Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige |
Waandishi Wetu SIASA za minyukano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaendelea kushika kasi na sasa wabunge wanne wa chama hicho wanatajwa kuwa wamekalia kuti kavu kutokana na kuanza kujadiliwa na vikao mbalimbali kwa matendo yao yanayoonekana kukiudhi chama hicho tawala.
Miongoni mwao ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye tangu alipong’olewa katika nafasi hiyo katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete Mei 4, mwaka huu amekuwa akitoa shutuma nzito dhidi ya CCM na baadhi ya makada wake.
Tayari chama hicho kimeonyesha kutoridhika na kauli hizo za Maige baada ya juzi Katibu wa Siasa na Uenezi wilaya ya Kahama, Mirco Ng'wanangolelwa kutoa taarifa ya kukanusha kauli zake dhidi ya chama na viongozi. "Tunakemea na kulaani utaratibu huu wa watu kukurupuka na kushutumu viongozi wa chama chetu kwa staili aliyotumia Maige. Lengo lake sio jema na wala halina nia ya kujenga chama chetu bali ni kubomoa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Tangu atimuliwe uwaziri, Maige amekuwa akitoa shutuma nzito kuhusu kufukuzwa kakwe kwamba kulitokana na majungu na fitina za wana CCM wenzake na kwamba kwa mtindo huo chama hicho kiko hatarini kufa. Pia mbunge huyo alimshambulia Katibu wa Itikadi na Uenenzi wa CCM, Nape Nnauye kwamba amekuwa akikiharibu chama hicho kutokana na kauli zake ambazo alisema zinakiua chama badala ya kukijenga, kauli ambayo hata hivyo ilikemewa na CCM Kahama.
Wengine ambao Maige amewashambulia hadharani ni Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii, James Lembeli kwamba wanahusika na kusherehekea kung’olewa kwake.
Habari ambazo Mwananchi limezipata kutoka Kahama na Shinyanga Mjini, zinasema Maige ambaye pia ni Mbunge wa Msalala atajadiliwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya ambacho kimepangwa kufanyika Jumanne ijayo wilayani humo. Habari zaidi zinasema kikao hicho ni cha dharura na ajenda zake bado ni siri ya Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Adam Ndalahwa ambaye ametoa maelekezo kiitishwe. Ng'wanangolelwa alithibitisha kuitishwa kwa kikao hicho lakini hakuwa tayari kuzungumzia ajenda kwa maelezo kwamba anayezifahamu ni Ndalahwa. Kuhusu suala la Maige kujadiliwa Ng'wanangolelwa alisema: “Hilo kwa kweli sifahamu maana sisi kama chama wilaya tumepokea maelekezo kwamba Katibu wa CCM wa Mkoa atafika kuzungumza na Kamati ya Siasa, kwa hiyo kama hiyo ajenda ipo au haipo mimi sifahamu”.
Kwa upande wake Ndalahwa alikiri kutaka kukutana na Kamati ya Siasa ya Wilaya lakini ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kichama wilayani humo, lakini akakanusha kuwapo kwa ajenda ya kumjadili Maige.
“Mimi ni Katibu wa CCM wa Mkoa, na nimepanga kwenda kwenye ziara ya kufuatilia chaguzi zetu ndani ya chama, tena nilipanga ratiba hii hata kabla ya Maige hajaanza ziara kwenye jimbo lake,”alisema Ndalahwa.
Sakata la Maige ni dhahiri sasa linachukua sura ya siasa za makundi ndani ya CCM kwani kauli ambazo zinafanya ajadiliwe amekuwa akizitoa kwenye mikutano ambayo imekuwa ikihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja.
Waliotaka Pinda ang’olewe Wakati hayo yakiendelea, wabunge wengine watatu wa CCM ambao walisaini kusudio la kumng’oa madarakani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda nao huenda wakajadiliwa kutokana na hatua yao hiyo. Wabunge hao Deo Filikunjombe (Ludewa), Nimrodi Mkono (Musoma Vijijini) na Alphaxard Kangi Lugora (Mwibara) walisaini hoja yenye kusudio la kutaka kumng’oa Waziri Mkuu, Pinda ambalo lilikuwa likitaka kuwasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.
Habari zinasema suala hilo ni moja ya mambo ambayo yaliwagawa wajumbe wa kikao cha Halmshauri Kuu ya CCM (Nec) kilichofanyika mwezi uliopita mjini Dodoma, lakini hakuna mwafaka wowote uliopatikana. “Wapo ambao tulitaka hawa wabunge wachukuliwe hatua za kinidhamu, lakini pia wapo ambao walikuwa na msimamo kwamba wabunge hao walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kikatiba, mjadala ulikuwa mkali lakini hitimisho lilikuwa kwamba suala hilo lirejeshwe kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM,”alisema mmoja wa wajumbe wa NEC.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alithibitisha suala hilo kijadiliwa ndani ya kikao hicho na kwamba ni kweli limerejeshwa katika kamati ya wabunge wa chama hicho. “Kimsingi hoja zote zinaanzia pale bungeni, na hata hayo ambayo yanadaiwa kuwa ni makosa yalifanyika katika mazingira ya Bunge, sasa kama chama tuliona ni vyema tuiachie kamati ya wabunge wetu, nao wataangalia kwa kutumia kanuni zao kama wataona kuna kosa, basi watachukua hatua,”alisema Nape na kuongeza: “...wanatakiwa watumie kanuni zao sasa inategemea zinawaelekeza vipi, kama wanaweza kutoa adhabu sawa, kama wanalifoward (wanalileta) kwetu nasi tutalipangia utaratibu mwafaka, lakini lazima lianzie huko kwa wabunge wenyewe, sisi hatuwezi kuwaingilia”. Katibu wa Wabunge wa CCM, Janester Mhagama kwa upande wake, alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo wa NEC na kwamba baada ya kuarifiwa, angeweza kulizungumzia.
“Kwa bahati mbaya katika NEC iliyopita sikuweza kuhudhuria nilikuwa na matatizo ya kifamilia, lakini niseme tu kwamba kama watatuletea kama walivyosema, basi kanuni zetu zipo na tutaangalia zinasemaje kuhusu hilo,”alisema Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho. Mhagama ambaye pia ni mmoja wa wenyeviti wa Bunge aliweka wazi kwamba anachofahamu yeye ni kwamba wabunge hao walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kikatiba lakini akakumbusha kuwa chama nacho kina nafasi yake.
Aliongeza: “Ndiyo maana nimesema lazima twende kwenye kanuni zetu za Bunge halafu pia tuangalie kanuni zetu za wabunge wa CCM, tutapata mwafaka hakuna haja ya kuwa na haraka”. Akizungumzia suala hilo, Filikunjombe alisema kuwa aliyoyazungumza bungeni ikiwa ni pamoja na kusaini fomu ya kutokuwa na imani na waziri mkuu ni kwa maslahi ya Serikali na CCM.
“Ukweli ni kwamba nilichokizungumza sikumsingizia mtu na nilifanya hivyo kwa maslahi ya Serikali yangu na chama change,” alisema Filikunjombe. Alifafanua kwamba wanaomuona adui na kutaka achukuliwe hatua na chama, wao ndio maadui namba moja wa Serikali na CCM.
“Rais Jakaya Kikwete mwenyewe aliwahi kukiri wazi kuwa amefurahishwa na mawazo ya wabunge waliyoyatoa kuhusu suala zima la kuwajibishwa kwa mawaziri”. Aliongeza, “Unajua watu wanadhani kwamba wenye uchungu na nchi hii ni wapinzani pekee…,hilo jambo sio kweli nchi hii ni yetu wote”.http://www.mwananchi.co.tz/component/content/article/37-tanzania-top-news-story/23500-ccm-waanza-kumkaanga-maige.html
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa