Wanafunzi hawa wanaandaa chakula nje kidogo ya nyumba waliyopanga. Baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule za sekondari za kata wilayani Kisarawe, wanalazimika kupanga mtaani kutokana na ukosefu wa mabweni.Picha na Pamela Chilongola Pamela Chilongola
HUKU mwili wake ukiwa umelowa jasho kutokana na jua kali la mchana, Sikitu Kamba amekaa chini ya mti wa mvule, anajisaili moyoni kuhusu mtu anayeweza kumfuata kumuomba ushauri baada kuhisi mabadiliko ya ghafla katika mwili wake.
Akiwa na wasiwasi mwingi juu ya hali hiyo, aliamini kama mama yake mzazi angekuwa hai, angeweza kumwomba ushauri juu mabadiliko hayo katika mwili wake huo mteke ambao ndiyo kwanza umetimiza miaka 15 ya kuishi kwake duniani.
Licha ya hali hiyo, Sikitu anayeishi kijiji cha Mtamba kilichopo wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, alifanikiwa kumaliza elimu ya msingi. Lakini miezi mitatu baadaye aligundua kuwa alikuwa mjamzito, hivyo kufifisha ndoto yake ya kuendelea na masomo ya sekondari.
Kwa mtazamo wake, anaamini kama asingeshiriki kile anachokiita ‘mchezo wa kitoto’ asingekuwa mzazi akiwa na umri mdogo…. “Siamini kwamba mchezo wa kitoto na kale kavulana ndiyo umenipa hali hii,”
Anasema mama yake alifariki akimwacha na umri wa miaka 13, hivyo hakukuwapo na mtu wa kumwongoza katika familia ya watoto watano akiwamo yeye ambaye ni mtoto wa kike pekee.
Anasema hata shuleni walimu wengi walikuwa wanaume, hali anayodai iliwanyima fursa wanafunzi wa kike kuwahusisha katika masuala mbalimbali ikiwamo kuomba ushauri wa afya zao.
“Naamini kama tungekuwa na walimu wa kike wa kutosha, ningekuwa nimejifunza mengi juu ya kujitunza kama msichana. Ujinga wa maumbile ulinifanya nikutane kimwili na mvulana wa kijijini bila ya kutambua athari zake,” anaeleza na kuongeza.
“Mwalimu wa kike anapokuwepo shuleni, anamsaidia mwanafunzi wa kike kumpa elimu ya kujitambua ili aweze kuepukana na mimba za utotoni.’’
Kimsingi, shule nyingi wilayani Kisarawe zina walimu wachache wa kike, hali ambayo baadhi ya watu wanasema inachangia ongezeko la wanafunzi wanaoacha shule kwa sababu ya ujauzito.
Mathalani, takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2010 na 2011, wanafunzi zaidi ya 100 walipata ujauzito.
Wakuu wa shule za sekondari za kata wilayani humo, wanasema ongezeko la wanafunzi katika shule zao haliendani na upatikanaji wa walimu hasa wa kike, jambo linalowafanya wanafunzi wa kike kukosa elimu ya kujitambua.
Baadhi ya shule kama vile Kibuta haina mwalimu hata mmoja wa kike, huku Chole, Mfulu na Masaki zikiwa na mwalimu mmoja pekee.
Aidha, wakuu hao wanasema ukosefu wa mabweni nao umekuwa chachu ya wanafunzi kupata ujauzito, kwa kuwa wengi wamekuwa wakiishi mbali na shule.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibuta, Musa Juma anasema mwaka 2009 wanafunzi zaidi ya 20 walipata mimba kwa sababu mbalimbali ikiwamo kubwa ya kupata vishawishi kwa kusafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shule.
“ Wanafunzi hao wanakuwa wamechoka na lazima wanakutana na vishawishi vya kila aina kama kupewa lifti ya usafiri na kupewa ofa ya chakula. Kama hivi sasa nimeletewa taarifa kuna mwanafunzi wa kidato cha tatu ni mjamzito, ”anasema Juma
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Maneromango, Lina Isaya anaisihi Serikali kama msimamizi wa shule za kata, kujenga hosteli ili kuepusha matukio ya wanafunzi wa kike kupata ujauzito kutokana na kupanga mitaani wanapokumbana na vishawishi mbalimbali.
Tamko la Serikali
Ofisa Taaluma wa Wilaya ya Kisarawe, Gideon Shangwe anasema wilaya yake ina utaratibu wa kutoa mafunzo kuhusu Ukimwi, lakini uendeshaji wake umeshindwa kuzaa matunda stahiki kutokana na kukosekana kwa walimu wa kike katika shule nyingi.
Ni kwa sababu hii anasema wanafunzi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu namna bora ya kuepukana na vishawishi vinavoweza kuchangia wakapata magonjwa ya zinaa na Ukimwi.
Hata wale wanafunzi wachache wanaobahatika kupata elimu hiyo, wengi wanashindwa kuifanyia kazi na kujikuta wakijitumbukiza katika uhusiano kwa sababu ya ugumu wa maisha unaozikabili familia zao.
Mkuu wa wilaya hiyo, Khanifa Karamagi anasema ujenzi wa mabweni unatakiwa kuongezwa kwa kasi ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaingia kwenye mabweni kupunguza ongezeko la mimba.
“Kuna umuhimu wa kuanzisha sheria zitakazowadhibiti wazazi wanaokataza wasichana kukaa katika mabweni….. Wazazi wanatakiwa kuwa makini na watoto wao na wasikubali kudanganywa na wanafunzi kwa kudai gharama ni kubwa,”anasema.
Kwa kuwa wanafunzi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda shule, huku wakikosa chakula, jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi wa kike kuacha shule, Mwenyekiti wa kitongoji cha Kibaoni, Kata ya Kisarawe, Helen Matoka anasema sasa ni wakati mwafaka kwa shule kuwa na mashamba yatakayozalisha chakula kwa wanafunzi.
“Ifike mahala Serikali irudishe elimu ya kujitegemea ili wanafunzi waweze kupata elimu ya kujitegemea na pia walime na kupata mazao kwa kupitia somo hilo,”anasema Matoka.
DONDOO KUHUSU MIMBA KISARAWE
Sekondari ya Masaki, mimba 11 mwaka 2o11 sekodari ya Kibuta, mimba 21 mwaka 2010 hadi 2011 Sekondari Jenguo, mimba 20 mwaka 2011,Sekondari ya Maneromango, mimba 3 mwaka 2011, Sekondari Chole , mimba 15 mwaka 2011, Sekondari ya Makurunge, mimba 23 mwaka 2011 , Sekondari ya Mfuru, mimba tano mwaka 2011 |
No comments :
Post a Comment
here u,re comments/acha ujumbe wako hapa