo wakati akijubu swali la papo kwa hapo kutokana na swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Bw. Freeman Mbowe.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Mbowe alitaka kujua Bw. Pinda anaizungumziaje kauli ya “litalo na liwe” na Serikali inachukua hatua gani za ziada kumaliza tatizo mgomo wa madaktari.
Juzi Bw. Pinda alilieleza bunge kuwa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kumaliza mgomo wa madaktari bila mafanikio na kuahidi kuwa kesho yake (jana), angetoa tamko la Serikali.
“Mheshimiwa Spika, nikiri kutamka liwalo na liwe lakini inawezekana neno hili limepewa tafsili nyingi, kilichokuwa kikinusumbua, jambo hili lipo mbele ya Mahakama Kuu, kama nitatoa kauli ni dhahiri nitaonekana mtovu wa taratibu zetu kikatiba.
“Ndioa maana nikafika mahali nikasema, katika mazingira yaliyopo nikieleza kinachoendelea na tunataka kufanya nini, viongozi wa muhimili mwingine watanilaumu, alisema Bw. Pinda.
Bw. Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi zaidi wa kauli ya “liwalo na liwe”, ambayo ilizua mjadala juzi bungeni huku Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee, akidai huenda ikawa na uhusiano na tukio la kutekwa Dkt. Ulimboka.
“Jana (juzi), nilimsikia dada yangu Mdee akiitafsili kauli hii vingine nikasema ni habari mbaya, wakati nikizungumze vile sikuwa nafahamu lolote bali nilichokisema, kilihusiana na mgomo wa madaktari na kuahidi kutoa kauli bungeni.
“Nilishauriana na vyombo vingine vya muhimili, ikaonekana
bado hatuwezi kutoa tamko wakati jambo hili limeahirishwa hadi mwezi ujao na mimi nikakubali ushauri huo,” alisema Bw. Pinda.
Bw. Pinda akizungumzia tukio la kutekwa Dkt. Ulimboka, alisema limemsikitisha na anamtakia kheri apone haraka kwani taratibu za kumaliza mgogoro uliopo ulikuwa ukienda vizuri.
“Kwanza nioneshe masikitiko yangu juu ya jambo hili na mimi namtakia kila la kheri apone haraka, ni bahati mbaya tu kwa sababu mchakato ulikuwa unaenda vizuri, tuliamini tungefika mahali tungeelewana vizuri tu, taarifa ambazo nimeletewa na mazingira ya tukio lenyewe yana utata mkubwa.
“Kila mtu ana hisia zake, wengine wanadhani ni Serikali...wengine vinginevyo...tumeagiza uchunguzi ufanywe haraka ili ukweli uweze kubainika, Dkt. Ulimboka tumekuwa naye muda wote.
“Tumeshirikiana vizuri katika jambo hili hadi tukafika mahakamani, vyombo vyote vinajua mgogoro uliopo upo katika hatua gani, kidogo inanipa tabu kama tukio hili litahusishwa na Serikali ili iweje! njia rahisi tusubiri uchunguzi wa kina,” alisema Bw. Pinda
Akijibu swali la Bw. Mbowe la kumtaka aeleze hatua ambazo Serikali itazichukua kuokoa maisha ya wananchi katika hospitali za rufaa ambako madaktari wamegoma, zikiwemo za Bugando, Mbeya, KCMC na Muhimbili, Bw. Pinda alisema Serikali imeomba Hospitali ya Jeshi Lugalo itumike ili kuhakikisha wagonjwa hawakosi huduma na hospitali ndogo zitumike kupunguza madhara.
Aliongeza kuwa, Serikali imechukua uamuzi wa kuwarudisha madaktari waliostaafu ili kukabiliana na hali hiyo pamoja na wale waliopo wizarani warudi hospitalini kutoa huduma.
Lissu ataka Pinda ajiuzulu
Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Lissu, alisema madaktari walipogoma Februari mwaka huu, suala hilo alilishughulikia Mwenyewe na Taifa likatangaziwa mgomo hautajirdia tena.
Alisema kabla miezi mitatu haijapita, madaktari wamegoma tena hivyo kwanini Bw. Pinda asijiuzulu kwa kushindwa kutatua matatizo ya madaktari
Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema; “Mheshimiwa Spika, yako mazingira unayoweza kuwajibika lakini si lazima yakawa yote, mimi sioni kama hili ni moja ya maeneo hayo, nakiri kuwa tatizo hili ni la muda mrefu lakini nimefanya jitihada kubwa kulimaliza na lina changamoto nyingi kwa sababu mambo yameingiliana.
Mgomo wahusishwa na ufadhili
Akiuliza swali kwa Bw. Pinda, Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Matha Mlata, alitaka kujua kama mgomo huo unachochewa na vikundi vya watu ambavyo vinawatumia baadhi ya madaktari kwa kuwapa fedha ili wahamasishe mgomo ili nchi isitawalike.
Aliitaka Serikali ichunguze uvumi huo ili kuokoa maisha ya
Watanzania wanaokufa.
Ajibu swali hili, Bw. Pinda alisema, mgogoro huo una maneno mengi kwani hata yeye amesikia maneno hayo lakini wameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia ili kujua kama yana ukweli.
Hali ya Dkt. Ulimboka
Hali ya Dkt. Ulimboka anayeendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inaendelea vizuri ambapo hivi sasa amehamishiwa katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), chini ya jopo la madaktari ambalo linaongozwa na Daktari Bingwa, Profesa Joseph Kihamba.
Ulinzi kwa ajili ya usalama wa Dkt. Ulimboka, imeimarishwa na madaktari wenyewe kwa kupeana zamu hali inayodhihirisha kuwa, bado wana mashaka na mazingira ya tukio lililomkuta mwenzao.
Kwa mujibu wa Profesa Kihamba, hali ya Dkt. Ulimboka imeimarika tofauti na juzi baada ya kuanza kuanza kutambua watu.
“Tuna matumaini makubwa kuwa atanyanyuka na kuendelea na shughuli zake kama kawaida, hali yake inatupa matumaini,” alisema Profesa Kihamba.
Uongozi wa MOI wanena
Ofisa Uhusiano wa Taasisi ya Mifupa (MOI), Bw. Almas Jumaa, alisema Dkt.Ulimboka amelazwa katika taasisi hiyo ingawa huduma zingine zote zimesitishwa isipokuwa zile za dharura.
Alisema hakuna huduma za kliniki isipokuwa za dharura kwa sababu madaktari haawapo.
Tume ya Serikali
Jumuiya ya Madaktari Tanzania, imesema haina imani na tume iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuchunguza mazingira yaliyosababisha Dkt. Ulimboka kujeruhiwa kwa madai hawana imani nayo.
Katibu wa jumuiya hiyo, Bw. Edwin Chitage, alisema wanahitaji tume huru ambayo itafanya uchunguzi huo lakini si tume iliyoundwa na polisi kwani tangu kutokea tukio hilo, baadhi ya madaktari hasa wa Mkoa wa Dodoma wameanza kupata ujumbe wa vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana.
“Tunawaomba madaktari wote nchi nzima kuendelea kushikamana hadi Serikali itakapotutimizia madai yetu bila kuogopa vitisho vinavyotolewa na baadhi ya watu,” alisema
Kutokana na hali hiyo, jumuiya hiyo imesisitiza hakuna njia nyingine ya kumaliza mgogoro huo zaidi ya kukaa meza moja na kufanya mazungumzo na Serikali.
Alisema katika kipindi hiki kigumu, kimewafanya madaktari nchi nzima kuungana pamoja bila ya kuvuruga amani ya nchi na kuwaomba madaktari kuwa watulivu ili wapate haki yao.
Tume ya Haki za Binadamu
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa taarifa ya kusikitishwa na kitendo cha kinyama cha kupigwa Dkt. Ulimboka na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande, kwani kitendo hicho kimekiuka haki ya msingi ya binadamu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jaji mstaafu, Bw. Amiri Manento, ambaye ni Mwenyekiti wa THBUB, ilisema kwa mujibu wa sheria ni kumteka na kumtendea mtu vitendo vya kinyama na udhalilishaji wa utu wake.
Alisema THBUB inalaani vikali kitendo hicho ambacho kimemnyima Dkt. Ulimboka haki yake ya kikatiba ya kuheshimiwa utu wake na kutofanyiwa vitendo vya kinyama na kudhalilisha.
Aliongeza kuwa, tume hiyo inatoa mwito kwa wananchi na vyombo vya dola kuheshimu sheria, utawala wa sheria, haki za binadamu, utawala bora na kuitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliofanya kitendo hicho cha kinyama.
TUCTA yang'aka
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limeitaka Serikali kuwajibika ipasavyo na kutoa tamko thabiti juu ya tukio, lililompata Dkt. Ulimboka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa TUCTA, Bw. Nicholas Mgaya, alilaani kauli iliyotolewa na Bw. Pinda, bungeni juzi kuwa Serikali itatoa msimamo wake na liwalo na liwe.
“Serikali lazima ichunguze vyombo vyake vya usalama, msitu wa Mabwepande unajulikana kwa mabaya hivyo lazima itoe tamko,” alisema Bw. Mgaya.
CUF yadai kukosa imani na tume
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hakina imani na tume iliyoundwa kuchunguza kipigo cha Dkt. Ulimboka, badala yake kimeshauri kazi hiyo ifanywe na vyombo vingine vilivyo huru kwa kushirikisha wanaharakati na asasi za kiraia.
Naibu Mkurugenzi Habari na Uenezi wa CUF Taifa, Bw. Abdul Kambaya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira,
Alisema CUF haina imani na chombo hicho kutokana na mazingira ya kutatanisha kuhusu gari lililotumika kumteka Dkt. Ulimboka ambalo linadaiwa halikuwa na namba.
Aliongeza kuwa, chama hicho kimesikitishwa na tukio la kutekwa kiongozi huyo, huku Serikali ikiwa na mgogoro na wanataaluma hao ambao wanadai haki zao.
“CUF hatuna imani na tume hii kwani gari lililohusika kufanya utekaji huu ina maana polisi waliokuwa doria hawakuliona barabarani hadi lifike Mabwepande,” alisema Bw. Kambaya.
CHADEMA yahoji intelejensia ya IGP
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimehoji ilikuwaje intelejensia ambayo Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Said Mwema, ambayo amekuwa akiitumia kudhibiti maandamano ya chama hicho kwa madai ya kuashiria uvunjifu wa amani isitumike kuwajua watu waliomteka Dkt. Ulimboka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Mafunzo na Organization wa chama hicho, Bw. Benson Kigaila, alisema mipaka ya intelejensia hiyo inaishia katika maandamano ya CHADEMA badala ya tukio hilo.
Alisema hilo sio tukio la kwanza kutokea nchini kwa watu wanaodai haki zao kufanyiwa vitendo kama hivyo na kuundwa tume ambazo hazina majibu kwa wananchi.
Imendika na Stella Aron, Rehema Maigala, Mariam Mziwanda, Goodluck Hongo, Grace Ndossa.
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa